Tafuta

"Heri Maskini wa roho maana Ufalme wa Mbingu ni wao." "Heri Maskini wa roho maana Ufalme wa Mbingu ni wao."  (@Vatican Media)

Katika Dilexi Te:ukosefu wa usawa ni chanzo cha matatizo ya kijamii

Jamii hutengwa ikiwa taasisi zake za kijamii, uzalishaji na matumizi hayana dhamira safi na kielelezo cha muungano na mshikamano kati ya watu.Tunahitaji kujitolea zaidi kutatua vyanzo vya mifumo ya umaskini.Na Injili inabaki kuwa mhimu katika udumifu wa mahusiano binafsi na mahusiano na Bwana kwa ajili ya ufalme wa Mungu kupitia Maskini.

Padre Angelo Shikombe – Vatican.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tutafakari sura ya nne inayojikita katika historia endelevu na hasa miundo ya dhambi inayoleta umaskini na ukosefu wa usawa uliokithiri

Ndugu msomaji/ msikilizaji, huko Medellín, Maaskofu walijitangaza wenyewe kuwapendelea maskini: “Kristo mwokozi wetu hakuwapenda tu maskini, pamoja na kuwa tajiri, alijifanya maskini.’ Akaishi maisha ya kimaskini, akihubiri ukombozi wao, na akaanzisha Kanisa lake likiwa ni ishara ya umaskini kati yetu. Ndugu zetu wengi maskini wanalilia haki, mshikamano, ushuhuda, majitoleo na juhudi zinazoelekezwa kutokomeza janga hili. Maaskofu walitangaza kwa ushujaa kabisa kwamba ili Kanisa, liwe aminifu kikamilifu kwa wito, lazima si tu kushiriki hali ya maskini, lakini pia kusimama upande wao na kufanya kazi kikamilifu kwa ajili ya maendeleo yao. Likikabiliwa na hali ya umaskini uliokithiri katika bara la Amerika ya kusini, mkutano wa Puebla ulisisitiza uamuzi wa Medellín wenye sauti ya kinabii kwa maskini huku ukilaani tabia ya ukosefu wa haki kama dhambi ya kijamii. Upendo una nguvu ya kubadili uhalisia; ni nguvu ya kweli ya mabadiliko ya kihistoria. Ni chanzo ambacho lazima kihamasishe na kuongoza kila juhudi za upantanisho na hufanya hivyo kwa haraka.

Ndugu msomaji/msikilizaji, ni matumaini yake Papa Leo XIV kuona kuwa wanasiasa wanakuwa na uwezo wa kufanya mazungumzo yenye lengo la kuponya mizizi ya ndani kabisa na sio tu kwa kujionesha. Ni jambo la kusikiliza kilio cha mataifa yote, hasa watu walio maskini. Ni lazima tuendelee, tena tukemea udikteta wa kiuchumi unaoua, na tutambue kuwa wakati mapato ya watu duni yanaongezeka kwa kasi, vivyo hivyo pengo linazidi kukua kati ya walio wengi kutokufurahia fursa za maisha. Tofauti hii ni matokeo ya itikadi zinatetea uhuru kamili wa masoko na tafiti za kifedha. Kwa hiyo, hawataki kuwepo kwa usawa kati ya nchi na nchi ulio kwa manufaa ya wote, na kutoingilia kabisa maamuzi yao. Udhalimu mpya unazaliwa usionekana na mara nyingi ni wa kifadhila, ambao pole pole hujiwekea sheria na kanuni zake.  Nadharia ni nyingi mno zinazodadafua uhalali wa mikakati ya kiuchumi wa kisasa zenye soko lisiloonekana lenye kutatua kila kitu. Katika waraka wake wa Dilexit Nos, Papa Fransisko alikumbusha kwamba dhambi ya kijamii hujenga “muundo wa dhambi jamii” ndani ya jamii yenyewe, na mara nyingi ni sehemu ya mawazo mgando ambayo hufikiriwa kuwa ya kawaida au ya kuridhisha tu jamii na hivyo husababisha utengano wa jamii. Mtazamo huu huwapuuza maskini na kuishi kana kwamba hawapo. Uchumi unaofuata nadharia hii hulenga kunufaisha kikundi kidogo kwa jasho la umma. Wakati huo maskini wanaambulia matone machache tu ya neema ambayo yanashuka katika vipindi vya migogoro.  Aina ya kweli ya kutengwa huja tunapojiwekea kikomo kwa visingizio vya kinadharia badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo halisi ya wale wanaoteseka.

Ndugu msomaji/msikilizaji, Mtakatifu Yohane Paulo wa II alimbua kuwa; “jamii hutengwa ikiwa taasisi zake za kijamii, uzalishaji na matumizi hayana dhamira safi na kielelezo cha muungano na mshikamano kati ya watu.” Tunahitaji kujitolea zaidi kutatua vyanzo vya mifumo ya umaskini. Hili ni hitaji kubwa ambalo "haliwezi kucheleweshwa, sio tu kwa sababu ya uharaka wake wa kutoa huduma kwenye jamii, lakini kwa sababu jamii inahitaji kuponywa ugonjwa ambao unaidhoofisha na kuikatisha tamaa, na ambao unaweza kusababisha machafuko mapya. Miradi ya ustawi, ambayo inakidhi mahitaji fulani ya dharura, yapaswa kuzingatiwa kama majibu ya muda tu.” Inasemekana kwamba ukosefu wa usawa ni chanzo cha matatizo ya kijamii. Hata hivyo, upatikanaji wa haki za binadamu si sawa kwa wote.

Kama ulivyo mtindo wa kisasa, wenye mwamko wa mafanikio na kujitegemea, hauelekei kuwasaidia wanyonge na wasioweza kupata fursa maishani. Hali hii hujirudia tena na tena. Je, hii ina maana kwamba wenye vipawa vidogo si binadamu? Au kwamba wanyonge hawana utu sawa na sisi wenyewe? Na wale waliozaliwa katika mazingira yenye fursa chache wao si wanadamu? Je, wanapaswa kuishi kwa kupata chochote cha kuweka kinwani tu? Mstakabari wetu na wa kesho yetu unategemea aina ya majibu tunayotoa kwa maswali haya. Ama tutetee heshima yetu ya kiadili na kiroho au tuanguke kwenye dimbwi la uchafu. Tusiposimama na kuchukua hatua madhubuti juu ya jambom hili, tutaendelea, hadharani au kwa siri, “kuhalalisha mtindo wa sasa wa mgawanyo, ambapo wachache wanaamini kwamba wana haki ya kufaidi kwa fursa ambayo haziwezi kuenezwa kwa watu wote, kwa kuwa ulimwengu hauwezi kuafiki hilo.”

Ndugu msomaji/msikilizaji, suala moja la kimkakati ambalo haliwezi kutatuliwa kwa amri za kimamlaka na linahitaji kushughulikiwa mapema iwezekanavyo linahusiana na maeneo, vitongoji, ujirani, makazi ya watu, na miji ambapo maskini wanaishi na kushinda. Sote tunathamini uzuri wa miji inayowajali walemavu, na kuwawekea miundo mbinu ya kimaendeleo. Na zaidi ya hapo, tunaitambua ile miji ambayo katika muundo wake wa usanifu ina nafasi za kukutania, kushirikishana, kubadilishana mawazo na kutambua nafsi ya mwingine. Hata hivyo, tungependa kufikiria athari za kuzorota kwa mazingira ya maisha ya watu, inayoibuka kama utamaduni wa kutumia na kutupa. Kwani kuzorota kwa mazingira huathiri watu hasa wanaoishi katika mazingira hatarishi. Waamini wote wa taifa la Mungu wana wajibu wa kufanya sauti zao zisikike, japo kwa njia tofauti, katika kukemea suala hili la kimkakati, hata kwa gharama ya kuonekana mjinga au wasio na maana yeyote. Mikakati ya kidhalimu inahitaji kutokomezwa kwa nguvu ya wema, kwa kubadili fikra, na kwa msaada wa sayansi na teknolojia, kwa kuandaa sera madhubuti za mabadiliko ya kijamii.

Ndugu msomaji/msikilizaji, ikumbukwe Injili inabaki kuwa mhimu katika udumifu wa mahusiano binafsi na mahusiano na Bwana kwa ajili ya ufalme wa Mungu (rej. Lk 4:43). Katika kumpenda Mungu anayetawala maisha yetu na ulimwengu tunaoishi, anatawala pia undani wetu, jamii zetu, akitutaka kuishi maisha ya udugu, haki, amani na utu. Mafundisho yote ya kikristo yanakusudia kuhuisha jamii, ili watu wautafute ufalme wa Mungu. Hatimaye, katika hati ambayo mwanzoni haikupokelewa vyema na kila mtu, tunapata tafakari hiyo inayotufaa kwa leo: “Watetezi wa itikadi kali ya kiimani wakati fulani wanashutumiwa kwa kutojali, kujinufaisha wenyewe, au kuwa na ushirikiano na wenye hatia katika hali zisizovumilika za dhuluma na tawala za kisiasa kandamizi ambazo zinatete kurefusa kwa vipindi vya utawala. Uongofu wa kiroho, ukuu wa upendo kwa Mungu na jirani, bidii ya haki na amani, maana ya Injili ya maskini na umaskini wenyewe, ni mahitaji ya kila mtu, na hasa kwa wachungaji na wale walio katika nafasi za uwajibikaji. Kujali na umakini wa usafi wa imani hudai jibu madhubuti katika utoaji wa huduma kwa jirani, maskini na waliokandamizwa na mitindo mipya ya kitalimungu. Ndugu msomaji/msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo. 

17 Desemba 2025, 09:35