Katika Dilxi Te:“Fumbo la Kristo ndani ya Kanisa limekuwa daima ni ni fumbo la Kristo kwa maskini"
Na Padre Angelo Shikombe – Vatican.
Mpendwa msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tutafakari katika sura ya nne inayojikita katika historia endelevu.
Ndugu msomaji/msikilizaji, karne mbili zilizopita zinajulikana kama karne za mafundisho jamii ya Kanisa. Kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na kijamii katika karne mbili zilizopita, ikiambatana na kupingana, na kugongana huku na huko, sio tu ilikuwa na athari kwa maisha ya maskini lakini pia umekuwa mjadala mkali na wenye kutafakarisha sana. Harakati mbalimbali za wafanyakazi, wanawake, wanaume na vijana, dhidi ya mapambano ya ubaguzi wa rangi, yameamsha mwamko mpya wa utu wa wale wanaoishi pembezoni mwa jamii. Mafundisho ya kijamii ya Kanisa pia yaliibuka kutoka mktadha huu. Uchambuzi wa mafundisho ya kikristo katika masuala ya kisasa, kijamii, kikazi, kiuchumi na kiutamaduni hayangewezekana bila mchango wa walei, wanaume na wanawake, ambao waliopambana kikamilifu wakijibu changamoto za wakati wao. Miongoni mwao walikuwemo watawa wa kiume na kike waliosadia kuwa na mtazamo mpya wa Kanisa.
Mabadiliko ambayo Kanisa linapitia leo hii yamelijengea Kanisa mazingira ambayo yameweza kuwakutanisha walei na Makleri, kati ya watu wa kawaida na watalaam, kati ya watu binafsi na taasisi. Hapa pia, uhalisia na tunu za Kanisa zinatazamwa vizuri zaidi kutoka pande zote na maskini wana mchango wa kipekee ambao ni muhimu kwa Kanisa na kwa wanadamu kwa ujumla. Mafundisho Tanzu ya Kanisa yaani “Majisterio” kwa miaka 150 iliyopita yamekuwa hazina adimu ya mafundisho kuhusu maskini. Baraza la Maaskofu wa Italia wametoa sauti yao kupitia mchakato wa kimapokeo wa Kanisa. Kupitia Barua ya kitume juu ya Mafundisho Jamii ya Papa Leo XIII inayojulikana kama “Rerum Novarum”, Papa Leo XIII aliongelea suala la wafanyakazi, akionesha hali isiyovumilika ya maisha ya wafanyakazi wengi viwandani akishauri uanzishwe utaratibu wa haki za kijamii.
Ndugu msomaji/msikilizaji, mapapa wengine pia walishazungumzia mada hii. Mtakatifu Yohane XXIII, katika Waraka wake unaojulikana kama “Materi et Magistra” yaani, “Kanisa ni Mama na mwalimu,” uliotolewa 1961, ulitoa rai na wito wa kuwepo kwa haki kitaifa na kimataifa: nchi tajiri hazipaswi kubaki baridi bila kujihusisha na mahangaiko yanayotokana na njaa na umaskini wa kupindukia, badala yake wawasaidie kwa ukarimu kwa mali zao zote. Mtaguso wa II wa Vatican ulikuwa ni hatua muhimu katika uelewa wa Kanisa juu ya maskini katika mpango wa Mungu wa kuokoa. Japokuwa mada hii ilibaki pembeni katika hati za maandalizi, Mtakatifu Yohane XXIII, katika ujumbe wake kwa Radio wa tarehe 11 Septemba 1962, yaani mwezi mmoja kabla ya kufunguliwa kwa mkutano, alitoa rai hii. Kwa maneno yake alisema; “Kanisa linajionyesha jinsi lilivyo na linavyotaka kuwa Kanisa la wote na hasa Kanisa la maskini”.
Jitihada kubwa za maaskofu, wanatheolojia na wataalam waliohusika na upyaishaji wa Kanisa, na kwa msaada wa Mtakatifu Yohane XXIII mwenyewe, walilipa Baraza mwelekeo mpya. Msingi wake alikuwa ni Kristo katika nyanja zote za kimafundisho ya kijamii na mafundisho mengi ya Mababa wa Kanisa yanaunga mkono mtazamo huu, kama ilivyoelezwa kwa ufasaha na Kardinali Lercaro alipochangia mnamo tarehe 6 Desemba 1962 akisema; “Fumbo la Kristo ndani ya Kanisa limekuwa daima ni ni fumbo la Kristo kwa maskini.” Aliendelea kusema kuwa, “hii si hoja moja kati ya nyingi, lakini ni hoja pekee ya mkutano mkuu”. Askofu Mkuu wa Bologna, naye alibainisha kuwa; “kipindi hicho ni kilikuwa kipindi cha maskini, yaani mamilioni ya maskini kokote waliko ulimwenguni. Na aliendelea kusema kuwa hiki ni kipindi cha mama Kanisa wa maskini. Kipindi cha fumbo la Kristo, hasa kwa maskini”.
Ndugu msomaji/ msikilizaji, tokea hapo Kanisa limechukua sura mpya, rahisi na ya kiasi, inayowakumbatia watu wote wa Mungu na uwepo wake ndani ya historia. Kanisa linalofanana zaidi na Bwana wake kuliko mamlaka za kidunia na linalofanya kazi ya kulea dhamira thabiti ya uwajibikaji wa watu katika kutatua tatizo kubwa la umaskini duniani. Katika ufunguzi wa kikao cha pili cha Baraza, Mtakatifu Paulo wa sita alisisitiza msimamo huu akimfuta mtangulizi wake, alisema; Kanisa linatazama kwa makini sana uwepo wa maskini, wanyonge, wenye njaa, wanaoteseka, na waliofungwa. Hii inamaanisha kuwa; linawatazama wote wanaoteseka na kulia: Kanisa liko nao linapoishi nadhiri zake za kiinjili. Katika kikao cha tarehe 11 Novemba 1964, Papa Yohane wa XXIII alionyesha namna maskini wanavyomwakilisha Kristo, huku akilinganisha sura ya Bwana katika maisha ya maskini.
Papa Yohane XXIII alidhihirisha uelewa wa pamoja katika uwakilishi wa Kristo ndani ya maskini; yaani kila mtu huwakilisha nafsi ya Kristo; maskini na mtume Petro wako sawa kinafsi lakini wenye uwakilishi ulio tofauti yaani ule wa kimaskini n aule wa kiti cha Utume wa mamlaka ya Petro. Kwa njia hii, kiungo cha ndani kati ya Kanisa na maskini kinaonyeshwa kiishara na kwa uwazi usio na kifani. Hati ya kichungaji yaani “Gaudium et Spes”, inayojengeka juu ya mafundisho ya mababa wa Kanisa, inakazia tofauti iliyopo kati ya upatikanaji wa rasilimali na mahitaji yake ya kijamii. Hati hii inasisitiza kwamba “Mungu aliumba dunia na vyote vilivyomo kwa ajili ya watu wote na mataifa yote ili vitu vyote vilivyomo vitumike kwa haki na kwa wote katika tendo la ukarimu. Kwa hiyo, kila mtu ana haki ya kumiliki kiasi fulani cha mali kinachomtosha yeye mwenyewe na familia yake. Katika ulazima wa matumizi ya vitu maskini wana haki ya kutumia mali za matajiri. Hivyo, mali binafsi ina kipenere cha kusaidia jumuyiya kwa manufaa ya wote.
Pale ambapo huduma ya jamii imesahaulika, umiliki huwa chanzo cha uchoyo na vurugu. Fundisho hili linapatikana katika mafundisho ya Mtakatifu Paulo VI katika Wataka unaojulikana kama “Populorum Progressio”. Hapo tunasoma kwamba hakuna aliyehalalishwa kumiliki na ziada kwa ajili yake pekee wakati wengine wanakosa hata mahitaji yao ya msingi. Katika hotuba yake kwa Umoja wa Mataifa, Papa Paulo VI aliongea na maskini na kuhimiza Umoja wa kimataifa kujenga ulimwengu wa mshikamano. Pamoja na mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II, alisisitiza kuwa; Kanisa limeimariha uhusiano wake na maskini na linaonesha ukuu wa uhusiano huu katika kuadhimisha pendo la kikristo ambalo mapokeo yote ya Kanisa yanalishuhudia. Katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis”, aliendelea kusema kuwa: “Leo, tukiwa na mwelekeo wa ulimwengu mzima ambapo swali la kijamii lidai kujibiwa, upendo huu wa namna yake kwa maskini, ni maamuzi yetu yanayotutia hamasa ndani yetu, yanakumbatia umati mkubwa wa wenye njaa, wenye uhitaji, wasio na makao, wasio na huduma ya matibabu na, zaidi ya yote, wasio na matumaini ya maisha bora ya baadaye.
Haiwezekani kutozingatia ukweli huu. Kuupuuza ukweli huu ni sawa na kujifanannisha na yule tajiri aliyejifanya hamjui Lazaro ombaomba aliyelala mlangoni pake (Lk 16:19-31). Mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II juu ya kazi vile vile ni muhimu kwetu kuyazingatia ili tuweze kutambua jukumu halisi la maskini na namna wanavyopyaisha Kanisa na jamii, na hivyo kuacha nakala ya uzalendo fulani wa kuwasaidia maskini. Katika Waraka unao inaoitwa “Laborem Exercens”, Yohane Paulo II alisema kwa ujasiri kwamba “kazi ni ufunguo, na pengine ni ufunguo wa hazina ya kijamii”. Ndugu msomaji/msikilizaji, katikati ya migogoro mingi iliyoashiria mwanzo wa milenia ya tatu, mafundisho ya Papa Benedikto XVI yalichukua mkondo wa kisiasa zaidi. Kwa hivyo, katika Wosia wake unaoitwa “Caritas in Veritate”, Papa Benedikto XVI anathibitisha kuwa “kadiri tunavyojitahidi kutunza mafaa ya pamoja yanayolingana na mahitaji halisi ya jirani zetu, ndivyo tunavyowapenda kwa ufanisi zaidi majirani zetu”. Aliendelea kusema kwamba; “njaa haitegemei sana uhaba wa vitu vya kimwili kama vile rasilimali za kijamii, ambazo ni muhimu zaidi katika kuendeleza taasisi zetu.
Kinachokosekana, kwa maneno mengine, ni mtandao wa taasisi za kiuchumi zenye uwezo kuhakikisha upatikanaji wa mara kwa mara wa chakula na maji ya kutosha kwa mahitaji ya lishe, na pia zenye uwezo wa kushughulikia mahitaji ya msingi yanayotokana na migogoro ya kila siku ya ukosefu wa chakula, iwe ni kutokana na sababu za asili au kutowajibika kisiasa, kitaifa na kimataifa. Papa Francisko alitambua kwamba katika miongo ya hivi karibuni, pamoja na mafundisho ya Maaskofu wa Roma, Mabaraza ya Maaskofu kitaifa, na kikanda yamezidi kukazia suala hilo. Yeye mmwenewe alishuhudia binafsi, dhamira fulani ya Baraza la maaskofu wa Amerika ya Kusini ya kufikiria upya uhusiano wa Kanisa na maskini. Katika kipindi chake, karibu Amerika Kusini yote kulikuwa na harakati za kikanisa kuwatambulisha maskini na kuwashirikisha kikamilifu katika kulinda uhuru wao.
Kulikuwa na umati mkubwa sana wa maskini wanaohangaika na ukosefu wa ajira, pengine uwepo wa ajira duni, mishahara isiyo ya haki wla halali kwa maskini. Kuuawa kwa Mtakatifu Oscar Romero, Askofu Mkuu wa San Salvador, kulikuwa ni ushahidi wenye nguvu na msukumo wa ajabu kwa Kanisa. Papa Francisko alifanya marekebisho makubwa ya utume wa kichungaji kulifanya kundi lakichungaji kuwa kitovu cha maono yake ya kichungaji. Baraza la Maaskofu wa Amerika Kusini ilililofanyika Medellín, Puebla, Santo Domingo, na Aparecida, lilikuwa tukio muhimu kwa Kanisa kwa ujumla. Kwa upande wake, baada ya kutumikia kama mmishonari huko Peru kwa miaka mingi, aliwiwa kutoa wosia huu wa kikanisa. Papa Fransisko alihusisha busara hii kwa makanisa mengine, hasa yale yaliyoko Kusini mwa dunia.
Ndugu msomaji/msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.