Hospitali ya Bambino Gesù&MAXXI:kuhamasisha ustawi wa watoto wagonjwa kupitia sanaa
Vatican News
Kuboresha ubora wa maisha katika mazingira ya huduma ya afya, na kufanya hivyo kupitia sanaa. Hili ndilo lengo la makubaliano yaliyosainiwa na Mfuko wa MAXXI na Hospitali ya Kipapa ya Watoto ya Bambino Gesù, kuanzisha ushirikiano wa miaka mitatu unaojumuisha utamaduni na huduma ya afya. Mkataba huo unachochewa na hamu ya kuimarisha mpango wa mapokezi wa Hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù na kuhakikisha watoto waliolazwa hospitalini na familia zao wanapata utamaduni na sanaa kama zana za ujumuishaji na ustawi: huduma inayotambua na kuongeza ufanisi wa kielimu na kijamii wa urithi wa kiutamaduni.
Sanaa inayoondoa hofu
"Tunashukuru sana Mfuko wa MAXXI kwa fursa hii, ambayo inaimarisha safari yetu ya utunzaji wa watoto kwa nguvu dhaifu ya sanaa," alisema hayo Tiziano Onesti, rais wa Hospitali ya Kipapa ya Watoto ya Bambino Gesù, baada ya kusaini makubaliano hayo. "Sanaa ina uwezo wa kupunguza hofu, kuchochea ubunifu, na kutoa kimbilio la kihisia katika nyakati ngumu zaidi. Kuleta warsha za upigaji picha, sanaa za kuona, na usanifu hospitalini kunamaanisha kuunda nafasi tofauti, ambapo watoto wanaweza kujieleza, kufurahi, na kuhisi kama wahusika wakuu, sio wagonjwa na familia zao tu, wanaopata wakati wa utulivu kutokana na kuona hili machoni pao. Pamoja na MAXXI," alihitimisha Rais Onesti kuwa, "tunataka kujenga mazingira ya utunzaji yanayozidi kukaribisha na ya kibinadamu, ambapo utamaduni na afya hutembea pamoja ili kuwapa watoto kile kilicho cha thamani zaidi: nafasi ya kuhisi tu kama watoto."
Muungano kati ya utamaduni na afya
Maria Emanuela Bruni, rais wa Mfuko wa MAXXI, alisisitiza thamani ya matibabu ya shughuli za ubunifu: "Sanaa ya kisasa inaweza kuwa chombo muhimu cha usaidizi katika njia ya kupona, msaada kwa watoto na familia zao katika kukabiliana na nyakati ngumu, na njia ya kuelezea na kushughulikia hisia ngumu. Tunaamini," alihitimisha, "kwamba utamaduni na afya vinaweza na lazima vijadiliane ili kutoa athari chanya na ya kudumu kwa jamii."
Ziara za kuongozwa Bila Malipo katika MAXXI
Ushirikiano huu unajumuisha mipango mbalimbali iliyojumuishwa, ambayo ilianza tarehe 19 Februari 2026, huku ya kwanza katika mfululizo wa warsha za sanaa hospitalini, ikiongozwa na wafanyakazi wa elimu wa Mfuko wa MAXXI kwa kushirikiana na wafanyakazi wa afya wa Hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù. Ziara za kuongozwa bila malipo za MAXXI pia zimepangwa kwa wagonjwa wa hospitali na walezi wao, pamoja na ushiriki katika shughuli za kielimu kwa familia zenye watoto wa miaka 6 hadi 11. Makubaliano hayo yanafungua njia kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya miradi ya pamoja ya kuoanisha mazingira ya hospitali na matoleo mapya ya kielimu kwa watoto, familia, na wafanyakazi wa afya. Makubaliano hayo pia yatawezesha ushiriki katika fursa za ufadhili wa umma na binafsi kwa ajili ya kukuza utamaduni kwa watoto na vijana.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here