Tafakari Dominika 15 ya Mwaka A wa Kanisa: Utume wa Bahari 2026
Na Padre Octavian O. Hinju, CP. - Jordan University, - Morogoro, Tanzania
Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2026 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa makini kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia: Kumwomba, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu, kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini: mchango na sadaka ya watu hawa, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu: “Zaidi ya bidhaa na biashara: sura ya kibinadamu ya bahari” ni kauli mbiu inayokumbushia dhamana na wajibu mkubwa unaotekeleza na mabaharia na wavuvi sehemu mbalimbali za dunia. Mlango Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) ni moja ya njia muhimu na nyeti zaidi za Bahari kwa uchumi na biashara ya kimataifa, kwani inakadiriwa kupitisha zaidi ya asilimia 20% ya mafuta na gesi asilia duniani.Kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz kunachochea mfumuko wa bei na kupunguza ukuaji wa uchumi wa Dunia na katika hali mbaya zaidi kusababisha ongezeko la umaskini kwa watu milioni 32 na njaa kali kwa watu zaidi ya milioni 45.
Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu linasema, hii inaonesha ni kwa jinsi gani binadamu kwa asilimia kubwa anategemea huduma ya bahari kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wana utu, heshima na haki zao msingi wanavyotekeleza dhamana na utume wao katika mazingira yenye matumaini na hofu, mizigo na ustahimilifu, mahusiano na ndoto zinazostahili kuonekana, kuheshimiwa, na kuthaminiwa.Masomo ya Dominika hii yanabeba ujumbe unaotukumbusha kuhusu nguvu ya Neno la Mungu na mwaliko wa kuwa udongo mzuri ili litulie ndani yetu na kuzaa matunda. “Neno lako ni taa ya kuniongoza, na mwanga katika njia yangu. Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu, kwamba nitashika maagizo yako adili (Zab.119:105). Haya ni maneno yenye kubeba ndani mwake faraja kuu itokanayo na kujizamisha katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Neno la Mungu, ndilo ambalo linatufundisha, kutuongoza, na kutufanya kuwa wafuasi wa kweli wa Kristo. Katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kusongwa na giza la migawanyiko, vita, na mateso, Neno la Mungu ni mwanga unaoangaza njia yetu. Kwa hivyo, tutapata nguvu ya kuishi maisha ya haki na amani kwa kufuata Neno la Mungu kila siku. Leo ni Dominika ya Utume wa Bahari: sala kwa ajili ya mabaharia na wavuvi!
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya mwaka A wa Kanisa katika kipindi cha kawaida yanaelezea maana na umuhimu wa Neno la Mungu katika roho na maisha ya Mkristu mbatizwa. Ni mwaliko wa kuzama katika ukimya na tafakari ili kulielewa neno nalo litazaa matunda na kuleta mavuno mengi ya kiroho. Ni katika tafakari ya Neno ndipo tunapata kumuelewa Kristu. Leo Kristu anatoa mfano wa kawaida katika shughuli za kilimo, yaani udongo, mpanzi na mbegu. Anatoa nafasi kwetu kuchagua ni aina gani ya mbegu tungelipenda kuwa kati ya zile tatu. Kadhalika tuangukie katika aina ipi ya udongo ili sisi tulio mbegu zipandwazo na Mwenyezi Mungu tuweze kuzaa matunda mema. Leo tunaalikwa kusali ili kuomba neema ya kuwa mbegu zitakazo anguka penye udongo mzuri ili matunda yetu yawe ni ya kufaa sana kutiliwa mfano na kufurahiwa na wengi. Dominika ya leo kadhalika ni siku ya kimataifa ya sala na maombi kwa ajili ya Utume wa Bahari yaani mabaharia na wavuvi. Ujumbe mkuu wa Dominika ya Utume wa Bahari unalenga kuwakumbuka, kuwaombea, na kutambua mchango mkubwa wa mabaharia na wavuvi katika uchumi wa dunia na maisha ya kila siku. Tunafanya hivyo ili kwa msaada wa sala zetu za kikristu wavuvi watumie stadi za kazi zao na maisha adilifu kuwavutia watu wengine kwa Kristu kwani hata yeye mwenyewe aliwaita wavuvi watu wa tabaka la chini kabisa na kuwafanya kuwa wavuvi wa watu.
Huu ni mwaliko wa Kanisa na jamii kuonesha shukrani na kuwasaidia kiroho na kimwili watu hawa wanaofanya kazi katika mazingira magumu, kama wanavyoendelea kutiwa moyo na maneno ya Mzaburi “Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, Hao huziona kazi za BWANA, Na maajabu yake vilindini. Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake. Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya, (Zab. 107:23-26). Sala na maombi kwa mabaharia na wavuvi inalenga kuwa kumbusha wanadamu wote thamani ya kazi na kwamba zote zilenge utakatifu wa mwanadamu. Kumbe Mama kanisa anaendelea kutambua mchango mkubwa unaotolewa na jamii hii ya wavuvi na hatari wanazozipitia katika kutekeleza wajibu huu wa msingi kabisa wa kumkuza mwanadamu kimwili kwa mahitaji yanayo timizwa na mazao ya Bahari. Mama kanisa anapenda kuwaombea na kuwatia moyo ili hata mara moja wasichoke na kukata tamaa. Daima wadumu waaminifu tayari kusadaka maisha yao kwa ajili ya manufaa ya watu wa Mungu.
Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Is. 55:10-11). Hizi ni aya tatu zinazihitimisha kitabu cha pili cha Nabii Isaya kinachoanzia sura ya 40 mpaka sura ya 55. Katika somo hili Nabii Isaya anashuhudia nguvu ya Neno la Mungu kuwa haliwezi kurudi nyuma au kubadilika kama vile mvua inyeshavyo haina budi kustawisha mimea. Katika somo yanaelezwa matukio katika kipindi cha pili cha unabii wa Isaya wakati ambapo Wayahudi walikuwa uhamishoni Babeli. Wakati huo walikuwa kwenye masikitiko na kukata tamaa. Nabii Isaya, katikati ya karne ya 6 (kabla ya Kristu) anatokea na kutuliza mioyo ya waisraeli huko Babeli. Itakumbukwa kuwa jina Isaya maana yake ni “Wokovu hutoka kwa BWANA.” Maana ya jina tu ilitosha kuwapa faraja na tumaini wana wa Israeli. Nabii Isaya ni mwana wa Amozi mzawa ya Yerusalemu. Isaya ni mmojawapo wa manabii maarufu katika Agano la Kale (Is. 8:1) ambaye anashuhudiwa kuwa mwenye imani na kupenda watu wamtegemee BWANA peke yake. Tena Isaya alipenda na kusisitiza unyofu (Is. 1:4; 17; 3:9; 14-15; 5:8-23), na uadilifu katika jamii (Is. 7:4-7; 30:15; 37:6-7). Historia ya maandiko matakatifu inaeleza hivi ya kuwa unabii wa Isaya uligawanyika katika vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni kabla ya uhamisho. Wakati huu ndipo Isaya alipoitwa kuwa Nabii. Ni wakati ambao Israeli na Yuda zilikuwa na msukosuko kisiasa. Mataifa makubwa yalikuwa karibu kuwavamia hivyo watu walifanya mbinu na mipango ya kupata misaada ya kivita kutoka kwa mataifa mengine yaliyo makubwa. Isaya alipinga mipango hiyo, alikazia sana katika kumwamini na kumtegem
Nabii Isaya Alisema kwamba kutegemea mataifa ni kujiangamiza wenyewe (Is. 1-39). Isaya alitangaza kuwa Mungu atawapa uhuru, atawarudisha katika nchi yao wakae katika miji yao ya awali na watakuwa na hali mpya. Anawakumbusha uwezo wa Mungu ulio mkuu sana. Hayo yote yatatukia kupitia utabiri wa “Mtumishi wa BWANA” (Is. 40-55). Kumbe utabiri wake ulichukua muda kabla ya kutimia hali hii iliwafanya wakate tamaa juu ya uweza wa Mungu wa kuwakomboa. Isaya anatokea tena Katikati yao kuwatia moyo na kuwahakikishia kuwa Neno la Mungu halibadiliki nalo ni hakika na litatimia kwa wakati wake. Tena ni Dhahiri kwamba waisraeli watarudishwa katika mji wao mtakatifu kutoka utumwani Babeli kwa sababu Mungu aliahidi hivyo. Vilevile, katika somo hili la kwanza Isaya anatufundisha kwamba, Mungu habadiliki katika neno lake na kwamba akitamka huwa hivyo. Anasema hivi kama mvua inyeshavyo na kurutubisha mimea kadhalika sisi nasi tunaneemeshwa kwa Neno la Mungu. Tofauti na wanadamu, Nabii Isaya anamwelezea Mungu aliye ukweli halisi asiye badilika hata katika nyakati ngumu. Nasi tumwombe Mungu atujalie neema ya kubaki waaminifu hasa kwa ahadi zetu za ubatizo na Roho Mtakatifu tuliye mpokea. Utabiri kwamba Mungu atawarudisha Israeli katika miji yao ni ujumbe wa matumaini kwao na ishara ya huruma ya Mungu asiye angalia madhaifu yetu bali kwa huruma anatupatia nafasi ya pili ili kuweza kujipatanisha naye.
Somo la II ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:18-23). Somo hili linaelezea chanzo cha mateso na mahangaiko ya mwanadamu kuwa ni dhambi. Linasisitiza kwamba ulimwengu umelaaniwa kwa ajili ya dhambi ya binadamu. Dhambi huleta dhiki na mateso makubwa katika roho na maisha ya mwanadamu. Haya ni matokeo ya tamaa ya mwanadamu kutaka kumiliki kila kitu peke yake kiasi cha kuathiri viumbe wengine. Tutambue kwamba mtu anapotenda dhambi ingawa huitenda peke yake lakini matokeo yake huwafikia wengine pia, kumbe basi ni vema kuwa waangalifu juu ya matendo yetu ili badala ya kuwa laana kwetu na watu wetu basi yawe baraka na neema kwa jamii nzima ya watu wa Mungu. mtume Paulo anaendelea kufundisha hivi, kwamba kwa Kadiri ile Mungu atakavyotukuza miili yetu ndivyo atakavyofanya kwa ulimwengu mzima, viumbe vyote vitarudi na kushiriki uhuru na utukufu wa Watoto wa Mungu. Tena kwa imani kubwa, Mtume Paulo anaendelea kutufariji kuwa mateso ya sasa si kitu kulinganishwa na utukufu utakaofunuliwa kwetu. Mtume Paulo anatueleza kuwa mateso na mahangaiko ya wakati huu ni ya kitambo kidogo tu na sio mateso yaletayo kifo cha umilele bali ni maandalizi ya mwanzo wa maisha mapya na ya umilele huko mbinguni. Baada ya faraja hiyo ya mwisho wa mateso kwa binadamu, mateso yaliyosababishwa na dhambi ya mwanadamu mwenyewe, Mwenyezi Mungu anatuahidia huruma yake endapo tuta mtumainia yeye na kuvumilia kwa Imani shida na mahangaiko ya hapa duniani.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:1-23). Sehemu hii ya Injili inahusu mfano maarufu wa mpanzi. Ni mfano mashuhuri hasa kwa jamii ya wakulima kwani inatumia lugha wanayoweza kuielewa kwa haraka na wepesi zaidi. Katika somo hili Mwinjili Mathayo anasisitiza kuwa kama vile mbegu iwezavyo kutoa mavuno mengi licha ya mapingamizi na vikwazo vingi, vivyo hivyo Neno wa Mungu aliyefanyika mwili akakaa kwetu, yaani Bwana wetu Yesu Kristo ndivyo anavyotuletea matunda mema na mengi katika maisha yetu licha ya uwepo wa maadui wanaopinga kazi yake. Katika moja ya tafakari zake, Mtakatifu Yohane Christostom anasema kuwa “katika mfano wa mpanzi Yesu anaeleza upendo na huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika kazi na matendo yake katika kumkomboa mwanadamu kutoka katika mahangaiko na utumwa wa dhambi. Yesu anaposema mpanzi alitoka, ni kile kitendo cha Mungu muweza wa yote aliyeko mahali pote kujishusha, kuchukua hali yetu ya kibinadamu katika fumbo la umwilisho akawa mwanadamu na kuja kukaa nasi kwa kuwa sisi hatukuwa na uwezo wa kumwendea yeye aliye mkatatifu kwa sababu ya dhambi zetu.” Tendo la “mpanzi kutoka” kama inavyo simuliwa katika Injili hii ya leo ni ashirio la upendo mkuu wa Mungu anaye shuka kwetu ili kujitambulisha na kujifananisha nasi. Kwa Neno wake, Mungu ananena nasi akituahidia uzima wa milele. Basi nasi tusali ili Neno wa Mungu awe kwetu ni taa yetu, silaha yetu ya mapambano dhidi ya mwovu shetani na nuru katika njia zetu. Kadhalika Injili hii inatupa nafasi pia ya kutafakari huruma na uvumilivu wa Mungu.
Huruma ya Mungu inajidhihirisha katika kujishusha kwake ili kuja kwetu. Lakini ni unyenyekevu pia kwani kwa kupitia unyenyekevu ana vumilia magumu katika kuipanda mbegu ya Neno lake ndani mwetu. Miiba na miamba inayo zuia mbegu pengine kumea vema n ahata zinapomea zikashindwa kuzamisha mizizi hata kwenye kina kirefu cha udongo; ndiyo dunia na Fahari zake ambazo humwondoa mwanadamu katika umakini wa Neno. Ni wajibu wa kila mbatizwa kupenda kulisoma nakulitafakari Neno la Mungu Baba analolipanda kama mbegu katika mioyo yetu bila upendeleo ama ubaguzi. Mbegu ya Neno wa Mungu ni Zawadi kwa kila mmoja wetu. Tufungue sasa mioyo yetu ili liweze kukaa ndani mwetu na kutuletea matunda. Basi tumwombe Mungu atuonyeshe uso wake katika haki kama wimbo wa wetu wa mwanzo siku hii ya leo unavyo imbwa ili tuamkapo tushibishwe kwa sura yake (Zab. 17:15), ambapo Mungu mwenyewe anatuonyesha mwanga wa ukweli wake kama tukiishika imani yetu. Kwa kufanya hivi basi hata pale tunapodanganywa na yule mwovu kwa kulinyakua Neno la Mungu ndani mwetu, Roho Mtakatifu atusaidie kwa mapajai yake kurudi katika njia ya haki. Tunasali leo ili udhia au dhiki ikitokea kwa ajili ya Neno la Mungu tusichukizwe na kuliacha na shughuli za dunia hii na udanganyifu wa mali usitusonge kiasi kwamba tukalisahau Neno la uzima wa milele. Amani ya Kristu iwe daima nanyi. Amina.