Tafuta

Msalaba ni kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo, alama ya ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waamini. Msalaba ni kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo, alama ya ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waamini.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 22 Mwaka A wa Kanisa: Njia ya Msalaba: Kielelezo Cha Ufuasi

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 22 ya Mwaka A inakazia kuhusu wito wa kujikana, kujitwika Msalaba na kumfuata Yesu Kristo. Ni mwaliko wa kuupenda na kuumkumbatia Msalaba kwa moyo radhi na utayari wa kuianza safari pamoja na Kristo Yesu kuelekea Mlimani Kalvari utakapo simikwa mti wa wokovu kama antifona ya kuabudu Msalaba siku ya Ijumaa Kuu inavyo tuita ikisema “Ecce lignum crucis, in quo salus mundi pependit: venite, adoremus, yaani" Msalaba!

Na Padre Octavian Onesmo Hinju, JUCo, - Morogoro, Tanzania.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 22 ya Mwaka A wa Kanisa, inakazia kuhusu wito wa kujikana, kujitwika Msalaba na kumfuata Yesu Kristo. Ni mwaliko wa kuupenda na kuumkumbatia Msalaba kwa moyo radhi na utayari wa kuianza safari pamoja na Kristo Yesu kuelekea Mlimani Kalvari utakapo simikwa mti wa wokovu kama antifona ya kuabudu Msalaba siku ya Ijumaa Kuu inavyo tuita ikisema “Ecce lignum crucis, in quo salus mundi pependit: venite, adoremus, yaani “Huu ndiyo mti wa msalaba ambao wokovu wa ulimwengu umetundikwa juu yake, njoni tuabudu.” Mababa wa Kanisa hawa ni walimu na wanataalimungu wa kwanza wa kikristu ambao wengi wao waliishi na kufanya utume katika karne za kwanza za ukristu. Tangu zamani Mababa wa Kanisa wamefundisha kuwa msalaba ni kitovu cha wokovu, ushindi dhidi ya Ibilisi, Shetani na tiba ya dhambi ya asili. Ni kwa njia ya msalaba tu yaani fumbo la mateso kifo na baadaye ufufuko wa Kristu ndipo sisi sote tunakombolewa. Mababa wa Kanisa kama vile Mtakatifu Ambrose na Mtakatifu Augustino walifundisha kuwa Msalaba ni “Mti wa pili” unaosahihisha makosa ya mti wa kwanza huko Edeni. Kumbe mti wa Msalaba ambao ni kielelezo cha Adamu Mpya yaani Kristu Yesu mwenyewe ni tiba dhidi ya mti wa Edeni ule ulioleta kifo, mauti na uharibifu kwa mwanadamu. Msalaba ni alama ya umiliki na ulinzi.

Msalaba ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu
Msalaba ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu   (Vatican Media)

Mababa wa Kanisa walieleza kuwa kufanya ishara ya Msalaba au kuishi chini ya Msalaba ni kama kuwekewa mhuri au chapa ya umiliki. Katika ulimwengu wa kale, chapa ilitumiwa kumtambulisha mchungaji kwenye kondoo wake, au askari kwa jenerali wake. Kwa Mababa hawa wa Kanisa, Msalaba humtambulisha Mkristo kuwa ni mali halisi ya Kristo na humpa kinga dhidi ya nguvu za giza. Msalaba ni ushindi dhidi ya shetani. Mababa wa Kanisa wa karne za kwanza kama Mtakatifu Ireneus wa Lyon na Mtakatifu Athanasius walifundisha kuwa Msalaba ulikuwa uwanja wa vita ambapo Kristo Yesu alimshinda Shetani. Kifo cha Yesu Msalabani hakikuwa tu adhabu, bali ni bei iliyolipwa ili kumweka huru mwanadamu aliyekuwa mtumwa wa dhambi na mauti. Msalaba ni nguvu na hekima ya Mungu. Wakifuata mafundisho ya Mtume Paulo katika waraka wake 1Wakorintho 1:18, Mababa wa Kanisa walisisitiza kuwa Msalaba unaonekana upuuzi kwa ulimwengu wa nje, lakini kwa waamini ni nguvu kuu ya Mungu inayobadilisha maisha na kuleta upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu. Kumbe ni katika mtazamo huo ipo maana ya kwanini masomo haya ya siku ya leo yanakazia wito wa kujikana, kujitwika msalaba na kumfuata Yesu Kristo. Ingawa misalaba inaumiza miili na hisia zetu za kibinadamu lakini upo ushindi na tuzo la mbingu katika Kristu Bwana wetu aliyetukomboa kwa njia ya mti huo endapo tutapokea misalaba kwa moyo wa toba, shukrani na imani huku tukishangilia na kusema “Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru, kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.”

Msalaba ni utambulisho wa Mwamini Mkatoliki
Msalaba ni utambulisho wa Mwamini Mkatoliki   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Yeremia (Yer. 20:7-9). Katika somo hili, Yeremia anamtolea Mwenyezi Mungu manung’uniko na uchungu ambao kazi yake ya unabii imemletea. Itakumbukwa kuwa Nabii Yeremia alifanya huduma yake ya kinabii kwa muda wa takribani miaka 40, kuanzia mwaka 627 KK wakati wa utawala wa Mfalme Yosia hadi baada ya kuangamizwa kabisa kwa mji mtakatifu wa Yerusalemu mwaka 587 KK. Nabii Yeremia aliitwa na Mungu akiwa kijana mdogo mnamo mwaka 627 KK, katika mwaka wa 13 wa utawala wa Mfalme mwema Yosia. Aliendelea kutoa unabii wakati wa utawala wa wafalme mbalimbali wa Yuda waliokuja baada ya Yosia, akiwemo Yehoahazi, Yehoyakimu, Yekonia na Sedekia hadi kuanguka kwa mji huo. Baada ya Yerusalemu kuteketezwa na Wababeli mnamo 587 KK, aliendelea kutoa ujumbe kwa mabaki ya watu huko Yuda na hata alipopelekwa Misri. Katika kipindi cha unabii wake taifa la Yuda lilikabiliwa na mambo kadhaa, mosi ni hali ya kiroho na kimaadili; kwamba taifa la Yuda lilikuwa katika hali mbaya ya uasi, kuabudu sanamu, uasherati na dhuluma bila kutubu, licha ya juhudi za awali zilizofanywa na Mfalme Yosia. Jambo la pili lilikuwa ni vitisho na hatari za kisiasa; nchi ilikuwa chini ya tishio kubwa la kijeshi kutoka kwa Milki ya Babeli, ambapo Yeremia alionya wazi kuwa kushindwa kwa Yuda na kuangamizwa kwa Hekalu kulikuwa hakuepukiki na kwamba walipaswa kujisalimisha kwa Babeli. Jambo la tatu lilikuwa ni mateso na upinzani. Kwa kawaida wanadamu hawaupendi ukweli ndio maana hayati Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu Katoliki la Jos huko nchini Nigeria Mhashamu Askofu mkuu Gabriel G. Ganaka alipata kusema “kweli itakuweka huru lakini kwanza itakufanya mnyonge na mwenye huzuni.” Hili ndilo alilolipitia Nabii Yeremia ambaye alitabiri kuwa wayahudi watapata adahabu ya kupelekwa uhamishoni Babeli.

Kujitwika vyema Msalaba wako na kumfuasa Kristo!
Kujitwika vyema Msalaba wako na kumfuasa Kristo!   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Vile Mungu hakutoa adhabu hiyo upesi Wayahudi walimcheka na kumdhihaki sana na kwa sababu ya ujumbe wake wa “adhabu na uharibifu ujao,” Yeremia alichukiwa, alionwa kama msaliti, alipigwa, aliwekwa kizuizini kwenye chumba cha gerezani, na kisha baadae alitupwa kwenye shimo lililojaa matope, jambo lililomfanya ajulikane kama “nabii wa kulia au wa mateso.” Hali hii ilimvunja sana moyo anamwambia Mwenyezi Mungu “umenihadaa nami nikahadaika” yaani umenidanganya nami nikadanganyika. Yeremia anaona amedanganyika kwa sababu ahadi ambazo Mungu alimpa alipomwita kuwa nabii zimegeuka kuwa kinyume. Sasa kila anayemwona anamcheka, neno analotangaza haoni kama linapenya katika maisha ya watu. Na hata yeye badala ya kupokelewa kama mjumbe wa Mungu anaonekana kituko machoni mwao. Pamoja na manung’uniko hayo yote, pamoja na kukata tamaa, Yeremia bado anashangazwa na kitu kimoja. Anapoamua kuiacha kazi ya unabii na kupanga kutokuhubiri tena Neno la Mungu, anashindwa. Hawezi kujinasua kutoka katika utume wa unabii aliokwisha upokea na aliokwisha uanza. Kimwili amekata tamaa lakini bado kwa ndani Neno la Mungu linawaka na linamsukuma aendelee kulitangaza. Yeremia bado alionja nguvu ya wito wake. Kumbe, hapa tujifunze mambo kadhaa; moja ni kwamba katika magumu Mungu hapotei, bado yuko nasi ila ni sisi tu ndio ambao hatumuoni, pili ni kuwa tusiogope kusema na kusimamia ukweli hata kama tutabaki peke yetu kwani jambo la uwongo haliwi kweli hata likisemwa na watu elu kadhalika kweli itasimama hata ikipingwa na ulimwengu mzima. “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru (Yoh. 8:32).” “Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Yn 17:19.”

Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu, kuyafia malimwengu
Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu, kuyafia malimwengu   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 12: 1-2). Katika mpangilio na mtiririko wa waraka huu wa Mtume Paulo kwa Warumi, sura hii ya 12 ambayo tunaisoma siku ya leo inafungua sehemu ya pili ya waraka, sehemu ambayo Paulo Mtume anajielekeza kutoa maonyo na maelekezo mbalimbali kuhusu maisha ya kila siku ya wakristo wa Roma. Leo kama sehemu ya katekesi yake Paulo anawaambia “itoleeni miili yenu kama sadaka hai na takatifu impendezayo Mungu (Rum. 12:1-2).” Na tena anawaonya wasishawishike kuiga mitindo ya watu wa ulimwengu bali wao kama wakristo wazigeuze fikra zao, wamuelekee Mungu ili walitambue na kulitenda lililo jema, lililo kamilifu na lile linalofaa. Pengine, tunaweza kujiuliza ni kipi hasa kilimsukuma Paulo kutoa katekesi hii? Paulo aliwaandikia na kuwapa maonyo haya akitambua fika mazingira ya Roma ya wakati huo. Huu ulikuwa ni mji mkubwa yalipokuwa makao makuu ya dola ya kirumi. Ni mji ulikusanya kila aina ya watu hivi kwamba pamoja na maendeleo uliokuwa nayo, ulijikuta kuwa pia na mmomonyoko mkubwa wa maadili na uchaji. Usia wa Paulo ulilenga kuwatahadharisa wakristo walioishi katika mji huu ili wasipoteze utambulisho wao wa kuwa wakristo na wasimezwe na mitindo ya wakazi wa mji huo. Somo hili linazungumza nasi pia ambao mazingira ya ulimwengu tunaoishi hayatofautiani sana na ya Roma ya wakati wa Mtume Paulo. Mwaliko unaotuangukia ni uleule wa kutunza utambulisho wetu ili tusimezwe na mitindo ya sasa ya ulimwengu.

Kumfuasa Kristo Yesu kuna masharti yake muhimu ya kuzingatiwa
Kumfuasa Kristo Yesu kuna masharti yake muhimu ya kuzingatiwa   (@Vatican Media)

Injili ya Dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo (Mt. 16:21-27).  Tutakumbuka kuwa Dominika iliyopita yaani ile ya 21A Injili (Mt. 16:13-20) ilimwonesha Petro kama shujaa wa imani aliye mkiri Yesu kuwa ndiye Kristo kiasi cha Yesu Kristo mwenyewe kumwita mwamba ambao juu yake atalijenga Kanisa lake, lakini leo anamgeukia na kumwita shetani. Tunasikia katika Injili ya leo Yesu anamwambia “rudi nyuma yangu Shetani maana wewe huyawazi yaliyo ya Mungu bali yaliyo ya wanadamu.” Nadharia na historia karibu katika Israeli yote kulikuwa na mambo makubwa mawili yaliyowatatiza watu kumhusu Yesu. La kwanza lilikuwa ni kuhusu umasiha wa Kristu Yesu kwa kukubali kuwa Yesu ndiye Kristo, yaani Yesu ndiye Masiha yule aliyetabiriwa na ndiye Masiha aliyekuwa akingojewa kwa miaka mingi. La pili, lilikuwa ni kukubali kuwa huyu Yesu ni Masiha atakayeteswa, yaani ataudhihirisha umasiha wake na kuwaokoa watu kwa njia ya mateso. Kwa myahudi ilikuwa haiingii akilini kuchora picha ya masiha mteswa. Ilikuwa ni fedheha na kashfa kubwa. Kama Myahudi, Mtume Petro alipomkiri Yesu kuwa ndiye Kristo alivuka kiunzi cha kwanza. Lakini alishindwa kuvuka kiunzi cha pili cha kukubali kuwa itampasa Yesu kuingia katika mateso hadi kuuwawa na siku ya tatu kufufuka. Yesu anamkaripia kwa kutumia maneno makali hadi kumuita shetani ili kurekebisha kasoro hiyo waliyokuwa nayo watu kumhusu.

Katika kumfuasa Kristo Yesu, Mungu apewe kipaumbele cha kwanza
Katika kumfuasa Kristo Yesu, Mungu apewe kipaumbele cha kwanza   (@Vatican Media)

Ni hapa tunaona kuwa karipio hili la Yesu kumwita Petro Shetani sio lake peke yake. Ni karipio la wote ambao wanamwamini Yesu kuwa ndiye Kristo lakini bado hawataki au hawako tayari kumfuata katika njia ya mateso ya Kristo Yesu huyo wanayemuamini. Katika hili tunauona ukigeugeu wa Petro katika Imani. Hii ni kwetu sote ambao imani yetu kwa Kristu bado haijakua na kukomaa kiasi cha kuzongwa kirahisi, basi tumwombe akuze na kukomaza zawadi hiyo ya imani. Katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu haya yale yenye chuki na madhulumu ya kikristo mfano huko Kaduna, Borno, Plateau, Benue, Zamfara na Katsina nchini Nigeria kushikilia imani kunaweza kufananishwa na kubeba msalaba msalaba mzito sana. Lakini tunayo hakika kuwa ni msalaba utakao tukomboa. Leo Kristu anaposema “Mtu akitaka kunifuata ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake na anifuate” anataka kutuasa tuzishike imani zetu na tuzikiri hata katika nyakati ngumu kwenye maisha. Tutambue kuwa ufuasi ni msalaba, basi tuibebe misalaba yetu kijasiri na tusonge mbele bila hofu na wasiwasi tukiamini kuwa Kristu yuko pembeni yetu katika safari na basi tusali kuomba uthabiti katika kuiishi vema zawadi hiyo ya imani na kamwe tusiwe vigeugeu kama Petro katika kumkiri na kisha kuona shaka. Amina.

Liturujia D 22 Mwaka A
29 Agosti 2026, 10:06