Tafuta

Picha mojawapo ya Papa kukutana na  Maskini wakati wa ziara yake ya kitume nchini Lebanon. Picha mojawapo ya Papa kukutana na Maskini wakati wa ziara yake ya kitume nchini Lebanon.  (@Vatican Media)

Katika Dilexi Te:Utamaduni wa milenia hii umetushawishi zaidi kuwatenga masikini

Maskini wanatukumbusha kuachana na tabia ya ujeuri na ya kichokozi isivyo na msingi imara hasa tunapokabiliana na magumu ya maisha.Wanatutahadharisha jinsi maisha yetu yalivyo bure na si salama kama inavyopaswa kuwa.Mtakatifu Gregory Mkuu anasema:“Mtu yeyote asifikirie kuwa salama,akisema,‘Siibi vya wengine,lakini nafurahia matunda ya jasho langu kama inavyostahili.’Si mara chache,mafanikio yetu yanatupofusha tusiweze kuona mahitaji ya wengine.

Na Padre Angelo Shikombe – Vatican.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tutafakari katika sura ya sura ya tano inayoelezea changamoto endelevu.

Ndugu msomaji/ msikilizaji, Papa Leo XIV, ametukumbusha historia ya zamani ya Kanisa ya utunzaji wa maskini na namna Kanisa lilivyoishi na maskini ili kuweka mkazo kuwa Kanisa limekuwa daima likiishi na maskini. Kuwajali maskini ni sehemu ya mapokeo ya Kanisa, ni mwanga wa kiinjili unaoangaza mioyo na unaowaongoza waamini kwa kila karne. Hii ndiyo sababu ya kujifungamanisha na kushirikishana mwanga wa Kristo katika maisha ya wanaoteseka na wahitaji. Upendo kwa maskini ni kipengele muhimu cha historia ya ukombozi ambapo Mungu anajihusisha kwa karibu katika maisha yetu. Unachomoza kutoka moyoni mwa Kanisa kama wito wa kudumu kwa mioyo ya waamini, kibinafsi na katika jumuiya zetu. Kama mwili wa fumbo la Kristo, Kanisa linashiriki maisha ya maskini kama sehemu ya mwili wake kwani wao ni mahali pa upendeleo ndani ya Kanisa la Mungu la hija. Kwa hivyo, upendo kwa maskini kwa namna yeyote ile ni alama mahususi ya uinjilishaji wa Kanisa lililo aminifu kwa Mungu. Kwa kweli, moja ya vipaumbele vya kila mara katika upyaisho wa Kanisa unawalenga daima maskini. Kwa mantiki hii, kazi ya kanisa kwa maskini inatofautiana kimsukumo na kimaarifa ukilinganisha na kazi zinaofanywa na mashirika mengine yeyote ulimwenguni.

Ndugu msomaji/msikilizaji, Papa leo XIV anakazia kuwa; asiwepo mkristo anayemwazia maskini kama tatizo la kijamii; wao ni sehemu ya “familia” yetu. Wao ni "miongoni mwetu." Wala uhusiano wetu na maskini hauwezi kugeuzwa kuwa shughuli ya kikanisa.  Kwa maneno ya Hati ya Aparecida, “inatudai kutolea wakati wetu kwa maskini, kuwajali kwa upendo, kuwasikiliza kwa shauku, kusimama nao katika nyakati ngumu, kuishi nao na kuongea nao, kila siku, na kila mwaka huku tukijitahidi kuyaboresha maisha yao, tukiwahusisha kwanza wao wenyewe. Tusisahau kwamba hilo ni agizo la Yesu, alilopendekeza kwa maisha yake, matendo na maneno yake mwenyewe.

Ndugu msomaji/msikilizaji, kwa mara nyingine tena tuangalie maisha ya Msamaria mwema. Utamaduni wetu endelevu mwanzoni mwa milenia hii umetushawishi zaidi kuwatenga masikini, kama watu wasio na tija na hawastahili hata heshima yetu. Papa Francisko katika Waraka wake unaoitwa “Fratelli Tutti”, alitupa changamoto ya kutafakari juu ya mithali ya Msamaria mwema (rej. Lk 10:25-37), ambayo inaweza kupokelewa kwa namna mbalimbali, juu ya mtu alijeruhiwa njiani na kuachwa manusura akiwa kufani. Ni Msamaria mwema pekee anayesimama na kumjali. Papa Francisko aliendelea kuuliza kila nafsi ya mmoja wetu: “Ni yupi kati ya waliopita njia hiyo unafanana naye? Swali hili butu, la moja kwa moja, na lililo wazi, linapaswa kuamsha nafsi zetu kuona namna tunavuowapuuza wengine kana kwamba hatuwaoni, hasa wanyonge. Tukubaliane kwamba, kwa maendeleo yote tuliyofikia, bado ‘hatujaelimika’; hasa linapokuja suala la kutembea pamoja, kutunzana, kujaliana, na kuwasaidia walio dhaifu na walio hatarini zaidi katika jamii zetu. Tumezoea kuangalia upande mwingine, kupita, na kupuuza hali halisi, hadi zituathiri sisi wenyewe moja kwa moja.

Ndugu msomaji/msikilizaji, ni muhimu kwetu kutambua kwamba simulizi la Msamaria mwema linabaki hai hata kwa wakati wetu wa leo. “Kama nitakukutana na mtu usiku wakati wa baridi amelala nje naweza kumwona kama kero, mvivu, kikwazo katika maisha yangu, au ni jambo la kutatanisha, ambalo huenda nikafikiria limeletelezwa na tatizo la wanasiasa kushindwa kutatua kero za watu. Maskini anachukuliwa kuwa ni takataka inayochafua mazingira ya umma. Je, tunaweza kujibu kwa imani na upendo, tukimtazama mtu huyo kama binadamu mwenye utu ulio sawa na wetu, mwenye kufanana nasi, kiumbe aliyeumbwa na Baba, na ndugu aliyekombolewa na Kristo?  Huko ndiko kuwa mkristo! Je, utakatifu unaweza kwa namna fulani kueleweka kwa kutambua utu wa kila mtu. Je, Msamaria mwema hakufanya hivyo? Jambo hili ni muhimu kwani linaitia dosari kubwa jamii yetu na jumuyiya zetu za kikristo.  Mitindo mingi ya kutojali imetapakaa pande zote na inatoa ishara za mwelekeo wa kuenea kwa maisha ya hila. Tunachokiona mara kwa mara ni mtu anayeteseka na kutusumbua. Inatutia wasiwasi, kwa kuwa hatuna muda wa kupoteza juu ya matatizo ya wengine. Hizi ni dalili za jamii isiyo na afya. Jamii inayotafuta mafanikio lakini hayapatikani. Tusije tukazama huko! Hebu tuangalie mfano wa Msamaria mwema.  Maneno yanayohitimish Injili hiyo yanasema; "Nenda nawe ukafanye vivyo hivyo" (Lk 10:37), yanawakilisha agizo ambalo kila mkristo lazima alibebe kwa moyo.

Ndugu msomaji/ msikilizaji, zipo changamoto zisizoepukika kwa Kanisa la leo. Katika kipindi muhimu sana katika historia ya Kanisa la Roma, wakati taasisi za kifalme zilikuwa zikianguka kwa uvamizi wa mataifa ya kipagani, Papa Mtakatifu Gregory Mkuu alihisi kuwa; ni muhimu kuwakumbusha waamini: “Kila dakika tunayokutana na Lazaro, tukimtafuta kila wakati, hata bila kumtafuta, tunamkuta mlangoni mwetu. Sasa wanatuzingira wakiomba msaada; wakituomba kuwa watetezi wao, na baadaye ndiwo watakaotushitaki mbele za Mungu au kutututetea mbele zake. Kwa hiyo tusipoteze nafasi ya kutenda kwa huruma; na tusihifadhi vitu msivyovihitaji.  Papa Mtakatifu Gregory Mkuu kwa ujasiri alishutumu mifumo ya kisasa ya chuki dhidi ya maskini, ikiwa ni pamoja na imani ya kwamba wao ndio wanaohusika na shida zao: “Wakati wowote ukiwaona masikini wanafanya jambo la kulaumiwa, usiwadharau wala kuwapuuza, kwani ugumu wa umaskini wao huenda unatakasa dhambi zao, hata kama ni kidogo namna gani. Si mara chache, mafanikio yetu yanatupofusha tusiweze kuona mahitaji ya wengine, na hata kufikiri kwamba furaha na utimilifu wetu hutegemea nguvu zetu wenyewe, mbali na misaada ya wengine. Katika hali kama hizi, masikini anabaki kuwa mwalimu wetu aliyeko kifichoni anayetufanya tutambue thamani yetu na kututia roho halali ya unyenyekevu.  Ingawa ni kweli kwamba tajiri humjali maskini, kinyume chake pia ni kweli. Huu ni ukweli unajifunua katika mapokeo yote ya kikristo.

Ndugu msomaji/msikilizaji, maisha yanaweza kweli kugeuzwa kwa kutambua hilo na maskini wengi wakatufundisha juu ya Injili na madai yake. Kwa ushuhuda wao wa kimya, wanatutafakarisha hatari ya uwepo wetu. Wazee, kwa mfano, kwa udhaifu wao wa kimwili, kunatukumbusha udhaifu wetu wenyewe, hata tunapojaribu kuuficha nyuma ya mafanikio yetu. Maskini pia, wanatukumbusha kuachana na tabia ya ujeuri na ya kichokozi isivyo na msingi imara hasa tunapokabiliana na magumu ya maisha. Wanatutahadharisha jinsi maisha yetu yalivyo bure na si salama kama inavyopaswa kuwa.  Hapa tena, Mtakatifu Gregory Mkuu ana mengi ya kutuambia: “Mtu yeyote asifikirie kuwa salama, akisema, ‘Siibi vya wengine, lakini nafurahia matunda ya jasho langu kama inavyostahili.’ Yule tajiri, hakuadhibiwa kwa sababu alichukua mali ya wengine, lakini kwa sababu, wakati akiwa na mali nyingi hakutenda haki kwa maskinii. Utajiri wake ulimfanya awe na kiburi na kiburi hicho ndicho kilichomfanya ashuke kuzimu, maana alikosa huruma.

Ndugu msomaji/msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume ya Papa Leo XIV kuhusu "Dilexi Te" yaani "Nimekupenda", usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.

19 Desemba 2025, 15:15