Askofu Bonaventura Bosco Gubazire Jimbo Katoliki la Kabale, Uganda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, tarehe 15 Julai 2026 ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Callist Rubaramira wa Jimbo la Kabale, Uganda la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Bonaventura, Askofu na Mwalimu wa Kanisa amemteuwa Mheshimiwa sana Padre Bonaventure Bosco Gubazire, M.Afr. kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kabale, Uganda. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Bonaventure Bosco Gubazire, M.Afr. alikuwa ni Gambera wa Seminari kuu ya “St. Martin of Tours Formation House” huko Ejisu, nchini Ghana. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Bonaventure Bosco Gubazire, M.Afr. alizaliwa tarehe 3 Machi 1974 huko Kitumba, Jimbo Katoliki la Kabale, Uganda. Baada ya masomo na malezi yake ya kitawa, tarehe 10 Agosti 2003 akapewa daraja Takatifu ya Upadre.
Baada ya Upadrisho wake alitumwa na Shirika huko Msumbiji kati ya Mwaka 2003 hadi Mwaka 2007, nchini Ufaransa mwaka 2008 na baadaye akatumwa kwenda kujiendeleza zaidi katika ujuzi na maarifa huko Dublin, nchini Ireland kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2010 na kujipatia shahada ya Uzamili katika Falsafa. Baada ya masomo yake, aliteuliwa kufundisha Falsafa Nyumba ya Malezi ya Lechaptois Formation House huko Balaka, nchini Malawi kati ya Mwaka 2013-2015. Na kunako mwaka 2014 alihudhuria Kozi ya Biblia huko mjini Yerusalemu na kati ya Mwaka 2016 hadi mwaka 2020 alitumwa kwenda nchini Ufilippin kuendelea na masomo ya ngazi ya juu na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha “San Carlos di Cebu” nchini Ufilippin.
Kati ya Mwaka 2017 hadi Mwaka 2022 alikuwa ni Mratibu na Mlezi wa maisha ya kiroho wa Marafiki wa Wamisionari wa Afrika na Mshauri wa Shirika, Barani Asia, huko Cebu, nchini Ufilippin. Kati ya Mwaka 2019 hadi 2020 aliteuliwa kuwa ni Gambera wa wa Seminari ya “Our Lady of Africa Formation House” huko Cebu, nchini Ufilippin. Kati ya Mwaka 2021 alikuwa ni Mkuu wa Taaluma katika Chuo Kikuu cha “Spiritan University College” huko Ejisu nchini Ghana. Tangu mwaka 2023 hadi mwaka 2025 alikuwa niMshauri wa Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Afrika: Ghana na Nigeria. Tarehe 15 Julai 2026 Kumbukumbu ya Mtakatifu Bonaventura, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa Mheshimiwa sana Bonaventure Bosco Gubazire, M.Afr. kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kabale, Uganda.
Itakumbukwa kwamba, Askofu Mstaafu Callist Rubaramira wa Jimbo la Kabale, Uganda alizaliwa tarehe 8 Februari 1950 Kijini Rubira Kyanamira. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 18 Mei 1975 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 15 Machi 2003 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kabale, Uganda na kuwekwa wakfu tarehe 8 Juni 2003. Kumbe, Askofu Mstaafu Callist Rubaramira amekuwa Padre kwa takribani miaka 51 na Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 23.