Katika Dilexi Te:Upendo wa kweli unawathamini maskini!
Padre Angelo Shikombe - Vatican.
Mpendwa msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assisi. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tutafakari katika sura ya nne inayojikita katika historia endelevu na maskini akiwa mhusika mlengwa.
Ndugu msomaji/msikilizaji, taswira maisha ya Kanisa la kiulimwengu inafafanuliwa kinagaubaga na mkutano wa Aparecida, ambapo maaskofu wa Amerika ya Kusini waliweka wazi chaguo la pekee la Kanisa kwa maskini. Liko katika ungamo la kikristo kwa Mungu ambaye alifanyika maskini kwa ajili yetu, ili atutajirishe kwa utajiri wake. Hati ya Aparecida inauweka utume wa Kanisa katika muktadha wa ulimwengu wa sasa wa utandawazi ulio na mapungufu mengi. Katika hitimisho lao, maaskofu waliandika kuwa: “Tofauti kuu kati ya matajiri na maskini inatualika kufanya kazi kwa kujitolea zaidi tukiwa wanafunzi wenye uwezo wa kushirikishana maisha, katika meza ya udugu wa Baba, usiomtenga yeyeto, tukitangaza upendeleo wetu katika kutatua changamoto za maskini. Wakati huo huo, Hati hii ikichukulia umhimu mada zilizojadiliwa katika mikutano ya awali ya bara la Amerika, bado inasisitiza juu ya haja ya utamaduni wa kujiendeleza kwa jamii zilizotengwa na sio kutegemea tu hisani kutoka upande wa wengine. Hii ina maana kwamba, jumuiya zina haki ya kukumbatia Injili, kusherehekea na kutangaza imani yao ndani ya mila na tamaduni zao. Uzoefu wao wa umaskini unawapa uwezo wa kutambua vipengele muhimu ambavyo wengine hawawezi kuviona; kwa sababu hii, jamii inahitaji kuwasikiliza. Ndivyo ilivyo kwa Kanisa, ambalo linapaswa kuzingatia vyema utendaji wake wa kiimani.
Ndugu msomaji/msikilizaji, tafakari juu ya Hati ya Aparecida inatusaidia namna ya kujibu changamoto za leo. Ukaribu kwa maskini na kujenga urafiki nao utatuwezesha kuthamini nafasi ya mtu maskini wa leo, hali kadhalika wao wakiwa watangazaji wa imani hai. Siku baada ya siku, maskini wanakuwa washenga wa uinjilishaji na ukuzaji wa tunu za utu. Wanawaelimisha watoto wao katika imani, wajishughulishe na mshikamano wa kidugu, wamtafute Mungu daima, na kujitoa kikamilifu katika hija ya Kanisa. Katika mwanga wa Injili, tunatambua hadhi yao kuu ya utu na thamani yao takatifu machoni pa Kristo, aliyekuwa maskini kama wao na kutengwa miongoni mwao. Kulingana na uzoefu huu wa kiimani, Papa Leo XIV anapenda kutetea haki zao. Haya yote yanahusisha kipengele kimoja ambacho ni lazima tukikumbuke kila mara, yaani kuwa makini kwa maisha ya wengine. Usikivu huu umemvutia Baba Mtakatifu na kumpa moyo wa kuanza kutafuta wema wao. Kwani pendo la kweli ni huwathamini maskini katika wema wao, katika uzoefu wao wa maisha, katika utamaduni wao, na katika njia zao za kuishi imani. Pendo la kweli daima ni la kutafakari, na huturuhusu kumtumikia mwingine kwa hiari, kwa sababu yeye ni mwema zaidi.
Ndugu msomaji/msikilizaji, kwa msingi huu, Baba Mtakatifu anapenda kuelezea hisia zake za dhati kwa ukaribu huu wa kweli unaotuwezesha kuandamana ipasavyo na maskini kwenye njia yao ya ukombozi. Kwa sababu hii, Baba Mtakatifu anatoa shukrani zake za dhati kwa wale wote ambao wamechagua kuishi miongoni mwa maskini, si tu kwa kuwatembelea mara kwa mara bali kuishi nao jinsi wanavyoishi. Aina ya utume huu inapaswa kuhesabiwa kuwa mojawapo ya aina za juu kabisa za maisha ya kiinjili. Kwa kuzingatia hili, ni dhahiri kwamba sisi sote tunainjilishwa na maskini na kukiri hekima ya fumbo ambalo Mungu anataka kushiriki nasi kupitia kwao. Kukua katika mazingira hatarishi, wakijifunza kustahimili hali mbaya zaidi, wakimtumaini Mungu pekee anayewasaidiana katika nyakati za giza zaidi, ni uthibitisho kwamba maskini wanajifunza mambo mengi ambayo wameyaficha mioyoni mwao. Miongoni mwetu ambao hatujapata nafasi kama hii ya kuishi, hakika kuna mengi ya kujifunza kutokana na hekima iliyofichika ya maisha ya maskini. Ni kwa kuhusisha tu mifano ya mateso yao katika unyonge wao tunaweza kupata karipio ambalo linaweza kutupa uponyaji na kurekebisha maisha yetu. Ndugu msomaji /msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.