Tafakari Dominika 14 ya Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu Masiha Mpole na Mnyenyekevu
Na Padre Octavian O. Hinju, CP. - Jordan University Morogoro.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 4 Julai 2026 amefanya hija ya kichungaji Kisiwani Lampedusa, Kusini mwa Italia kwa kutembelea Makaburi na kutoa heshima kwa Marehemu waliolazwa mahali hapa! Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, linasema tangu mwaka 2014 wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 32, 700 wamefariki dunia wakijaribu kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Kunako mwezi Oktoba 2013 watu zaidi ya 368 walifariki dunia kwenye Kisiwa cha Lampedusa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kusali katika ukimya na kuweka shada la maua kwenye Makaburi; amekutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji kwenye Mlango wa Ulaya: “Porta d’Europa” baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria wa Bandari Salama “Portosalvo.” Amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, watoto wagonjwa pamoja na watu wa kujitolea.
Kristo ni mfano na kielelezo cha urafiki wa kweli. Kama ilivyo kwa upendo, urafiki wa kweli huchukulia na kuvumilia yote pasi na kuhesabu mabaya ndio maana Kristo mwenyewe anasema ‘Ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu, (Yoh. 15:15). Rafiki wa kweli yuko radhi kujitoa sadaka ili kuokoa uhai wa mwingine. Kadhalika, rafiki mwema anatoa mfano mwema kwa rafiki zake kama tunavyosikia katika Injili ya leo Yesu anaposema “jitieni nira yangu mjifunze kutoka kwangu.” Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 14 ya mwaka A wa Kanisa katika kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yamesheheni ujumbe unaojielekeza katika kumwonesha kwetu sisi Bwana wetu Yesu Kristo kuwa ndiye Masiha mpole na mnyenyekevu. Huu ni utimilifu wa kinabii kwani tangu kale manabii waliagua juu ya ujio wake Kristu Mwana wa Mungu, Masiha na Mfalme mwenye haki. Hivyo nasi tumfuate yeye kwa kuishi maisha mema ya kiroho yaliyo sheheni upendo na utakatifu ili tujipate uzima wa roho zetu na heri ya milele. Masomo yetu yanatoa mwaliko kwetu kumkubali na kumpokea Kristu Masiha wetu na mkombozi anayetoa pumziko kwa waliochoka; ili kwa kuchota yale ya kimungu kutoka kwake sisi nasi tuweze siku moja kuwa naye huko ambako tunatumaini kuwa siku moja nasi tutafika, yaani mbinguni kwa Baba.
Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Nabii Zakaria (Zak 9:9-10). Somo hili linasimulia matukio ambayo kimsingi yanatukia siku ya Dominika ya Matawi yaani utabiri juu ya ufalme wa Masiha Bwana wetu Yesu kristu. Katika somo hili Nabii Zekaria anataja sifa za mfalme huyu ya kuwa ni mnyenyekevu hapandi farasi wa vita bali anatumia punda. Unyenyekevu ni mama wa fadhila zote, kwani mtu mnyenyekevu yuko radhi siku zote kujifanya Daraja ili wengine wapite na anajali siku zote mahitaji ya wengine bila kuweka mbele maslahi yake binafsi hata kama anao uhitaji mkubwa wakati huo. Mfalme mnyenyekevu anajitanabaisha kwa mtindo wa maisha yake yaliyo sawa na watu wa rika na tabaka zote hasa wale wa tabaka la chini ambao wengi ni watu duni na fukara. Hili linajionyesha kwani mfalme hapandi farasi wa vita bali mwanapunda. Punda ni mnyama anaye ashiria unyenyekevu na kujishusha kwa kiasi kikubwa. Kristu ndiye mfano halisi wa unyenyekevu kwani aliacha Fahari za mbinguni ili kuchukua ubinadamu wetu akishiriki kila kitu Pamoja nasi isipokuwa dhambi, “yeye kwa asili alikuwa sawa na Mungu, lakini hakuona kwamba kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikilia sana. Bali alikubali kuacha vyote, akachukua hali ya mtumishi, akazaliwa na umbo la wanadamu. Alipochukua umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii mpaka kufa, tena kifo cha msalaba. Kwa sababu hiyo, Mungu alimwinua juu kabisa, akampa jina ambalo ni kuu kuliko majina yote; ili kwa jina la Yesu, kila goti lipigwe, mbinguni na duniani na kuzimu; na kila ulimi ukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu (Walp. 2:6-11).
Kumbe ni kwa kuiishi vema fadhila hii ya unyenyekevu Mungu hutuinua kama tunavyo Sali hivi katika sala ya kolekta “Ee Mungu kwa njia ya unyenyekevu wa mwanao umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu ili hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi, wapate kuifikia furaha ya milele.’ Sifa nyingine ya Mfalme, yaani Kristu ni amani. Hili linaelezwa na uamuzi wa kutopanda farasi wa vita. Ni ishara wazi na kweli ya maridhiano ya dhati na utayari wa kupatana miongoni mwa jamii na ndugu waliokoseana. Hayati Baba Mtakatifu Francisco katika waraka wake kitume “Fratelli Tutti” yaani “udugu wa kibinadamu”, anaendelea kwa nyakati zote kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutochoka wala kukata tamaa kwa ajili ya kuombea amani duniani. Anasema kwa bahati mbaya, kuna maeneo ya vita ambayo yamesahaulika kwenye medani mbalimbali za Jumuiya ya Kimataifa. Kuna mapigano, machafuko, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbalimbali za dunia. Kama Baba alihubiri amani kwa viongozi wa nchi changa ya Sudani Kusini alipobusu miguu ya viongozi wakuu wa nchi akiwataka kutorudi tena vitani. Hata leo hii tunashuhudia bajeti kubwa za nchi zikielekezwa katika manunuzi ya silaha za maangamizi badala ya madawa ya matibabu na huduma nyingine msingi za kijamii kama vile elimu na barabara.
Naye Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” kuhusu mchakato wa uimarishaji amani kati ya watu wote katika ukweli, haki, upendo na uhuru” anasema, mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha mazuri na haki zinazohusu tunu za kimaadili na kiutamaduni. Haki ya kumwabudu Mungu kulingana na maongozi ya dhamiri nyofu, haki ya mtu kuchagua hali ya kuishi anayoipenda zaidi; haki zinazohusu uchumi; haki ya kuhama na kuhamia mahali pamoja na haki za kisiasa. Kuna uhusiano usiovunjika baina ya haki na wajibu wa kila mtu, kati ya watu mbalimbali; katika kushirikiana, mintarafu moyo wa uwajibikaji; watu kuishi katika jamii inayosimikwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru wa kweli. Hizi ni nguzo kuu zinazosimika mchakato wa amani ya kweli, mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu katika ujumla wao wanaounda jumuiya ya Kisiasa. Amani katika ukweli inafumbatwa katika mchakato wa kuheshimu utu na haki msingi za binadamu; kutafuta na kuuambata ukweli; uhuru wa kujieleza pamoja na uwepo wa mazingira bora ya kila mtu kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu. Iwapo jamii inaundwa katika misingi ya haki na wajibu; watu wanatambua haraka thamani za maisha ya kiroho na za kiakili, wala sio wagumu katika kuelewa ni nini maana ya ukweli, haki, upendo na uhuru na juu ya Mungu wa kweli. Huyu ni Mungu aliye nafsi ambaye ndiye mkuu kuliko maumbile ya binadamu. Hutambua kwamba, uhusiano wao na Mwenyezi Mungu unaunda msingi wa kweli wa maisha yao, yaani maisha ya ndani ya kiroho, na maisha ambayo wanaoishi katika jamii na wenzao. Amani na haki ni Watoto wawili wa baba moja ambao huwezi kuwatenganisha. Tutende haki ili amani iendelee kuwepo ulimwenguni.
Somo la pili linatoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 8:9, 11-13). Somo hili linaeleza ujumbe ambao pengine sio rahisi kuuelewa katika muktadha wa kawaida, yaani kuishi kwa mwili. Kwa Kadiri ya Paulo Mtume, kuishi kwa mwili tu maana yake ni kuishi katika hali ya dhambi. Ni kujisahau na kuusahau ukweli kwamba miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu hivyo tusimuhuzunishe Roho kwa kuishi tungali tumekumbatia dhambi. Kinyume chake kuishi kwa roho ni kuishi katika Imani na ubatizo na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ni kawaida sana sasa katika nyakati zetu hizi kuona na kushuhudia watu wakiigeuza miili yao kuwa chanzo cha kipato kwa kuitumia Kutenda yasiyo yafaa. Huku ni kumkosea mwenyezi Mungu na kusudi la kuumbwa kwetu. Kumbe tukiishi kwa mwili tu tutapokea na kuangamia kabisa bali tukiishi kwa roho tutaokoka na kuurithi uzima wa milele. Kiini cha somo hili ni kuhusu umuhimu wa maisha ya kiroho. Tunaagizwa hivi maisha yetu tuliyozoea kuita maisha ya kawaida, yaani yale ya kila siku, ni maisha yanayopaswa kujengwa juu ya msingi wa maisha ya kiroho. Yeyote yule asiye na maisha ya kiroho basi anajiweka katika hatari ya kuyaishi maisha yake kijuu juu sana pamoja na hatari ya kuyumbishwa na vionjo mbalimbali maishani. Maisha ya kiroho si ni tu msaada unaomfanya mtu aishi kama mtoto wa Mungu bali pia humuwezesha mtu kuyasimika maisha yake katika msingi imara. Tupokea ujumbe wa somo hili ili utusaidie kutambua vitu mbalimbali vinavyosaidia kukuza na kuimarisha maisha ya kiroho: kuuishi uwepo wa Mungu katika sala, Misa Takatifu na maisha ya sakramenti pamoja na kushiriki yale yanayoitwa mazoezi ya kiroho: mafungo, hija na uchaji mbalimbali katika vyama vya kitume.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 11:25-30). Leo Kristu anatoa mwaliko kwetu sote kumwelekea yeye ili atupe pumziko katika shida na mahangaiko yetu. Yesu anasema “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.” Huu ni mwaliko wa upendo wa kimungu kwa wanadamu, ni ishara wazi ya urafiki ambao unajali na kufikiri kuhusu watu wengine. Tangu zamani katika jamii na tamaduni za kiyahudi, Torati na sheria na miongozo yote ilifahamika pia kwa jina la “Nira.” Neno hili linapata tafsiri rahisi ya lile jembe la ng’ombe la kulimia. Yesu anaposema “jitieni nira yangu mjifunze kutoka kwangu” anatoa mwaliko kwa wafuasi wake kupokea upendo kama sheria mpya inayoongoza namna ya kuishi, “legis plenitudo caritas yaani upendo ni utimilifu wa sheria’ (Rum. 13:10). Kristu anatulika kujifunza kutoka kwake kwa maana yeye ameuishi upendo hadi upeo wake wa mwisho pale Msalabani, “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi, (Yoh. 13:34-35). Kwingineko wataalamu wa Maandiko Matakatifu wanatoa fasili ya sehemu hii ya Injili wakionesha namna ambavyo Yesu anaweka amri yake ya mapendo sawasawa na Torati ya kiyahudi. Mwinjili Mathayo anatueleza kuwa hata Yesu mwenyewe alijifahamu na kujiona ya kuwa ni Mwana halisi wa Mungu hivyo ana alika wale wote wanao endelea kusumbuliwa kwa ajili ya Injili na anaonyesha utayari wa kuwapokea kwake. Yumkini zipo nyakati Fulani katika maisha tuzongwa na mambo mengi kiasi cha kukata tamaa basi Kristu anauita kwake. Tunaposikia sauti ua wito wake tusikawie kumwelekea naye atatupokea kwa upendo mkubwa. Tuombe neema ya kumjua Kristu pekee naye atufae katika yote. Amina.