Mkutano:Kuzingatia hali ya kimataifa,Magnifica Humanitas,Sinodi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tafakari kuhusu hali ya kimataifa na maisha ya Makanisa mahalia, majadiliano ya mada muhimu katika waraka wa Magnifica Humanitas, na taarifa mpya kuhusu utekelezaji wa Sinodi, itakuwa kitovu cha Mkutano ulioitishwa na Papa Leo XIV unaotarajiwa kufanyika tarehe 26, 27 na 29 Juni 2026. Mada za mkutano huo ziliainishwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali, katika barua iliyotumwa tarehe 3 Juni 2026 kwa Makardinali wote wataoshiriki. Katika barua hiyo, Kardinali Re anaelezea kwamba Papa anatamani mkutano huo, kama ule uliofanyika tarehe 7-8 Januari mwaka huu, utumike kama "nafasi ya kusikilizana, kupambanua na kutafakari pamoja kuhusu masuala muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa leo."
Kardinali Re anakumbusha kwamba Papa Leo XIV anaona kuwa Mkutano na Makardinali ni kama fursa "ya kukusanya uzoefu na ushauri wa wajumbe wote wa Baraza la Makardinali" na kutegemea "msaada na usaidizi wa kila mmoja katika sehemu na majukumu mbalimbali ambayo wanahudumia Kanisa." Kwa sababu hiyo, anaandika, majadiliano yanapaswa kufanyika katika "roho ya kusikiliza, uhuru na umoja," na kukuza mchakato wa utambuzi wa pamoja. Katika kufafanua zaidi kuhusu Mkutano huo, kipindi cha kwanza kitazingatia hali ya kimataifa na ukweli wa Makanisa mahalia. Makardinali wataalikwa kushirikisha mateso, mivutano na changamoto zinazoathiri watu na jumuiya za Kanisa zilizokabidhiwa kwa uangalizi wao, pamoja na ishara za matumaini, uaminifu kwa Injili na matarajio ya upatanisho ambao wanaamini unapaswa kuwasilishwa kwa umakini wa Baraza hilo la Makardinali.
Magnifica humanitas
Kipindi cha pili na cha tatu kitajitolea kwa ajili ya waraka wa Papa Leo XIV wa Magnifica Humanitas, uliochapishwa tarehe 25 Mei 2026. Kipindi cha pili kitachunguza Sura ya Tano, yenye kichwa "Utamaduni wa Nguvu na Ustaarabu wa Upendo." Kardinali Re anakumbusha kwamba katika aya ya 182 ya waraka huo, Papa anaandika kwamba katika ulimwengu unaokisiwa na "utengano, vurugu na migogoro inayoongezeka," amani "si suala moja kati ya mengine, bali ni sharti la manufaa ya wote na mtihani wa ukomavu wa maadili ya watu."
Ulimwengu Uliojeruhiwa na Vita
Makardinali kutoka maeneo yaliyoathiriwa na vita wataalikwa kushiriki jinsi migogoro imeunda moja kwa moja na kwa uchungu uzoefu wao wa kichungaji, huku wengine wakiombwa kutafakari kuhusu kuibuka tena kwa "lugha, mantiki na desturi" zinazodhoofisha upatanisho na kuishi pamoja kwa amani. Majadiliano pia yatazungumzia jinsi Kanisa linavyoweza kuthibitisha leo "kushinda nadharia ya 'vita vya haki,' ambayo mara nyingi hutumika kuhalalisha vita yoyote," kama Papa Leo anavyoandika katika aya ya 192 ya hati hiyo, na ni njia gani za vitendo zinazoweza kuwasaidia watu na jumuiya za Kikristo kuhifadhi na kujenga amani. Kipindi cha tatu kitazingatia mada ya "kujenga katika wema," mtazamo unaounda utangulizi na hitimisho la Magnifica Humanitas. Washiriki watachunguza wito wa waraka wa kutafsiri mabadiliko ya wakati huu kwa mwanga wa Injili na kuelekeza utafutaji wa binadamu wa furaha na utimilifu kuelekea maendeleo kamili ya binadamu.
Utekelezaji wa Sinodi
Sehemu ya kwanza ya kikao cha mwisho itawapatia Makardinali taarifa mpya kuhusu utekelezaji wa Sinodi, hasa kwa mwanga wa hati ya hivi karibuni, kuelekea Mikutano ya Sinodi 2027–2028: Hatua, Vigezo na vyombo vya Maandalizi. Sehemu ya pili itajitolea kwa ajili ya mazungumzo ya wazi kati ya Makardinali na Papa, huku hatua zikipunguzwa kwa dakika tatu kwa kila moja. Kardinali Re pia alibainisha kuwa vikao vya Mkutano wa tarehe 26 na 27 Juni, vitafanyika katika Ukumbi wa Paulo VI na Ukumbi wa Sinodi. Mkutano huo utahitimishwa tarehe 29 Juni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ambapo Papa Leo XIV ataongoza Misa ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, atabariki pallia na kuwadhibitisha Maaskofu Wakuu wapya wa majimbo Makuu ya Majiji. Kama ilivyotangazwa hapo awali, hakutakuwa na misa ya pamoja tarehe 28 Juni 2026.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here