Tafuta

Askofu mkuu Nkwande amewahimiza mapadre hao kumfuasa Mungu na kuitii sauti yake ndani mwao katika mazingira ya sasa bila kutegemea kupata mali wala anasa zingine za dunia. Askofu mkuu Nkwande amewahimiza mapadre hao kumfuasa Mungu na kuitii sauti yake ndani mwao katika mazingira ya sasa bila kutegemea kupata mali wala anasa zingine za dunia.  

Wosia wa Askofu Mkuu Renatus Nkwande Kwa Mapadre Wapya!

Askofu mkuu Nkwande amewahimiza mapadre kumfuasa Mungu na kuitii sauti yake ndani yao katika mazingira ya sasa bila kutegemea kupata mali wala anasa za dunia. Amesema kuwa "Mungu amewaita ili washiriki katika kazi yake ya ukombozi kwa uaminifu ambayo kwa gharama kubwa Kristo Yesu aliifia Msalabani na kufedheheshwa.” Pia amewasisitiza kuwa na tamaa ya imani kwa kupenda kuona watu wanamwitikia na kumkubalia Kristo Yesu, huku wakijenga umoja!

Na Mwandishi Maalum, Jimbo kuu la Mwanza, - Mwanza, Tanzania

Kimsingi Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, Jimbo kuu la Mwanza
Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, Jimbo kuu la Mwanza   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Mapadre wameaswa kutimiza vema wajibu wao kwa kuyatoa maisha yao kwa ajili ya huduma ya Kanisa na Ulimwengu mzima kama wachungaji na wafuasi wa Kristo. Katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi watatu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza amewaasa Mapadre wapya kutambua safari ya Daraja Takatifu ya Upadre walioufikia ambao ni safari ya maisha ya sadaka kwao na kwa jamii na kwa ulimwengu mzima. Askofu mkuu Nkwande amewahimiza mapadre hao kumfuasa Mungu na kuitii sauti yake ndani yao katika mazingira ya sasa bila kutegemea kupata mali wala anasa zingine za dunia. Amesema kuwa "Mungu amewaita ili washiriki katika kazi yake ya ukombozi kwa uaminifu ambayo kwa gharama kubwa Kristo Yesu aliifia Msalabani na kufedheheshwa.” Pia amewasisitiza kuwa na tamaa ya imani kwa kupenda kuona watu wanamwitikia na kumkubalia Kristo Yesu, huku wakifanya kazi ya kuungana na waamini wengine kama: Makatekista, waamini walei na umoja wa wakristo yaani katika majadiliano ya kiekumene na waamini Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kuhakikisha kwamba watu wanamfuata Kristo Yesu.

Padre Theogenes Madushi Jimbo kuu la Mwanza
Padre Theogenes Madushi Jimbo kuu la Mwanza

Katika hatua nyingine Askofu mkuu Nkwande amewasisitiza Mapadre kuleta mabadiliko chanya katika jamii ili watu wamwendee, wamwamini na kumuishi Kristo Yesu, ili wawe: watakatifu, wakamilifu, wema, waadilifu na zaidi sana watu wayajali maisha ya wengine ambayo ndio zawadi ya pekee ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu. Aidha Askofu mkuu amesema kuwa mara baada ya miaka yote ya malezi na majiundo ya Mapadre hao wapya, sasa wanapaswa kuwa watu wa neema na baraka katika Kanisa na sio watu wa kufedheheka na manung'uniko na zaidi wawe ni mashuhuda na wapatanishi wazuri katika Kanisa na jamii watakayokuwapo. Amewasihi pia kutimiza wajibu wao kwa kutekeleza huduma Takatifu ya: Kuongoza, kutakatifuza na kufundisha kwa Jina la Kristo mwenyewe aliye mwalimu, na kuwakumbusha waamini wote kuwa maisha ya Upadre sio maisha ya raha bali ni ya sadaka na Msalaba ambapo Mapadre wanapaswa kumtazama zaidi Kristo Yesu na kuwa yote watakayoyapata katika hija ya maisha yao, wayatumie kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kuwashirikisha watu wote Neno la Mungu ambalo nao wanapaswa kulipokea kwa furaha ili watu wote wamjue Mungu, wampende na hatimaye waweze kufika kwake Mbinguni.

Wageni waalikwa waliohudhuria Ibada ya Upadrisho
Wageni waalikwa waliohudhuria Ibada ya Upadrisho

Amewasihi pia waishi katika sheria ya Bwana kwa "kusadiki kile wanachokisoma, na kufundisha kile wanachosadiki na kuishi kile wanachokifundisha" ili mafundisho yao yawe na manufaa kwa watu wote na matendo yao yawe furaha kwa wanaomwamini Kristo Yesu, huku wakizihangaikia roho za watu kwa kuzitembelea familia na jumuiya ili watu wapokee Sakramenti za Kanisa. Mwishoni Askofu mkuu Nkwande amewasisitiza mapadre hao wawe watu wa: Kulitafakari kwa kina Neno la Mungu; Wawe ni watu sala; kwa kusali na kuuombea ulimwengu mzima bila ubaguzi wa imani, kabila taifa na hata itikadi kwa sababu wao wamewekwa wakfu kwa ajili ya: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ikumbukwe kuwa Jimbo Kuu la Mwanza ni moja kati ya majimbo Kuu nchini Tanzania na mbio za kutolewa kwa daraja Takatifu ya Upadre Jimboni hapo ndio zimeanza rasmi katika Parokia ya Kahangala ambapo mashemasi watatu kati ya mashemasi 11 kutoka Parokia tofauti za jirani walipokea daraja Takatifu ya Upadre, wawili wakiwa ni mashemasi wa Jimbo hilo ambao ni Shemasi Theogenes Madushi wa Parokia ya Kahangala na Shamasi Francis Igosha wa Parokia ya Ihimbili na Shemasi Michael Kimario kutoka shirika la Wamisioni wa Afrika, SMA ambae ni mzaliwa wa Parokia ya Magu Jimboni kuu la Mwanza.

Mapadre Jimbo kuu la Mwanza
09 Julai 2026, 16:03