Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Fumbo la Mwili na Damu Azizi ya Yesu
Na Padre Octavian O. Hinju, CP. Jordan University, - Morogoro.
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya imani. Kwa njia ya mageuzo hutendeka: “mageuzo-uwamo” “transubstantiatio” ya mkate na divai kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Chini ya maumbo yaliyogeuzwa ya mkate na divai yumo Kristo Yesu mwenyewe, hai na mtukufu kwa namna iliyo kweli, halisi na ya uwamo kamili, Mwili wake na Damu yake pamoja na Roho yake na uungu wake. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya ushirika, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa umoja na upendo huu, unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Rej. KKK 1413. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; Zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Ni kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku tarehe 6 Juni 2026 anafanya mkesha na vijana wa kizazi kipya kutoka Hispania, kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo, yaani Ekaristi Takatifu: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini inayoadhimishwa Dominika tarehe 7 Juni 2026. Hii ni fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha imani yao katika Fumbo hili kuu la Ekaristi Takatifu, kwa kuunganisha sauti za nyimbo kama kielelezo cha moyo wa shukrani, kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake.
Ni wito kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwani Mwenyezi Mungu kwa wingi wa baraka na neema zake ni Mhusika mkuu, lakini anategemea pia ushiriki wa waamini katika kuganga na kuponya magonjwa ya waamini kiroho na kimwili. Kristo Yesu ni daktari wa roho na mwili! Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Yesu Kristu, Mungu-Mtu katika maumbo ya mkate na divai (Yoh. 6:1-71, Mt. 26:26-28). Kanisa kwa nyakati zote linafundisha kwamba ‘Mwokozi wetu, katika karamu ya mwisho usiku ule alipotolewa aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa yaani kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa na roho hujazwa neema, ana ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele. (KKK, 1323, SC, 47). Kumbe kwa mkristu, Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya kikristo. (LG, 11, KKK 1324). Ekaristi ni Karamu ya upendo, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo Yesu aliyeko kwenye Maumbo ya Mkate na Divai; Kumwabudu Kristo Yesu katika Sakramenti kuu; kwa kumtangaza na kumshuhudia kwa njia ya maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu kuzunguka maeneo mbalimbali kielelezo cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu katika maisha ya waja wake. Maandamano haya makubwa ni ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; mwaliko wa kujenga na kudumisha: Umoja na udugu wa kibinadamu; haki na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watoto, vijana na familia kushiriki kwa wingi katika maadhimisho haya, kielelezo cha uwapo angavu na endelevu kwa watu wa Mungu.
Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu: Leo Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Neno la Mungu katika Liturujia ya Sherehe hii linatutafakarisha kuwa, Ekaristi takatifu ni ishara endelevu ya uwepo wa kristo miongoni mwa watu wake. “Ekaristi Takatifu ni Ishara ya Upendo na Ukarimu wa Kimungu kwa wanadamu, ambapo kwa tendo la kiekaristi Mungu Baba anaendelea kwa nyakati zote katika kila adhimisho la misa kumtoa kwetu Mwanae wa pekee awe ni chakula cha uzima wetu (Yoh. 3:16).” Kristo aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu siku ya Alhamisi Kuu jioni kabla ya kuteswa (1Kor. 11:23), ili ibaki kama kumbukumbu ya daima ya uwepo wake Katikati ya watu wake. Katika karamu ya mwisho, usiku ule Bwana Yesu alipotolewa, alitwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wafuasi wake akisema: “Huu ndio mwili wangu utakao tolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe cha divai, akasema: “Hiki ni kikombe cha damu yangu, damu ya agano jipya la milele linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka mimi (1 Kor. 11:23-25). Ekaristi ni moyo wa maisha na utume wa Kanisa. Katika Ekaristi, Kristu mwenyewe yupo na watu wake katika fumbo la Pasaka. Ndio maana ‘Mwokozi wetu, katika karamu ya mwisho usiku ule alipotolewa aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa yaani kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa na roho hujazwa neema, ana ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele. (KKK, 1323, SC, 47).
Kumbe kwa mkristu, Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya kikristo. (LG, 11, KKK 1324): Msingi wa maisha ya kikristu ni Yesu mwenyewe anaye jifunua kwetu katika Ekaristi takatifu. Kwa hiyo, Yesu ambaye ndio Ekaristi anakuwa kwetu ni kiini cha maisha ya kikristu. Ekaristi ni karamu ya upendo wa Mungu kwa wanadamu, yaani pendo lisilo na kikomo. Kwani kwa fumbo la umwilisho na kazi yake ya ukombozi sisi tumeponywa na kuitwa kushiriki maisha mapya, maisha ambayo yanatufunga pamoja kama wana wa Mungu na warithi wa maisha katika Utatu Mtakatifu. Ndio maana kwa sababu hii Ekaristi inakuwa ni kiini na taji la Imani ya kikristo. Kwa Sakramenti hii Kristu anajitoa kwetu nasi tuna kimbilia kwake. Ekaristi sio tu alama ama sherehe bali ni sakramenti ambayo kazi ya Kristu ya ukombozi na zawadi za kimungu zinatufikia sisi sote. Itakumbukwa kuwa sherehe hii kwa kawaida hutakiwa kuadhimishwa siku ya Alhamisi mara baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu, lakini kwa sababu za kichungaji, katika majimbo mbalimbali na mahali pengi duniani huadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Mama Kanisa ameamua hivyo ili kuwapa Watoto wake yaani jamii nzima ya waamini nafasi ya pekee sana ili kumfurahia, kumsifu, kumwabudu, kumtukuza na kumpa Mungu heshima ya pekee katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa maandamano yanayofanyika baada ya Misa Takatifu ili kuliishi, kulitafakari, kulishuhudia na kuonesha umuhimu na uhitaji wa Fumbo hili Takatifu katika Maisha yetu ya kiroho. Maandamano ya Ekaristi Takatifu tunayo yafanya leo Yesu wa Ekaristi akiwa ndani ya Montransi ni ukumbusho wa wana wa Israeli walipotembea na sanduku la agano kuelekea nchi ya Ahadi hata wakafunikwa kwa wingu ili jua lisiwachome wakati wa mchana (Yosh. 3:3,5); lakini pia maandamano ni ukumbusho wa Yesu mwenyewe anaye watokea na kuandamana nao wanafunzi wale wawili kuelekea kijijini Emau (Lk. 24:13-35). Leo waamini wanaalikwa kuonesha moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo Yesu katika hija za maisha yao hapa duniani, ili kwa Sakramenti ya kitubio na maungamo iwe kwao ni njia ya kujiandaa kikamilifu kumpokea Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai.
Kwingineko Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Juni 2025, alifundisha akisema hivi, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, bila kuona aibu au kuruhusu uvivu wa roho uwatawale bali wajitokeza kwa wingi katika maandamano ya Ekaristi Takatifu kwenye Parokia zao. Matamasha mbalimbali ya nyimbo za Ekaristi Takatifu yaendelee kupyaisha ushuhuda wa upendo wao kwa Kristo Yesu na hivyo kuwa tayari kujifunua katika mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha. Kristo Yesu, katika maumbo ya Mkate na Divai, anaendelea kuwa kati pamoja na wafuasi wake, huku akiwakirimia nguvu ya kushinda kishawishi cha kukata na kujikatia tamaa, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kwani hiki ni kielelezo makini cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo katika maisha ya waja wake, Kristo anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega. Huyu ni Kristo Yesu anayefanya hija ya imani pamoja na waja wake. Kwa mantiki hiyo, Ekaristi Takatifu inatukirimia na kutupa waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, ya uzima na utukufu wa Baba wa milele huko mbinguni.
Ndugu wapendwa, Ekaristi Takatifu inajenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwani uwepo wa kanisa mahalia au lile la kiulimwengu usingeweza kufikirika bila kuwepo kwa Ekaristi Takatifu. Vilevile hakuna jumuiya ya kikristu inayoweza kujengwa kama haina msingi wake katika maadhimisho ya Sakramenti Takatifu ya Ekaristi Takatifu (PO, 6). Hii ni kutokana na ukweli kwamba, “Sakramenti zote, kama vile huduma zote za kikanisa na matendo ya kitume, zimeunganika kiundani na Ekaristi takatifu na huelekea kwayo. Maana ndani ya Ekaristi takatifu yamo manufaa yote ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, aliye Pasaka yetu na mkate ulio hai; naye, kwa njia ya Mwili wake (carnem suam) uhuishwao na Roho Mtakatifu na yenye kuhuisha, anawapa uzima wanadamu ambao kwa njia hii wanaalikwa na kuhimizwa kujitoa wenyewe pamoja naye, na kutoa pia matatizo yao, na viumbe vyote. Kwa sababu hii Ekaristi huwa kama chemchemi na kilele cha uinjilishaji wote, hivi kwamba wakatekumeni wanaingizwa polepole katika kushiriki Ekaristi, na waamini waliokwisha tiwa muhuri wa Ubatizo mtakatifu na wa Kipaimara wanaingizwa kikamilifu katika Fumbo la Mwili wa Kristo (Corpori Christi) kwa njia ya Ekaristi (PO, 5). Kumbe, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake takatifu sana inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Historia inasimulia hivi, kwamba Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ilianzishwa rasmi katika Kanisa kutokana na uwepo na kusambaa kwa ibada mbalimbali kwa heshima ya Ekaristi Takatifu, uwepo halisi wa Mungu katika maumbo ya mkate na divai mapema katika karne ya 13AD. Kwa kusaidiwa na wanataalili mbalimbali na viongozi wa Kanisa kwa wakati huo, Sherehe hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1246 katika Jimbo la Liége huko Ubelgiji ikijulikana kama “Corpus Christi”, yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo. Mwaka 1264 Baba Mtakatifu Urbano IV aliidhinisha Sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa lote la kiulimwenguni. Alimwomba Mtakatifu Thoma wa Akwino kuandika nyimbo na machapisho mbalimbali ya kiliturujia kwa ajili ya sherehe hii kama vile “Pange Lingua, Tantum Ergo na Adore te.”
Mwaka 1263, uliotokea muujiza wa Ekaristi Takatifu huko Bolsena, nchini Italia ambapo Hostia Takatifu ilivuja damu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu wakati ambapo Padre aliyeadhimisha alikua na mashaka juu ya uwepo halisi wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Muujiza huu ulipelekea kukua na kusambaa kwa haraka kwa ibada kwa Ekaristi Takatifu, na kwa namna ya pekee Sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Baadaye Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) walifundisha kuwa, “Tunapaswa kumpa heshima Bwana wetu Yesu katika Ekaristi Takatifu hadharani ili wale wanaotazama Imani ya Wakristo Wakatoliki waweze kuvutwa na Yesu Ekaristi Takatifu, na kuweza kuamini katika Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai na mzima katika Fumbo Takatifu sana la Ekaristi Takatifu” Hii ilitokana na kuwepo kwa mafundisho mbalimbali ya uzushi juu ya Ekaristi Takatifu juu ya uwepo halisi wa Kristo katika maumbo ya Mkate na divai, kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya Ibada ya Misa Takatifu na maandamano ya Ekaristi Takatifu. Katika marekebisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: 1962-1965, Sherehe hii iliunganishwa na Sherehe ya Damu Takatifu sana ya Yesu ambayo huadhimishwa tarehe 1 Julai, ili kusisitiza taalimungu ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Na hivyo jina lilibadilika kutoka Corpus Christi yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo na kuitwa “Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi”, yaani Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo na ndivyo inavyojulikana hata sasa. Leo tuna sherehekea Imani yetu juu ya uwepo halisi na wa kweli kabisa wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai ambapo ni Kristo mwenyewe anaye toa mwili wake kama Chakula na Damu yake kama kinywaji kwa ajili yetu. Ndio maana Mzaburi alipoyatafakari hayo alisali hivi “nimewalisha kwa unono wa ngano, nimewashibisha kwa asali itokayo mwambani.” (Zab. 81:16), wimbo wetu wa mwanzo siku hii ya leo. Kadhalika Kristu, aliwapa Mitume wake mamlaka ya kuadhimisha Fumbo hilo Takatifu kwa ukumbusho wake mpaka atakaporudi tena (Rej. Mt. 26:26-29; Mk. 14:22-25; Lk. 22:14-20; 1 Kor. 11:23-26, Yoh. 6). Hili ndilo Adhimisho la Ibada ya sadaka ya Misa Takatifu tunaloadhimisha kila siku, kama ukumbusho wa sadaka ya Kristo pale msalabani. Ndugu wapendwa, labda tujiulize ni nini kinatokea katika mageuzo wakati wa ibada ya misa Takatifu? Katika ibada ya Misa Takatifu, mkate hugeuzwa kuwa mwili wa Kristo na Divai kuwa Damu ya Kristo. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Trento wanafundisha hivi, “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba huu ndio mwili wangu, akautoa mwenyewe kwa namna ya mkate na damu kwa namna ya divai. Hivyo kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake.” Uwepo huu halisi na kweli katika maumbo haya ya mkate na divai huanza katika mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwapo. Hivyo, Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao. Kwa jinsi hii, kuimega Ekaristi Takatifu hakumgawanyi Kristo hata kidogo. Uwepo wa Yesu unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika hata katika kila tone la damu yake, uwepo wa Yesu umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima (Rej. KKK 1376-1377).
Somo la Kwanzani kutoka katika Kitabu cha Kum. 8:2-3; 14-16a. Somo hili linaelezea kwa kina hali ya maisha ya wana wa Israeli huko jangwani. Wakiwa jangwani, walijifunza kumtegemea Mungu kwa kila kitu. Mungu kama Baba mwenye huruma na upendo, alijifunua kwao na kuwalisha mana chakula alicho kitengeneza yeye mwenyewe. Mana ilikuwa ni kielelezo cha Ekaristi itakayo kuja kuadhimishwa kwa vizazi vyote. Kama ambavyo wana wa Israeli hawakuweza kuishi bila mana sisi nasi hatuwezi kuwa na uzima pasipo Ekaristi, Sine Eucharistia non possumus, sine Dominico non possumus. Kwa nyakati zote hata ukamilifu wa dahari, Bwana ataendelea kutulisha kwa upendo akisema “inuka ule vinginevyo safari hii itakuwa ngumu kwako (1 Wafalm. 19:7). Ekaristi takatifu ni kifungo cha umoja ndio maana Paulo Mtume katika somo la Pili (1 Kor. 10:16-17) anatukumbusha kuwa ndani ya Ekaristi tunampokea Yesu mzima hivyo tunaungana naye. Kwa muungano huu Pamoja na Kristu, wakristu wote huunda umoja kati yao. Kumbe, sisi nasi kwa maisha safi na adilifu tuangalie tusije tukavunga muungano huu na umoja huu na Kristu ili tuweze kudumu nae hata mwisho. Nalo somo la Injili ya leo (Yoh. 6:51-58) inatuonyesha tusadiki ukweli kuwa Kristu Yesu ni chakula cha kweli na cha uzima, kwa sababu ametoa uzima wake ili kutupa sisi uzima wa kimungu. Tunapaswa kumpokea Yesu katika Ekaristi takatifu tukitaka kupata uzima wa milele na kushiriki furaha za mbinguni. Tunapoendelea kumtembeza Kristu katika mitaa mbalimbali tumuweke kwanza mioyoni mwetu ili awe kwetu ni dira na kielelezo cha maisha. Tutambue kuwa Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, tunapaswa kulisadiki kwa dhati, tuliadhimishe kwa ibada na uchaji na tulimwilishe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Katika Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu ambaye kwa mapendo makubwa alimtoa kwetu mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo (Yoh. 3:16), akatwaa mwili na kukaa kati yetu (Wafil. 2:6-11), akashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake (Yoh. 1:14), na bado amebaki nasi kwa daima katika maumbo ya mkate na divai. Tuombe neema ya kudumu katika ushirika na Kristo, kwa kumpokea daima kwa imani na katika hali ya neema katika Ekaristi Takatifu ili tuweze kunufaika na matunda yatokanayo na kule kupokea kwetu Fumbo hili Takatifu. Amina. Tumsifu Yesu Kristu.