Tafuta

Sherehe ya Pentekoste: Siku ya Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; Ni Siku ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu ni Siku ya Kuzaliwa Kanisa! Siku ya Waamini Walei Sherehe ya Pentekoste: Siku ya Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume; Ni Siku ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu ni Siku ya Kuzaliwa Kanisa! Siku ya Waamini Walei  (@Vatican Media)

Sherehe ya Pentekoste: Zawadi ya Roho Mtakatifu; Nguvu ya Mungu

Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka kabisa pa kumjua Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; Katika Mapokeo ambayo Mababa wa Kanisa siku zote ndio Mashuhuda wake halisi, Katika Mamlaka fundishi; katika Liturujia ya Sakramenti: kwa maneno na alama zake ambamo Roho Mtakatifu anawaingiza waamini katika ushirika na Kristo; Katika sala, karama na huduma zinazolijejenga...

Na Padre Daniel R. Ntakwizile, - Roma.

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka kabisa pa kumjua Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; Katika Mapokeo ambayo Mababa wa Kanisa siku zote ndio Mashuhuda wake halisi, Katika Mamlaka fundishi ndani ya Kanisa “Magisterium”; katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa kwa maneno na alama zake ambamo Roho Mtakatifu anawaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu, Katika sala ambako anawaombea; katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika Ishara na maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na kuendeleza kazi ya ukombozi. Rej. KKK 683-730. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 anafanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi na mashirika pamoja na makampuni ya uhalifu.

Sherehe ya Pentekoste ni siku ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu
Sherehe ya Pentekoste ni siku ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu   (@Vatican Media)

Leo ikiwa ni Dominika ya Pentekoste, Mama Kanisa anatualika wote kwa pamoja kusheherekea utimilifu wa ahadi ile ya Kristo kwetu, ya kutuletea Mungu Roho Mtakatifu katika maisha yetu sisi wanadamu, ambaye atauhakikishia ulimwengu wetu huu katika habari zote zihusuzo dhambi, haki na hukumu (Yoh.16:8). Hivyo sherehe hii ya Pentekoste kwa namna ya pekee, inaunadi ujio huo wa Mungu Roho Mtakatifu ulimwenguni. Mungu Roho Mtakatifu aliye Nafsi ya Tatu ya Mungu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, anafahamika kwa jina lingine kama ‘Nguvu ya Mungu’, na kwa sababu hiyo, katika sherehe hii ya Pentekoste ya leo, ambayo Roho huyo, Nguvu hiyo inashuka tena kwetu, Mama Kanisa kupitia ujumbe wa Neno la Mungu anatudhihirishia wazi ya kuwa, ‘Pasipo Nguvu hiyo ya Mungu kwetu, Hakuna Jema Linaloweza Kufanyika’. Katika Injili Takatifu, Kristo anapowatokea wanafunzi wake waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, anawatoa hiyo hofu kwanza na kishapo anawapatia Nguvu ya Mungu, anawapatia Roho Mtakatifu, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu…’. Na baada ya kuwapatia Nguvu hiyo ya Roho wa Mungu, wanapata sasa uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Uwezo huo wa kuwapatanisha watu na Baba, uwezo huo wa kuwafungia pia watu dhambi zao ili wajirudi na kumrudia Baba, ni jambo lenye kupendeza machoni pa Mungu, ni jambo jema, na linawezeshwa na Nguvu hiyo ya Mungu; ‘Pasipo Nguvu ya Mungu kwetu, Hakuna Jema Linaloweza Kufanyika’.

Roho Mtakatifu ni chemchemi ya upendo, umoja na ushirika
Roho Mtakatifu ni chemchemi ya upendo, umoja na ushirika   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Dhana hiyo inajidhihirisha pia hata katika somo la kwanza toka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Tunaona ambavyo wafuasi wa Kristo walivyokuwa katika ile nyumba ambapo baadaye uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi ukaja na kuijaza nyumba yote, na Roho Mtakatifu akawashukia kila mmoja kwa ishara zilizotambulikana kama ndimi za moto, na kishapo wote wakaanza kunena kwa lugha mbalimbali juu ya matendo makuu ya Mungu. Unenwaji huu wa matendo makuu ya Mungu, na utangazwaji wa habari njema ya Kristo Mfufuka kwa watu wa mataifa mbalimbali kwa lugha zao wenyewe, ni tendo lenye kupendeza machoni pa Mungu, ni tendo jema, na limewezeshwa na Nguvu hiyo ya Mungu; ‘Pasipo Nguvu ya Mungu kwetu, Hakuna Jema Linaloweza Kufanyika’. Wapendwa ndugu zangu, hata Mtume Paulo mwenyewe katika somo la pili tulilosikia toka katika Waraka wake wa Kwanza kwa Wakorintho, anaanza kwa kusema bayana kabisa ya kuwa, ‘Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu’, kwa maneno mengine, hakuna mtu yeyote awezaye kumshuhudia Kristo kwa maneno na mifano ya maisha yake, asipowezeshwa na Roho Mtakatifu, asipowezeshwa na Nguvu hiyo ya Mungu. Ushuhuda wa Kristo Mfufuka kwa maneno na mifano ya maisha ya Mkristo, ni jambo la kupendeza sana machoni pa Mungu, ni jambo jema, na linawezeshwa na Nguvu hiyo ya Mungu; ‘Pasipo Nguvu ya Mungu kwetu, Hakuna Jema Linaloweza Kufanyika’.

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu, Ushuhuda, Mwanzo wa Kanisa
Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu, Ushuhuda, Mwanzo wa Kanisa   (@VATICAN MEDIA)

Baada ya kulielewa hilo, swali laweza kuja; Tunaipataje hiyo nguvu ya Mungu katika maisha yetu, ili tuweze kufanya mambo mema muda wote? Wapenda taifa la Mungu, Nguvu hiyo ya Mungu ambaye ni Roho Mtakatifu, tayari ameshakuja kwetu; Ameshakuja kwetu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, na kwa namna ya pekee pia ameshakuja kwetu kwa Sakramenti ya Kipaimara. Roho huyo (ama Nguvu hiyo), tayari ameshakuja kwetu tangu kuanzishwa kwa Kanisa, na anaendelea kutembea nasi milele akitukumbusha daima juu ya habari ya dhambi, haki na hukumu. Kwa maneno mengine, tunayo tayari hiyo nguvu ya Mungu ndani yetu. Changamoto yaweza kuwa, ‘Kama tunayo tayari hiyo Nguvu ya Mungu, kwa nini basi wakati fulani tunashindwa kutenda mema?’ Kwa nini tunaendelea kushuhudia vita na migogoro mingi ulimwenguni? kwa nini tunaendelea kuuana na kupotezana kwa sababu ya madaraka fulani katika utawala? Kwa nini baadhi yetu tunachukiana na kutakiana mabaya, Kwa nini wakati fulani hakuna jema tunaloliweza kulifanya licha ya Nguvu hiyo ya Mungu kuwepo ulimwenguni?’

Hii ni Siku ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu
Hii ni Siku ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu   (@VATICAN MEDIA)

Mtume Paulo katika Waraka wake huohuo kwa Wakorintho anapohimiza juu ya uelewa wa utofauti wa karama na vipaji vyetu, na kutuonesha kuwa asili ni Roho yuleyule mmoja, kwa maneno mengine anataka kutuambia kuwa, shida siyo Mungu katika maisha yetu kwa sisi kufanya ubaya, bali ni sisi wenyewe tunapoanza kujipambanua na asili tofautitofauti, tunapoanza kujipambanua na utofauti wa maweza yetu, nguvu zetu, na mamlaka yetu tukidhani kuwa sisi tu bora zaidi kuliko wengine, na kuliko mataifa mengine; Sisi tuna Roho zaidi kuliko wengine; Sisi tumebarikiwa zaidi kuliko wengine na kadhalika; tukisahau ya kuwa Ukristo wetu, na zaidi sana ubinadamu wetu hauna utaifa wala hauna utamaduni; Roho wa Mungu vilevile, hana utaifa wa utamaduni, hivyo tuwe Wayunani ama tuwe Wayahudi; Tuwe wa Afrika ama tuwe Wazungu; Tuwe wa Asia ama tuwe Wamarekani; Tuwe Wachaga ama tuwe Wangoni n.k, sote ni watoto wa Baba mmoja, na zaidi sana, sote tulinyweshwa Roho mmoja, aliyekuja ulimwenguni kwa ajili ya walimwengu. Hivyo leo tunapousheherekea ujio wa Roho huyo ulimwenguni, tufishe hizotofauti zetu, tujitahidi kila mmoja kwa nafasi yake kumruhusu Roho huyo aingie katika undani wa maisha yake, ili amsaidie kutenda yote vema, kwa maana pasipo Yeye huyo, hata kama tutafanya mengi makubwa, kwa hakika hakuna jema litakaloweza kutoka kwetu. Pasipo Roho wa Mungu katika maisha yetu, ‘Pasipo Nguvu hiyo ya Mungu kwetu, Hakuna Jema Linaloweza Kufanyika toka kwetu.’ Nawatakieni nyote Pentekoste Njema!

Sherehe ya Pentekoste 2026
22 Mei 2026, 18:00