Tafuta

Kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwenda kwa Baba ni kilele cha Ushindi na Utukufu wake. Kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwenda kwa Baba ni kilele cha Ushindi na Utukufu wake.   (Vatican Media)

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Mashuhuda wa Injili & Upashanaji Habari Ulimwenguni

Siku ya tatu akafufuka, kadiri ya Maandiko Matakatifu, akapaa mbinguni, ameketi kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu, kuwahukumu wazima na wafu! Kristo Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni kwa Baba yake, aliwaagiza wanafunzi wake akisema, "Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi": Huu ni mwaliko wa kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Injili. Ni Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwengu: Kuheshimu na Kuhifadhi sura na sauti...

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, siku arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Kupaa Mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Kabla ya kupaa kurudi kwa Baba, Bwana wetu Yesu Kristo aliwaachia Mitume wake Agizo, “Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” Aliwaahidi kwamba hatowaacha yatima, watapokea nguvu ya Roho Mtakatifu, uwepo wa kudumu wa Kristo mwenyewe kati ya wanafunzi wake. Mitume mara baada ya kumpokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, Msaidizi ambaye Kristo aliwaahidi, walianza mara moja kutekeleza Agizo hili la Kristo, la kuwa mashuhuda wa Injili, wakifundisha, wakibatiza na kuwafanya wengi kuwa wanafunzi wa Kristo. Huu kimsingi ndio wito na utume wa Kanisa hata leo, Kanisa lililojengwa imara juu ya msingi wa Mitume, kama chombo cha wokovu kwa watu wa Mataifa yote. Nasi sote tuliobatizwa tunatumwa kuwa Wamisionari wa Habari hii Njema ya Injili.  Ndio maana Dominika hii iliwekwa rasmi pia kama Dominika ya Upashanaji Habari. Baba Mtakatifu Leo wa XIV katika Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, katika sherehe hii ya kupaa Bwana mbinguni anatutafakarisha kwa kauli mbiu isemayo, “Kuheshimu na kuhifadhi sura na sauti za kibinadamu” akitambua changamoto kubwa iliyopo katika ulimwengu mamboleo, Baba Mtakatifu katika Ujumbe wake anahimiza kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu katika ulimwengu huu unaozidi kutawaliwa na Akili Mnemba na teknolojia za kidijitali. Maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia yameleta changamoto kubwa si tu katika teknolojia yenyewe, bali pia katika nyanja ya muhimu kabisa ya utu wa mwanadamu.

Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni: Akili Mnemba
Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni: Akili Mnemba

Matumizi ya kupitiliza ya Akili Mnemba yamepunguza kwa asilimia kubwa sana uwezo wa kufikiri kwa kina (fikra tunduizi), na ubunifu binafsi. Hivyo ni vyema elimu na uelewa sahihi kuhusu matumizi ya akili bandia yatolewe hasa kwa kwa vijana wadogo, ili waweze kujijengea uwezo binafsi wa kufikiri kwa kina, na kufanya mang’amuzi sahihi ya maisha katika uhuru wa kweli. Baba Mtakatifu anasema Akili Mnemba (AI) inapaswa kuwa chombo cha kumsaidia mwanadamu na kurahisisha mawasiliano, lakini haipaswi kuchukua nafasi ya uwezo wa mwanadamu wa kuhisi, kufikiri, kuamua, kuhusiana, uwezo wa kimaadili, ukweli na uwajibikaji.Baba Mtakatifu Leo XIV anasisitiza kuwa sauti na sura ya mwanadamu ni vitu vitakatifu vinavyobeba utambulisho wa kipekee na haviwezi kubadilishwa na mashine. Hivyo anaonya dhidi ya matumizi ya picha, video na sauti za kutengeneza (deepfakes) zinazoweza kupotosha ukweli na kuharibu, utu, thamani, heshima na hadhi ya mwanadamu na kuvunja mahusiano ya kweli baina ya watu katika jamii. Hivyo anatoa wito kwa wagunduzi wa teknolojia, waandishi wa habari, na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhakikisha teknolojia inatumika kama chombo cha kuunganisha watu, kulinda hadhi, haki, ut una heshima ya mwanadamu na sio kudhoofisha. Pia amekazia kuhusu maadili na ukweli katika uandishi wa Habari katika ulimwengu wa sasa. Waandishi wanatakiwa kusimamia maadili, ukweli na uaminifu katika uandishi wa Habari, badala ya kukimbilia umaarufu au faida ya haraka ya kibiashara hata kwa kuufukia ukweli na kutoa habari za uwongo na za kupotosha jamii. Hayo ndiyo yaliyojiri kwa kifupi katika ujumbe huu wa Baba Mtakatifu. Hebu tutazame sasa liturjia ya Neno la Mungu kwa ufupi na mafundisho tunayoyapata katika Sherehe hii ya kupaa Bwana wetu Yesu Kristo mbinguni.

Matumizi mabaya ya akili unde yana athari sana kwa jamii
Matumizi mabaya ya akili unde yana athari sana kwa jamii   (REUTERS)

Somo la Injili Takatifu: Ni Injili ya Mathayo 28:16-20. Kila Dominika tunakiri katika Kanuni ya Imani yetu kwamba, “Kristo aliteswa akafa, akashukia kuzimu, siku ya tatu akafufuka kadiri ya Maandiko, akapaa mbiguni, ameketi kuume kwa Baba...” Kupaa Mbinguni kwa Bwana wetu Yesu Kristo ni kilele cha mpango wa Mungu wa ukombozi wa wanadamu wote, ulioanza kwa Fumbo Takatifu la umwilisho, Kristo alipotwaa mwili akaingia katika historia ya wanadamu (Yn 1:14). Sasa kwa mwili wa utukufu, anapaa kurudi kwa Baba yake. Kupaa kwa Kristo ni ishara ya kutukuzwa kwake, kuketi kwake mkono wa kuume wa Mungu ni ishara ya mamlaka yake juu ya ulimwengu wote. Kumbe kupaa kwake ni kilele cha kazi ya ukombozi lakini sio mwisho wa kazi hiyo. Kabla ya kupaa, aliacha Agizo kwa wafuasi wake, kuhubiri Injili kwa kila kiumbe, kwani wokovu ni kwa watu wote, si kwa Wayahudi pekee, naye anawaahidi kutenda kazi pamoja nao kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea siku ya Pentekoste. Somo la 1: Ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 1:1-11. Kitabu cha Matendo ya Mitume chaeleza maisha na utume wa Mitume wa Yesu baada ya Yesu kuteswa, kufa na kupaa kwake mbinguni. Chaeleza Mwanzo wa utume wa Mitume wa Kristo na utume wa Kanisa, kama mashuhuda wa Injili ya Kristo. Mwinjili Luka anatuarifu tena kwa mara nyingine wosia wa Kristo kwa Mitume wake kabla ya kupaa kwenda kwa Baba. Mitume walisubiri Ahadi ya Kristo kuwapelekea msaidizi, na wakiisha kumpokea, walianza kwa nguvu kupeleka Habari Njema ya ufufuko wa Kristo kuanzia Yerusalemu, Samaria hata miisho ya dunia. Mwinjili Luka anatuandikia sisi sote, tulio wapendwa wa Kristo, kwamba sisi pia tu mashahidi wa Injili ya Kristo kwa njia Roho Mtakatifu tuliyempokea kwa njia ya ubatizo na kipaimara.

Mtakuwa ni Mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia
Mtakuwa ni Mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia   (@Vatican Media)

Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso 1:17-23. Katika somo la pili, Mtume Paulo anatufundisha, Kwanza, kuwa ni Mungu alimfufua Kristo kutoka wafu na akamweka mkono wake wa kuume juu sana kuliko ufalme wote na akamweka kuwa kichwa juu ya vitu vyote. Kwa njia hiyo ameshinda kifo na mauti, ametuletea ushindi na ukombozi wa milele sisi tulio viungo vya mwili wake yaani Kanisa. Pili, Tumaini letu sisi sote ni kuwa siku moja nasi tutainuliwa juu na kwenda kuungana na Kristo na kutawala naye milele yote. Ili tuweze kufika alipo Kristo, hatuna budi nasi kila mmoja wetu kutimiza kwa uaminifu utume ambao Mwenyezi Mungu ametukabidhi kila mmoja wetu katika maisha yetu ya ufuasi kwake hapa duniani. Tatu, tunaalikwa kuwa wamisionari wa Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo. Mtume Paulo alifanya kazi kubwa ya kumhubiri Kristo mfufuka kwa watu wa mataifa nasi kwa njia ya maneno na matendo yetu, tuwe Injili inayotembea. Maisha yetu yamhubiri Kristo hata pasi na maneno mengi. Kwa nini Bwana wetu Yesu Kristo alipaa kwenda kwa Baba? Nasi tunajifunza nini hasa katika sherehe hii? Ndugu mpendwa, Masomo yetu yote katika dominika hii yanatutafakarisha juu ya wazo hili kuu la kupaa mbinguni kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Ahadi ya Roho Mtakatifu na utume wa Kanisa. Kila Dominika tunakiri katika Kanuni ya Imani yetu kwamba, “Kristo aliteswa akafa, akashukia kuzimu, siku ya tatu akafufuka kadiri ya maandiko, akapaa mbiguni, ameketi kuume kwa Baba...” Licha ya hivyo, Kristo alikwisha waambia mitume wake mara kadhaa kwamba, “Nakwenda kwa Baba” Huu ni ukweli wa imani yetu, na maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kanisa, na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa yanatufundisha juu ya ukweli huo wa imani yetu, imani iliyojengeka katika msingi wa mitume. Ningependa katika sherehe hii tutafakari pamoja swali hili la msingi sana, kwamba kwa nini Kristo siku, arobaini baada ya ufufuko wake alipaa kwenda kwa Baba?

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injli ya Kristo
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injli ya Kristo   (@Vatican Media)

Sababu ya Kwanza: Kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwenda kwa Baba ni kilele cha Ushindi na Utukufu wake. Bwana wetu Yesu Kristo mara baada ya kutimiza kazi aliyotumwa na Baba kuifanya hapa ulimwenguni, kazi ya kuuletea ulimwengu ukombozi wa milele, aliyoanza kwa kutwaa mwili katika Fumbo Takatifu la Umwilisho, kwa utume wake wa wazi, kwa mateso, kifo na ufufuko wake, kilele chake ni kutukuzwa kwake Mbinguni. Huko ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Anatuambia katika somo la Injili Takatifu, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” Kuketi mkono wa kuume wa Baba ni utimilifu wa maono ya nabii Danieli kuhusu Mwana wa Adamu kwamba, “Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatatoweka, na ufalme wake ni ufalme usioharibika” Dan 7:13-14 (KKK #664). Ndugu mpendwa, kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwenda kwa Baba kunatupa nasi sote tulio safarini hapa duniani, tunaotembea katika njia yake ya Msalaba nguvu na ujasiri kwamba, licha ya mateso na kifo, lipo bado tumaini hai la maisha mapya ya ushindi. Bwana wetu Yesu Kristo alipitia dhihaka, maumivu, dharau, fedheha na kifo cha aibu msalabani kabla ya kufufuka na kupaa kwa utukufu mbinguni. Kifo hakikuwa mwisho bali njia ya kuelekea utukufu mpya wa milele na sababu ya wokovu wetu. Katika maisha yetu ya kila siku, nasi tunapokumbana na changamoto mbalimali, ziwe za kifedha, za kifamilia, magonjwa, dhuluma, fedheha, au kufeli, tukumbuke kuwa hayo siyo maisha yetu ya kudumu. Huo sio mwisho wa historia yetu. Ushindi unakuja baada ya mapambano; vumilia kwa uaminifu, mtazame Yesu na songa mbele. Hii inatupa nguvu ya kupambana kutimiza kwa uaminifu majukumu Mungu aliyotukabidhi hapa duniani, kwa muda ambao yeye ametujalia kuishi. Daima tunapokata tamaa kwa sababu mbalimbali tumtazame yeye, aliyetuonesha kuwa mateso na kifo sio mwisho wa maisha bali ni ngazi ya kutufikisha kwenye ushindi na utukufu. Mateso na kifo havina sentensi ya mwisho ya kimaamuzi juu ya hatma ya maisha yetu. Hakuna utukufu pasipo mateso, hakuna uzima mpya pasipo kifo, hakuna kiza kikuu kisichokuwa na pampazuko. Hata misalaba yetu inapotuelemea kiasi gani, hatupaswi kuiacha, hatupaswi kuikimbia, hatupaswi kuipunguza urefu bali kuvumilia na kutembea pamoja na Yesu hadi tuufikie ushindi yaani kule yeye alipokwenda kutuandalia makao. Hiyo ndiyo ngazi yetu ya kufika kwa baba.

Kristo Yesu amepaa mbinguni, ameketi kuu kwa Baba!
Kristo Yesu amepaa mbinguni, ameketi kuu kwa Baba!

Sababu ya pili: Kristo alipaa Mbinguni ili kutuletea zawadi ya Baba, yaani Roho Mtakatifu. Bwana wetu Yesu Kristo alikwishawaambia mitume wake alipokuwa nao katika karamu ya mwisho kwamba, “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu” (Yohane 16:7). Katika somo la kwanza, kutoka katika kitabu cha matendo ya mitume, ile sura ya 1:1-11, Bwana wetu Yesu Kristo kabla ya kupaa kwake alipokutana nao tena mitume wake aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje Ahadi hiyo ya Baba, ile ambayo walisikia habari zake kwake. Hivyo kupaa kwake kimwili kuliruhusu ujio huu wa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, Roho ambaye sasa anakaa ndani ya Kanisa na ndani ya kila muamini na kuliongoza Kanisa ulimwenguni kote mpaka ukamilifu wa dahari. Nasi sote tumempokea Roho huyo katika ubatizo na kuimarishwa katika kipaimara. Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha uhusiano na ushirikiano wa kipekee ulio katika Utatu Mtakatifu. Tunakiri pia katika kanuni ya imani yatu kwamba Roho Mtakatifu anatoka kwa Baba na Mwana (Filioque). Baba ndiye Muumbaji, Mwana ni mkombozi na Roho Mtakatifu ni mfariji wetu. Kumbe Kristo kama alivyowaambia mitume wake kwamba, sitawaacha ninyi Yatima, kwa kupaa kwake mbinguni anamtuma kwao Roho Mtakatifu. Yeye ameondoka kwenda kwa Baba lakini bado ataendelea kuwa kati yao kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea siku ya Pentekoste. Roho Mtakatifu tuliyempokea ni uwepo wa milele wa Kristo ndani ya kila mbatizwa na ndani ya Kanisa. Hajatuacha yatima, tunaye mfariji, tunaye mwalimu anayetufundisha yale yote tuliyoyasikia kutoka kwa Kristo mwenyewe. Anatupa mapaji saba yanayotuimarisha katika safari yetu ya kuelekea mbinguni alipo Kristo mwokozi wetu.

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Siku 40 baada ya Ufufuko wa Kristo Yesu
Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Siku 40 baada ya Ufufuko wa Kristo Yesu   (Vatican Media)

Sababu ya tatu: Kristo Yesu alipaa Mbinguni ili kututayarishia sisi sote makao ya milele mbinguni, ili alipo yeye nasi tuwepo. Kristo katika ile karamu ya mwisho (Yn 14:1-12) alikiwishawaambia wanafunzi wake kwamba, “Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi...Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu, ili nilipo mimi nanyi muwepo. Katika tamaduni za Wayahudi, kawaida kijana aliyetaka kuoa, baada ya kumchumbia bi Arusi, alipaswa kwanza kurudi nyumbani kwa Baba yake.  Huko aliandaa makazi mapya (menō), chumba kipya ambacho kimsingi kiliungana na nyumba ya Baba yake. Na mara makazi yalipokuwa tayari alirudi kumchukua bi Arusi, katika muda na saa ambayo haikufahamika. Hivyo bi Arusi naye alipaswa kujiandaa na kujiweka tayari kwa ujio wa Bwana Arusi (Tunafahamu simulizi ya wanawali kumi). Hivyo Kristo, Bwana arusi, kwa mateso, kifo na ufufuko wake na kupaa kwake mbinguni, anakwenda kwa Baba, kutuandalia makao ya milele. Kurudi kwake, hapa mwinjili Yohane alimaanisha kwa nafasi ya kwanza, kurudi Yesu kwa mitume wake baada ya ufufuko wake siku ya tatu, kwa nafasi ya pili, ni ujio wa Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste na tatu ni ujio wake mara ya pili mwisho wa nyakati. Atakuja kulichukua kanisa, bi arusi wake, nasi twapaswa kujiandaa kwa ujio wake huo. Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo anatuhakikishia makazi ya milele, ambapo tutaishi katika ushirika naye pamoja na Baba na Roho Mtakatifu. Maisha ya hapa duniani ni ya mpito tu. Tunajua kuwa makao yetu ya kudumu yako mbinguni, na duniani tunapita tu, naye amwekwisha tuandalia makao hayo ya milele. Hii inatufundisha kutoweka mioyo yetu yote katika mambo ya ulimwengu huu ambayo kimsingi ni ya kupita tu. Kristo akiwa anatuandalia makao, anatualika nasi tusilale kiroho, viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu zapaswa daima kuwa zimewaka. Tukitambua hilo, tutafanya kazi kwa moyo, kwa juhudi na maarifa lakini tukiwa na matazamio ya kujenga na kuwekeza katika makazi yetu ya kudumu mbinguni. Lakini pia Kristo anatupa moyo kwamba hata mateso na kifo sio mwisho.  Tunapojua kuwa Yesu ameandaa mahali, kifo kinakuwa ni kuhama tu kutoka kwenye chumba cha muda, au nyumba ya kupanga ya wageni hapa duniani na kuelekea kwenye makazi ya kudumu yenye amani katika uzima wa milele. Hii inatupa faraja ya kweli hasa tunapoomboleza, au kupitia katika magumu na hofu. Tuishi tukijua kabisa kwamba dunia hii si makazi yetu. Kiburi, chuki, visasi, majivuno, mali, utajiri, vyeo na mamlaka, visitufunge macho tukaona kama ulimwengu huu ndiyo tumekwishakufika. Vitu vya dunia hii tutaviacha vyote, tupo safarini na tunaishi katika nyumba ya kupanga ya wageni.

Wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu

Sababu ya nne: Kristo Yesu alipaa kwenda kwa Baba na huko yeye kama kuhani wetu mkuu anatuombea sisi kwa Baba. Waraka kwa Waebrani unatueleza juu ya Kristo kuhani wetu mkuu ambaye kwa sadaka yake Msalabani aliingia Patakatifu pa patakatifu, aliingia mbinguni hasa aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu (Ebr 9:24). Yeye ndiye kuhani mkuu anayetufaa sana (Ebr 14:14-15), kwa kuwa alitwaa hali yetu ya kibinadamu, akawa mmoja wetu sawa na sisi isipokuwa hatukutenda dhambi. Kumbe Kristo anajua mahangaiko yetu, anajua jinsi tunavyopambana na dhambi na udhaifu wetu, anafahamu changamoto zetu zote na kwa kuwa alikua sawa na sisi basi yeye anatuombea daima kwa Baba. Kwa kupaa kwake mbinguni Kristo kuhani wetu mkuu anakuwa sasa mpatanishi na mtetezi wetu kwa Mungu. Ndugu mpendwa, Kama Yesu anavyotusimamia na kututetea mbele ya Baba, na sisi tunaitwa kuwa watetezi wa wenzetu katika maisha ya kila siku. Tusiwe watu wa kusengenya, kuhukumu, kuumiza, kukandamiza, kudhulumu au kufurahia maanguko au maumivu ya watu wengine.  Badala yake, tuwe watu wa kuwakingia kifua wanyonge, kuwaombea wanaopitia magumu na mkato wa tamaa, tujifunze kusemea mema ya wengine. Je katika maisha yangu, katika cheo changu, katika kazi zangu, katika utumishi wangu, nimekua mtu wa kuumia na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine? Ninaona uchungu kwa maumivu niliyowahi au ninayowasababishia wengine? Ninawaombea wengine hata kama nami nilishapitia nyakati za maumivu? Kristo aliteseka, akafa, akazikwa, lakini kwa kufufuka na kupaa kwake mbinguni bado ametukumbuka na anatukumbuka na kutuombea daima sisi ambao kwa sababu ya dhambi zetu alikufa. Roho Mtakatifu atusaidie tuwe tayari kuwa watetezi wa wengine na kuishi kwa ajili ya wengine.

Mtakuwa ni mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia
Mtakuwa ni mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia   (ANSA)

Sababu ya tano: Kristo alipaa Mbinguni ili kubadilisha namna ya uwepo wake kati yetu, sasa anadumu nasi katika Utume wa Kanisa, kwa watu wa Mataifa yote. Katika somo la kwanza na somo la Injili Takaitifu, Kristo aliwaahidi mitume zawadi ya Roho Mtakatifu, na kisha kuwapa utume mpya ambao kimsingi ndio utume wa kanisa hata sasa kwamba, “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote na Samaria na hata miisho ya dunia. Mwinjili Mathayo anatuhabarisha kwamba, Kristo aliwaamuru mitume wake kwenda Galilaya, mpaka kwenye mlima ule aliowaagiza. Ni pale pale alipoanza utume wake kati ya watu wa mataifa ndipo hapo hapo hapo anawatuma mitume kuendeleza kazi hiyo kabla ya kupaa kwenda kwa Baba. Sasa Utume mpya wa Kanisa si kwa Wayahudi pekee bali ni kwa watu wa mataifa yote. Kwa kuwarudisha Galilaya kwenye mlima ule ule alipowafundisha Heri za Mlimani, Yesu alikuwa anawaonesha kuwa safari yao haijaisha bali sasa inachukua sura mpya. Wanarudi walipoanzia ili kutumwa sasa kwenda kwa mataifa yote. Ni mitume kumi na mmoja, ishara ya jeraha la kukosekana kwa Yuda ambaye alimsaliti Bwana. Wengine wanamwamini na wengine bado walikuwa na hofu, licha ya hayo Kristo atawaimarisha wote na kuwapa utume mpya. Ndugu mpendwa, mwinjili Luka katika somo la kwanza pia anatupa simulizi hili la kupaa mbinguni kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na anamwandikia Theophilos, yaani mpendwa wa Bwana. Mpendwa huyu wa Bwana ni mimi na wewe, ni wale wote wanaosikia habari hizi hata sasa, ni wale wale walio dhaifu kama hawa mitume, ni wale wale ambao nyakati fulani tunaamini na nyakati nyingine tunapoteza imani, ndio sisi tulio ndani ya kanisa, tunaopokea wito huu kila siku wa kuwa mashuhuda wa Kristo.

Mitume wa Yesu: Mashuhuda wa Injili ya Kristo!
Mitume wa Yesu: Mashuhuda wa Injili ya Kristo!   (@VATICAN MEDIA)

Mitume wanapokea uwezo wa Roho Mtakatifu na wanatumwa sio tu kuwafundisha watu kuyashika yote aliyotuamuru Kristo. Kristo anatuahidi uwepo wake wa kudumu pamoja nasi, atatupa nguvu ya kuishi huo ushuhuda wa injili si tu kwa maneno bali kwa maisha yetu. Kristo ametuita ili kutuimarisha kwa ajili ya utumishi wake. Ni kwa njia ya uwepo wake katika kanisa, katika Neno lake na katika sakramenti zake tunaendelea kila siku kuimarishwa na kutumwa ili tuendelee kumhubiri Kristo hasa kwa mifano ya maisha yetu. Wewe u mpendwa wa Bwana, pokea wito wa kuwa shuhuda wake, kila siku ya maisha yetu.Hitimisho: Sisi sote tu mashuhuda wa Fumbo la Pasaka. Kwa njia ya Ubatizo wetu tunakiri fumbo hili kubwa la Imani yetu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, tunapata nguvu ya kuiishi na kuishuhudia Imani yetu. Kristo hajatuacha yatima, amekwenda kutuandalia makao ili alipo yeye nasi tuwepo. Yupo kati yetu, katika nyakati mbalimbali za maisha yetu, tuwapo hapa safarini kuelekea kule alipo yeye. 

Tafakari Kupaa Bwana
15 Mei 2026, 15:44