Kiindonesia inakuwa lugha rasmi ya 57 ya Vatican News
Vatican News
Kiindonesia kinakuwa lugha ya 57 inayopatikana kwenye Vatican News.
Kutokana na utiaji saini uliofanyika tarehe 25 Machi 2026, wa Mkataba wa Maelewano kati ya wawakilishi wa Kiindonesia na Baraza la Kipapa la Mawasiliano, watu wengi zaidi wataweza kupokea ujumbe wa Papa katika lugha yao wenyewe. Utiaji saini huo ulifanyika katika makao makuu ya Vatican News na Radio Vatican jijini Roma, mbele ya wajumbe wanaowakilisha Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Tume ya Mawasiliano ya Kijamii ya Baraz la Maaskofu wa Indonesia, na Balozi wa Jamhuri ya Indonesia anayewakilisha Nchi yake katika Kiti Kitakatifu
![]()
Saini ya makubaliano
Sherehe ya urafiki wa kudumu
Askofu Agustinus Tri Budi Utomo, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Kijamii ya Baraza la Maaskofu wa Indonesia (KWI), aliyeshiriki katika tukio hilo, alilielezea kama "sherehe ya urafiki wa kudumu, utambuzi wa utambulisho wetu wa kitaifa, na uimarishaji wa daraja la imani kati ya Indonesia na moyo wa Kanisa la ulimwengu wote."
Aliongeza kuwa ni aina ya kisasa ya "Habari Njema" kwa Wakatoliki wa Indonesia, inayoanzisha "njia ya moja kwa moja ya kupata taarifa za Kanisa la ulimwengu kwa watu wa Indonesia" kwani "Wakatoliki nchini Indonesia na Malaysia sasa wanaweza kusikia sauti ya Baba Mtakatifu na ujumbe wa Kanisa la Ulimwengu wote katika lugha yao mama."
![]()
Kutia saini ya Makubaliano
Kukuza ujumuishi na hisia ya kina ya muunganisho
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Dk Paolo Ruffini, Mkurugenzi wa Uhariri Dk. Andrea Tornielli, na Dk. Massimiliano Menichetti, Naibu Mkurugenzi wa Uhariri na mhusika mkuu wa Radio Vatican - Vatican News, walibainisha wakati wa utiaji saini kwamba makubaliano hayo yatasaidia "kukuza ujumuishi, kuimarisha mawasiliano ya kichungaji, na kukuza hisia ya kina ya muunganisho kati ya Vatican na waamini wa eneo hilo."
Pia walibainisha jinsi Kanisa la eneo hilo litakavyoona kuwa rasilimali muhimu katika juhudi zao, na pia kuhakikisha ujumbe muhimu wa amani na udugu kwa wote unawasilishwa na kushirikishwa wazi ndani ya muktadha wa kiutamaduni wa Indonesia.
![]()
Utiaji saini wa Makubaliano
Wakati wa kihistoria kwa Indonesia
Pia alikuwepo wakati wa utiaji saini huo, Balozi wa Jamhuri ya Indonesia anayewakilisha nchi yake Vatican Bw. Michael Trias Kuncahyono, ambaye alielezea furaha yake katika kutimizwa kwa makubaliano haya, akibainisha kuwa tukio hilo linaashiria "wakati wa kihistoria kwa Indonesia" na "hasa kwa Wakatoliki" wa taifa. Kuingizwa kwa lugha ya Kiindonesia katika Vatican News, ambayo sasa ni lugha ya 57 ya chombo cha habari, kutawaruhusu Waindonesia kusoma katika lugha zao mama habari na taarifa kuhusu Papa na Vatican, pamoja na habari za Kanisa ulimwenguni kote.
Ongezeko hili jipya la lugha litaruhusu watu wengi zaidi kuungana na Kanisa na watu kote ulimwenguni ili kujenga ulimwengu unaoangaziwa kwa kusikiliza, kujifunza, kujadiliana na kusherehekea maadili ya pamoja ya amani, udugu na maelewano ya kidini.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.