Tafuta

Kardinali Parolin: Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Msumbiji: 14 Desemba 1994. Kardinali Parolin: Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Msumbiji: 14 Desemba 1994.  ((foto X - ©TerzaLoggia))

Kumbukizi ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Vatican na Msumbiji

Kardinali Pietro Parolin, kuanzia tarehe 5 Desemba-10 Desemba 2025 anafanya hija ya kitume nchini Msumbiji kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 tangu Vatican ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Msumbiji miaka 30 iliyopita. Tayari Kardinali amekwisha kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali wakiongozwa na Rais Margarida Adamugy Talapa. Dominika tarehe 7 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Msumbiji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR. Tarehe 26 Juni 2018, Vatican na nchi ya San Marino wameridhia kwa pamoja mkataba wa ushirikiano na Kanisa ili kutoa fursa ya kufundisha dini shuleni. Tarehe 23 Agosti 2018 Vatican na Benin ziliridhia mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa na kwamba, kwa sasa Serikali ya Benin inalitambua Kanisa kisheria! Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018; ukapyaishwa tena tarehe 22 Oktoba 2020, 22 Oktoba 2022 na hatimaye 22 Oktoba 2024. Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka minne yaani hadi mwaka 2028. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuwapatia watu wa Mungu wachungaji wema na watakatifu. Vatican na China vimetiliana sahihi mkataba wa muda unaotoa fursa na uwezo kwa Kanisa kuteuwa Maaskofu mahalia. Katika kipindi cha Mwaka 2024 Vatican ilitia saini mikataba kati yake na Burkina Faso pamoja na Jamhuri ya Watu wa Czech.

Maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Kitaifa nchini Msumbiji
Maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Kitaifa nchini Msumbiji

Hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amegusia kuhusu umuhimu wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Mataifa mbalimbali duniani na kwamba, yanatekelezwa kwa uvumilivu mkubwa, hata sehemu ambazo kuna ugumu, kwa kuwa kuna matumaini ya familia bora ya wanadamu kwa siku za mbeleni. Shughuli za kidiplomasia ni nyenzo katika kufuatilia, kushiriki, na kutoa ushawishi katika Jumuiya ya Kimataifa. Utume wa Kanisa ni kuhangaikia kwa matumaini na kushuhudia ile hamu ya haki, amani, ustawi na mafao ya wengi. Diplomasia ya Kanisa sio upendeleo unaotolewa na Serikali kwa Kanisa, bali ni haki ya msingi ambayo Kanisa inayo, na hivyo katika Jumuiya ya Kimataifa, Kanisa lina haki sawa kama vyombo na Jumuiya zingine wanachama. Kwa zama hizi, ni wajibu wa Kanisa kutafuta mahusiano ya amani kati ya Mataifa, wakati likizingatia lengo la mwisho, yaani wokovu wa roho za watu. Katika ulimwengu mamboleo kuna matatizo na changamoto mbalimbali zinazohitaji kushughulikiwa kwa kutumia kanuni ya kidiplomasia. Leo hii kuna tabia ya ukuaji wa utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kiasi cha baadhi ya mataifa kujimwambafai, na hivyo kuhatarisha diplomasia ya kimataifa. Kimsingi, matatizo na changamoto mbalimbali zinapaswa kujadiliwa kwa kuzingatia msingi ya ukweli na uwazi; kwa kuibua mbinu mkakati na hatimaye, sera za utekelezaji wake. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni amani. Kuna baadhi ya Mataifa yanatishia kufumbia macho: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hali ambayo inayatumbukiza Mataifa yenye mwelekeo kama huo katika uchoyo na ubinafsi. Mafanikio ya taifa lolote lile yanapata chimbuko lake katika elimu na tafiti makini.

Hayati Papa Francisko akiwa nchini Msumbiji
Hayati Papa Francisko akiwa nchini Msumbiji

Kardinali Pietro Parolin, kuanzia tarehe 5 Desemba hadi tarehe 10 Desemba 2025 anafanya hija ya kitume nchini Msumbiji kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 30 tangu Vatican ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Msumbiji tarehe 14 Desemba 1994, miaka 30 iliyopita. Tayari Kardinali amekwisha kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Msumbiji, wakiongozwa na Rais Margarida Adamugy Talapa. Dominika tarehe 7 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji sanjari na kufunga Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa. Kardinali Parolin, ametembelea Kituo cha Huduma Kwa Maskini, “Casa Mateus25. Tarehe 8 Desemba 2025, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asali anatembelea Jimbo Katoliki la Pemba na hatimaye, kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na wa kidini na hatimaye, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, tarehe 9 Desemba 2025 anakutana na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Msumbiji na baadaye, anatarajia kufanya majadiliano ya kiekumene na kidini na viongozi mbalimbali nchini Msumbiji. Mwishoni mwa hija yake ya kitume, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican atatembelea Kituo cha mradi wa “DREAM” kinachoendeshwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio huko Zimpeto.

Kardinali Parolin akiwa Mjini Maputo, Msumbiji
Kardinali Parolin akiwa Mjini Maputo, Msumbiji   (©Rogério Maduca)

Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” ilizinduliwa tarehe 7 Juni 2018 na Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji. Inaendesha mradi mkubwa wa kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto unaojulikana kama “DREAM” yaani “Disease Relief Through Excellent and Advanced Means”. Huu ni Mradi mkubwa uliozinduliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kunako mwaka 2002 na kwa sasa unatekelezwa katika nchi 10 za Kiafrika. Lengo ni kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama mjamzito kwenda kwa mtoto pamoja na kuendelea kudhibiti magonja nyemelezi. Wanawake wengi wajawazito waliokuwa wameambukizwa Virusi vya Ukimwi, wakajifungua bila watoto wao kuathirika, wanaliona jambo hili kuwa ni muujiza mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mradi wa “DREAM” ulipata chimbuko lake nchini Msumbiji na kwa sasa unaendelea kutoa tiba kwa wagonjwa zaidi ya 500, 000 katika nchi 10 za Kiafrika. Hii ni taarifa fupi ya Dr. Cacilda Massango, Mratibu wa Mradi wa “DREAM” nchini Msumbiji. Wanawake waliopata fursa ya kujifungua bila ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, wakishakupona na wao pia wanajiunga katika mchakato wa huduma kwa wagonjwa, kwa kuwasindikiza katika safari yao ya matibabu. Dr. Cacilda Massango, Mratibu wa Mradi wa “DREAM” nchini Msumbiji ni kati ya wanawake waliopata bahati ya kujifungua watoto bila maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, leo hii ni kati ya wafanyakazi wa Hospitali hii wanaotoa huduma kwa waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi. Hii ni familia mpya ambayo imewezesha kupata tiba na kurudisha tena utu na heshima yake kama binadamu na kwamba, anayo matumaini kwa leo na kesho iliyo bora si tu kwake binafsi, bali hata kwa watoto wake. Kwa njia ya Mradi huu, wananchi wengi wa Msumbiji wamepata matumaini mapya!

Diplomasia
07 Desemba 2025, 15:50