Tafuta

Kauli mbiu ya CSW68:“Kuharakisha mafanikio ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote kwa kushughulikia umaskini na kuimarisha taasisi na kufadhili kwa mtazamo wa kijinsia.” Kauli mbiu ya CSW68:“Kuharakisha mafanikio ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote kwa kushughulikia umaskini na kuimarisha taasisi na kufadhili kwa mtazamo wa kijinsia.”  (AFP or licensors)

CSW68:Wanawake wakijumuishwa kifedha wanaweza kujikwamua!

Waziri wa Jinsia na Uendelezaji wa Familia nchini Rwanda alisema taifa lake linajivunia programu mahsusi za ujumuishaji wanawake kifedha ikiwemo uwekaji akiba.Kwa Uganda:Benki zimeanzisha Programu maalum kwa wanawake; Zimbabwe,wameanzisha hadi Benki za Vijana na Wanawake.Kenya,Wanawake wanatumia majukwaa ya kidijitali kusajili makundi na kukopa fedha.Afrika Kusini,Uviko-19 ulitumbukiza wanawake kwenye umaskini,lakini wakachukua hatua.Hayo yamesikika katika CSW68,jijini New York,Marekani

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ndugu msikilizaji/Msomaji kama tulivyokwisha kuanza kusikiliza juu ya Mkutano wa 68 wa Kamisheni, kwenye kumbi mbalimbali za makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, ulioanza tangu tarehe 11 Machi na  utakunja jamvi lake mnamo tarehe 22 Machi 2024, hata Mawaziri kutoka nchi wanachama wa nchi 193 wa umoja huo wamepata fursa ya kuelezea kile ambacho nchi zao zinafanya ili kutekeleza kauli mbiu ya mkutano huo ambayo ni: “Kuharakisha mafanikio ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote kwa kushughulikia umaskini na kuimarisha taasisi na kufadhili kwa mtazamo wa kijinsia.”

Valentine Uwamariya, Waziri wa Jinsia na Uendelezaji wa Familia nchini RWANDA alisema taifa hilo linajivunia programu mahsusi za ujumuishaji wanawake kifedha ikiwemo uwekaji akiba, vikundi vya ushirika na mafunzo ya ujasiriamali, mambo ambayo yamewezesha ujumuishaji wanawake kifedha kufikia asilimia 92 takribani saw ana kiwango cha wanaume. “Ongezeko la mwelekeo wa wanawake kujitegemea kifedha ni dhahiri kutokana na ongezeko la idadi yao wanaojihusisha na kukopa fedha benki na taasisi za utoaji za kifedha,” alisema Bi. Uwamariya. Akiendelea kueleza aliongeza kuwa kujitegema kifedha kunaimarishwa zaidi kupitia sheria za kuhakikisha wanawake wanamiliki ardhi na mali. Halikadhalika elimu ni kwa wote ni kipaumbele ambapo uandikishaji wasichana kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati(STEM) ni asilimia 46.2, wakati Vyuo vya Ufundi Stadi na Elimu (TVET) ni asilimia 43.2:  “Juhudi za sasa ni kutokomeza mila na desturi potofu hasa mfumo dume na kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye sekta za kiuchumi, kijamii na utawala. Tunaoanisha pia stadi za kiufundi za wanawake na fursa za ajira,” alisema Waziri huyo kutoka Rwanda.

Kwa upande wa UGANDA: Benki zimeanzisha Programu maalum kwa wanawake ambapo Amongi Betty Ongom, Waziri wa Uganda anayehusika na Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii alitaja hatua kadhaa zilizochukuliwa ili kuhamasisha  Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake(GEWE.) Kwa mujibu wake alisema “Kwa kuingia ubia na Benki na Taasisi za Fedha ili zianzishe huduma za kifedha mahsusi kwa wanawake: Benki na taasisi hizo zimeanzisha Programu Maalum kwa Wanawake Wafanyabiashara zenye lengo la kurahisisha wanawake kupata fedha na huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji yao.” Na alitaja benki hizo kuwa ni pamoja na BRAC Uganda Bank Limited, Stanbic Bank/Stanbic for Her na Centenary Bank na mradi wao wa Super Woman. Halikidhalika Uganda imejengea uwezo wa stadi wanawake wajasiriamali ili waongeze thamani kwenye bidhaa zao hasa mazao ya kilimo.

Kwa upande wa nchi ya  ZIMBABWE, walianzisha hadi Benki za Vijana na Wanawake. Waziri wa Masuala ya Wanawake, Jamii, Maendeleo ya Biashara ndogo na za Kati, Monica Mutsvangwa  alibaisha kuwa Zimbabwe imeendelea kujumuisha suala la jinsia inapokuwa inaunda, inaendeleza, inatekeleza, inafuatilia na kutathmini sera, mikakati na mipango yote kuhusu masuala ya kiuchumi, kifedha na utokomezaji umaskini. Mathalani utekelezaji wa mpango wa kwanza na wa sasa wa Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishi wa Kifedha, kwa kiasi kikubwa umeimarisha ujumuishi wa wanawake na fursa za kupata fedha, kama inavyodhihirishwa na huduma ambazo zimeanzishwa kwa ajili ya wanawake, vijana na makundi mengine yaliyo hatarini,” amesema Waziri huyo.  Aidha Bi Monica Mutsvangwa alitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa dawati la wanawake na vitengo karibu katika Benki zote, kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Zimbabwe ya kutoa mikopo, Benki ya Uwezeshaji Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Ingawa hivyo amesema licha ya mafanikio wanatambua kuwa bado safari ni ndefu kuelekea kuimarisha taasisi, utoaji wa fedha unaozingatia jinsia na kutokomeza umaskini miongoni mwa wanawake na wasichana.

Na kwa mwakilishi wa KENYA ambaye alisema kuwa Wanawake wanatumia majukwaa ya kidijitali kusajili makundi na kukopa fedha Taifa hilo la Afrika Mashariki liliwakilishwa na Waziri wake wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi  Bi Aisha Juma Katana ambaye alisema serikali ina sera na mikakati ya kiuchumi na kijamii inayohamasisha kusaka fedha na kufanikisha ujumuishaji wanawake kwenye sekta ya fedha. Miongoni mwake ni Sera ya Taifa kuhusu Jinsia na Maendeleo ya mwaka 2019 na rasimu ya sera ya Taifa kuhusu malezi na uwezeshaji wanawake kiuchumi, ambazo amesema msingi wao ni Katiba ambayo inahamasisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake na wakati huo huo kuhakikisha kuna usawa na hakuna ubaguzi. Bi Juma alitolea mfano wa hatua za kusongesha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kuwa ni Mfuko wa Wanawake wa Ujasiriamali , WEF, ambao amesema umeshatoa jumla ya dola milioni 6.72 kwa makundi 18,955 na kupata kukusanya dola 313,967.16 kama akiba. “Kenya pia imetumia vizuri mbinu za kidijitali kuziba pengo la kidijitali kwenye jinsia kwa kuchagiza mfumo bora jumuishi wa kifedha. Mipango mahsusi juu ya matumizi ya dijitali imewekwa na kuwezesha wanawake wanaotaka kukopa fedha kusajili vikundi vyao, kupata mikopo na kukusanya akiba kupitia majukwaa ya kidijitali. Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wametengewa asilimia 30 ya zabuni za serikali,”  amesema Bi. Juma.

Ndugu msikilizaji, kwa AFRIKA KUSINI, Uviko-19 ulitumbukiza wanawake kwenye umaskini, lakini wakachukua hatua. Hayo yalisemwa na mwakilishi wa Afrika Kusini  Bi Lindiwe Zulu, Waziri wa Maendeleo ya Jamii ambaye kwa hakika alieleza kuwa janga la Uviko-19 lilifichua ukosefu wa usawa, umaskini utokanao na ukosefu wa ajira na njaa kwenye nyumba, ambavyo vilichochea ongezeko la mzigo wa kazi zisizo na ujira na majukumu ya kazi za nyumbani kwa wanawake na wasichana na hatari wanazokumbana nazo kutokana na ukatili wa kijinsia. Akielezea ni nini ambacho serikali ya taifa hilo lililofanya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994 lilifanya alisema kuwa: “ilichukua hatua haraka kwa kupanua wigo wa hifadhi ya jamii, malipo maalum kwa wanawake wanaopatiwa msaada wa malezi ya watoto ili wakabiliane na kukosekana kipato kutokana na Uviko-19, ongezeko la umaskini na ukosefu wa uhakika wa chakula. Serikali pia ilipitisha kanuni ya malipo maalum ya kuleta unafuu kwa watu wasio na ajira, hatua ambayo bado inatekelezwa.”

Baada ya kusikiliza wawakilishi kutoka Tanzania, Kenya, Zimbabwe, Rwanda, Afrika Kusini na Uganda, tutaendelea kuwajuza taratibu, hususani wawakilishi kutoka Afrika, na hata mataifa mengine  nini mataifa mengine hasa wanawake hao wamiwakilisha katika mkutao huu mkubwa wa Kamishna ya Wanawake (CSW) ambao ulianza tarehe 11 Machi na unakunja jamvi lake tarehe 22 Machi 2024.

CSW68, wanawake wakiwezeshwa wanaweza kwa mujibu wa mawaziri wanawake
21 March 2024, 15:27