Katika Dilexi Te:Pendo ni wajibu.Kanisa haliweki mipaka ya kupenda
Na Padre Angelo Shikombe – Vatican.
Mpendwa msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuhitimishe tutafakari hii tukielezea changamoto endelevu na nini kifanyike. Ndugu msomaji/ msikilizaji, kwetu sisi wakristo, tatizo la maskini hugusa kiini cha imani yetu. Mtakatifu Yohane Paulo II alifundisha kuwa upendo wa pekee kwa maskini ni muhimu na umeshakuwa utamaduni na sehemu ya kimapokeo ya Kanisa. Unaisukuma jamii kutilia maanani uwepo wa maskini licha ya maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi.
Kwa wakristo, maskini si kundi la kijamii, lakini ni sehemu ya mwili wa fumbo la Kristo. Haitoshi kukiri fundisho la umwilisho wa Mungu kwa kuegemea tu ujumla wake, ili kuzama kwenye fumbo hili kuu, tuna haja ya kuelewa wazi kwamba Bwana alitwaa mwili wenye njaa na kiu, na akauishi udhaifu wetu katika kifungo cha umaskini. Kanisa maskini kwa ajili ya maskini huanza kwa kuugusa mwili wa Kristo. Tunapougusa mwili wa Kristo, tunaanza kuelewa kitu fulani, kuelewa umaskini huu ni nini, ni umaskini wa Bwana ambao si bure. Kwa asili yake Kanisa hushikamana daima na maskini, waliotengwa, walioko pembezoni na wote waliosahaulika. Maskini ndio moyo wa Kanisa kwa sababu “imani yetu katika Kristo, ambaye alifanyika maskini, na daima alikuwa karibu na maskini na waliotengwa, ndiyo msingi wa kujali kwetu katika kutetea maendeleo fungamano ya wanajamii waliosetwa. Katika mioyo yetu, tuna kiu ya kujibu hitaji hili, lenye asili ya neema ya msaada ndani ya kila mmoja wetu, na hivyo si utume wa wachache tu.
Ndugu msomaji/msikilizaji, wakati fulani, vuguvugu au makundi ya kikristo yameibuka yenye nia ndogo au kutopendezwa kabisa na manufaa ya pamoja ya jamii hususan, ulinzi na maendeleo ya watu walio katika mazingira magumu zaidi. Hata hivyo tusisahau kuwa, dini, hasa dini ya kikristo, haiwezi kuwekewa mipaka kama taasisi binafsi, kana kwamba waamini wake hawana jukumu la kupaza sauti zao ili zisikike kuhusu matatizo yanayoathiri asasi za kiraia na masuala yanayoihusu jumuyiya nzima. Kwani jumuiya yoyote ya Kanisa, itakayofikiri inaweza kwenda kinyume na kutokuwa na ushirikiano mzuri na maskini katika kuwasaidia kuishi kwa heshima utu wao, iko hatarini kuanguka. Inaweza kupeperushwa kwa urahisi na kuingia katika ulimwengu wa kiroho unaofichwa na mazoea ya kidini, mikutano isiyo na tija na mazungumzo matupu. Hata hivyo mengi yanazungumzika kuhusu masuala ya kijamii au namna ya kuikosoa serikali. Wala si suala la kutoa tu huduma ya ustawi wa jamii na kufanya kazi ya kuleta haki-kijamii. Wakristo wanapaswa kuwa makini na aina mpya ya kutokujali wanapowahudumia maskini. Kwa kweli, “ubaguzi mbaya zaidi ambao maskini wanateseka ni ukosefu wa huduma za kiroho… Upendeleo wetu lazima uwe na ependeleo kwa maskini na hata katika utoaji wa huduma za kiroho. Usikivu kwa huduma za kiroho kwa maskini utiliwe mkazo, kwani hata miongoni mwa wakristo, kunaweza kuwa na chuki fulani kutokana na ukweli kwamba tunaona ni rahisi kuwafumbia macho maskini.
Ndugu msomaji/ msikilizaji, kuna wanaojidai kujihusisha tu na mafundisho ya Kanisa huku wakitenganisha kipengele hiki cha kidini na maendeleo shirikishi, pengine huenda mbali zaidi wakisema kwamba ni kazi ya serikali kuwatunza maskini, au kwamba si muhimu zaidi kuwapa chochote maskini kwani ingetosha tu kuwaelimisha wajitegemee na wafanye kazi wenyewe. Wakati fulani, takwimu za uwongo za kisayansi hutumika kuunga mkono madai ya kwamba uchumi wa soko huria ni suluhisho la kudumu la tatizo la umaskini duniani. Wakati mwingine tunaweza pia kushawishika tuchague kufanya kazi za kichungaji na wasomi tu, eti kwa kuwa tunaweza kupoteza muda tukijihusisha na maskini, eti huenda ingekuwa bora kuwajali matajiri, wenye ushawishi na wataalamu, ili kwa misaada yao wa kitaaluma tuweze kutatua matatizo ya kijamii na Kanisa kubaki na ulinzi. Ni rahisi kutambua hila ya kidunia nyuma ya hili pazia, ambayo huenda ikatuongoza kutazama ukweli kupitia lenzi hafifu, zisizo na mwanga wowote kutoka kwa Mungu, na kutusaidia kusitawisha uhusiano unaotuweka salama na kulinda maslahi yetu binafsi.
Ndugu msomaji/msikilizaji, katika kipengele cha utoaji wetu wa ukarimu, Papa Leo XIV angependa kuhitimisha wosia wake kwa kusema jambo fulani kuhusu ukarimu, ambalo halipewi upendeleo hata miongoni mwa waamini. Sio tu kwamba inafanywa mara chache, lakini hata wakati mwingine hudharauliwa. Baba Mtakatifu Leo anasema kwamba njia muhimu zaidi ya kuwasaidia wasiojiweza ni kuwasaidia katika kujipatia maisha mazuri, ili waweze kuishi kwa heshima zaidi kwa kukuza uwezo wao na kuchangia kwa pato lao. Kwa maana hii, “ukosefu wa kazi unamaanisha mengi zaidi ya kutokuwa na vyanzo thabiti vya mapato. Kazi yaweza pia kuwa ni hicho, lakini ili kuwa sahihi zaidi. Tunapofanya kazi tunakuwa watu walio kamili, utu wetu unastawi, vijana hupevuka wanapofanyakazi. Mafundisho ya kijamii ya Kanisa yanakazia kila mara juu ya kazi ya binadamu katika kushiriki kazi ya Mungu ya uumbaji inayoendelea kila siku, kwa vielelezo vya mikono, akili na mioyo ya wafanyakazi. Kwa upande mwingine, ambapo hili haliwezekani, hatuwezi kuwatelekeza wengine walio katika mazingira hatarishi na kwa hatima ya kukosa mahitaji ya maisha yenye heshima. Kwa hiyo, ukarimu kwa sasa ni njia muhimu ya kuwasiliana, kukutana na kuhurumiana pamoja na wale wasiobahatika.
Ndugu msomaji/msikilizaji, wadau wa ukarimu wanaujua vyema ukweli huu kwamba kujitolea hakumwondoi mtu uwezo wake wa kimamlaka, majukumu yake, wajibu wake, wajibu wa vyombo vya serikali kuwahudumia maskini, au kupunguza juhudi zinazofaa za kuhakikisha haki inatendeka. Ukarimu unatupa nafasi ya kushirikiana na maskini, kuangaliana machoni, kuwagusa na kuwashirikisha maisha yetu. Kwa vyovyote vile, ukarimu ni sadaka, hata kama ni wa kiasi kidogo, huleta mguso wa huruma katika jamii, vinginevyo unaweza kugeuka kuwa maonesho na harakati za kujinufaisha binafsi. Katika kitabu cha Mithali kuna sehemu inasema: “Heri wakarimu kwa maana wanagawana chakula chao na maskini”. Agano la kale na Agano jipya lina nyimbo zinazosifia ukarimu zikituasa kuwa na subira na mtu aliye katika hali duni, na usimcheleweshee zawadi yako. Hifadhi hazina yako, nayo itakuokoa na kila balaa. (Sir 29:8, 12) Yesu alienda mbali zaidi akisema: “Uza ulivyo navyo na uwape maskini. Jiwekeeni hazina yenu mbinguni ambako nondo wala mwivi hawaharibu” (Lk 12:33).
Ndugu msomaji/ msikilizaji, Mtakatifu Yohane Chrysostom anajulikana kwa msemo wake usemao: “Ukarimu ni bawa la sala. Na kama hautasali kwa mbawa, huwezi kuruka. Katika mkondo huo huo, Mtakatifu Gregory wa Nazianzus alihitimisha mojawapo ya hotuba zake maarufu kwa maneno haya: “Ikiwa unafikiri kwamba nina jambo la kuteta nanyi, watumishi wa Kristo, ndugu na warithi, na tumtembelee Kristo wakati wowote tupatapo; tumtunze, tumlishe, tumvishe, tumkaribishe, na kumheshimu, si wakati wa chakula tu, kama wengine wafanyavyo. Tuumtie mafuta, kama Mariamu alivyofanya kwa maziko yake, kama Yusufu wa Arimathaya kwa kuandaa mazishi yake, au kama Nikodemo, ambaye alimpenda Kristo ki-ndumilakuwili, au kwa kumpa dhahabu, uvumba na manemane, kama Mamajusi walivyofanya na wengine wote. Bwana wa wote anataka rehema, na si sadaka... Basi na tumuonee huruma katika nafsi za maskini na wale ambao bado wanalala barabarani jalalani, na madarajani, ili tutakapoyaacha maisha haya watupokee katika makao ya milele.
Ndugu msomaji/msikilizaji, upendo wetu na imani yetu inahitaji kusitawishwa daima, na tunafanya hivyo kwa matendo yetu. Kubaki katika nadharia, huku tukishindwa kutekeleza kwa vitendo vya upendo na ukarimu, kunaweza kupelekea hata kupoteza matumaini na matamanio yetu. Kwa sababu hii, sisi wakristo tusijibandue kwenye ukarimu, bali tuendelee kuwa wakarimu kwa hakika tutapata ufanisi zaidi. Ni heri kitu fulani kuliko kutofanya kabisa. Kwa namna yoyote ile, ukarimu utawagusa na kulainisha mioyo yao migumu. Hautakuwa suluhisho la tatizo la umaskini duniani, lakini bado utawasaidia kama utatolewa kwa weledi na utashi kama alama ya uwajibikaji wa kijamii.
Kwa upande wetu, tunahitaji kutoa ukarimu kama njia ya kunyoosha mkono na kuugusa mwili unaoteseka wa maskini. Upendo wa kikristo huvunja kila kizuizi, huwaleta karibu wale waliotengana, hukaribisha wageni, na kupatanisha maadui. Ukarimu huziba mashimo ambayo kibinadamu haiyazibiki, na kujipenyeza hadi kuziba mipasuko iliyofichika zaidi ya kijamii. Kwa asili yake, pendo la kikristo ni la kinabii: hufanya miujiza na halina mipaka. Huwezesha kisichowezekana. Pendo ni mtazamo na ni wajibu. Kanisa lisiloweka mipaka ya kupenda, lisilojua maadui, ila tu linaona ndugu wa kuwapenda, ndilo Kanisa ambalo ulimwengu unahitaji leo. Kupitia kazi yako, juhudi zako za kubadilisha miundo ya kijamii isiyo ya haki au ishara yako ya ukaribu, na misaada yako, maskini watakuja kutambua kwamba maneno ya Yesu yanamhusu kila mmoja wao yaani; “Nimekupenda wewe” (Ufu 3:9).
Ndugu msomaji/msikilizaji, tumefikia hitimisho la waraka huu wa kitume Papa Leo XIV, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.