Tafuta

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora." Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora." 

Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, Kenya Kuanzia Tarehe 19-26 Julai 2026

Kaulimbiu inayonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Nairobi, Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kaulimbiu inayonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan Kongwe, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.

Kumbukizi ya Miaka 65 tangu kuanzishwa kwa AMECEA
Kumbukizi ya Miaka 65 tangu kuanzishwa kwa AMECEA

Askofu Charles Sampa Kasonde, wa Jimbo Katoliki Solwezi, Zambia ambaye ni Mwenyekiti wa AMECEA anasema, Mkutano huu unakuwa ni chemchemi halisi ya matumaini na wakati wa neema kubwa kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Hii ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana: Matatizo, changamoto na fursa katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya. Mababa wa Kanisa wanasema, Jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko mpya wa ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume huu inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia waamini ari na nguvu ya kuwa kweli ni mitume wamisionari tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Maaskofu zaidi 140 kutoka katika Majimbo 128 wanashiriki
Maaskofu zaidi 140 kutoka katika Majimbo 128 wanashiriki

Kwa namna ya pekee, waamini walei wanahamasishwa kuwa ni mitume wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; kwani ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika huduma makini kwa maskini wa kiroho na kimwili. Askofu Charles Sampa Kasonde anakaza kusema, huu ni muda wa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya ambao ni tumaini na jeuri ya Kanisa la leo na lile la kesho. Ni muda muafaka wa kujifunza kutoka kwa vijana kutokana na tajiriba yao; kutetea na kudumisha dhamana na utume wao katika Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kwa pamoja, AMECEA inataka kubuni sera na mbinu mkakati utakaomwilishwa katika vitendo, kwa kujenga madaraja imara ya umoja na ushirika ili kuvuta mipaka yao; kujenga matumaini katikati ya changamoto za Afrika Mashariki na Kati; haki kwa wote na utawala bora katika medani mbalimbali za maisha ndani na nje ya Kanisa.

AMECEA pamoja na Vijana wa Kizazi Kipya
AMECEA pamoja na Vijana wa Kizazi Kipya   (AFP or licensors)

Kwa upande wake, Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba wa Jimbo kuu la Kisumu na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, anapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha washiriki wote wa Mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA na kwamba, hii ni fursa ya pekee, dhamana na wajibu mtakatifu wa kichungaji wa watu wa Mungu nchini Kenya. Mkutano huu ni wakati wa neema kuu kwa Kanisa nchini Kenya, kwa kufungua malango ya nyoyo na akili zao kwa washiriki wote wa Mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA, ili kutafakari juu ya utume wao wa pamoja kama wabatizwa. Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba anamwomba Roho Mtakatifu apende kuimarisha ari na mwamko wao wa utume wa pamoja katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaozamishwa katika medani mbalimbali za maisha ya waamini. Maadhimisho ya Mkutano huu, iwe ni fursa ya kuimarika kiroho; kudumisha usalama, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; anawataka wajumbe wote kujisikia wako nyumbani nchini Kenya.

Mkutano Mkuu wa AMECEA 2026

 

17 Julai 2026, 16:31