Tafuta

Mkurugenzi Mtendaji wa Wanawake Umoja wa Mataifa(UN Women)Bi Sima Bahous akisalimiana na Bi Amina J.Mohammed,Kaimu Katibu wa UN huko jijini New York. Mkurugenzi Mtendaji wa Wanawake Umoja wa Mataifa(UN Women)Bi Sima Bahous akisalimiana na Bi Amina J.Mohammed,Kaimu Katibu wa UN huko jijini New York. 

CSW68,Hakimu Achieng:Wasichana ni majaji watarajiwa,fuata ndoto zenu!

Hakimu Pamela Achieng wa Kenya alitoa ujumbe wa kutia moyo kwa wasichana shuleni ili waweze kujiamini na kuingia katika masomo ya uanasheria na hatimaye kuchangia kuongezeka kwa mahakimu au majaji wanawake.Ni katika Mkutano unaondelea wa Kamisheni ya 68 ya kila mwaka ya Hali ya Wanawake (CSW68)huko New York Marekani ulioanza tarehe 11na utamalizika 22 Machi 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kamisheni au Tume ya 68 ya Hali ya Wanawake (CSW68), ambao ni mkutano mkubwa zaidi wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, ulifunguliwa tangu tarehe 11 na utahitimishwa tarehe  22 Machi 2024 huko New York, Marekani, chini ya kaulimbiu: “Kuharakisha mafanikio ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote kwa kushughulikia umaskini na kuimarisha taasisi na kufadhili kwa mtazamo wa kijinsia.” Ulimwengu uko kwenye njia panda muhimu kwa usawa wa kijinsia. Ulimwenguni asilimia 10.3 ya wanawake wanaishi katika umaskini uliokithiri leo, na wao ni maskini zaidi kuliko wanaume. Maendeleo ya kumaliza umaskini yanapaswa kuwa ya haraka mara 26 ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030.

Katika taarifa ya Tume ya Hali ya Wanawake ya Kikao cha sitini na nane wameendelea kujikita na Kipengele cha 3 (a) cha ajenda ya muda kuhusu  Ufuatiliaji wa Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake na kwa kikao maalum cha ishirini na tatu cha Baraza Kuu,iliyoongozwa na mada: “Wanawake 2000: usawa wa kijinsia, maendeleo naamani katika karne ya ishirini na moja”: utekelezaji wa malengo ya kimkakati na hatua katika maeneo muhimu ya wasiwasi na hatua na mipango zaidi katika kuongeza kasi ya mafanikio ya usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wote kwa kukabiliana na umaskini na kuimarisha taasisi na kufadhili na mtazamo wa kijinsia. Kwa njia hiyo katika taarifa ya Katibu Mkuu alibainisha kuwa Maendeleo ya haraka yanahitaji uwekezaji. Takwimu kutoka nchi 48 zinazoendelea zinaoesha kuwa dola bilioni 360 za ziada zinahitajika kwa mwaka ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika malengo muhimu ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kumaliza umaskini na njaa. Katika mwaka 2024 wa maamuzi, watu bilioni 2.6 wanapopiga kura, wana uwezo wa kudai uwekezaji wa juu zaidi katika usawa wa kijinsia.

Suluhisho za kumaliza umaskini wa wanawake zinatambulika kwa upana: kuwekeza katika sera na programu zinazoshughulikia ukosefu wa usawa wa kijinsia na kukuza wakala na uongozi wa wanawake. Uwekezaji kama huo hutoa faida kubwa: Kwa sababu kwanza kabisa zaidi ya wanawake na wasichana milioni 100 wangeweza kuondolewa katika umaskini ikiwa serikali zingeweza kuweka kipaumbele katika elimu na upangaji uzazi, mishahara ya haki na sawa, na kupanua faida za kijamii.  Takriban nafasi za kazi milioni 300 zingeweza kuanzishwa ifikapo 2035 kupitia uwekezaji katika huduma za matunzo. Kuziba mapengo ya kijinsia katika ajira kunaweza kuongeza Pato la Taifa (GDP) kwa kila mtu kwa asilimia 20 katika kanda zote. Katika (CSW68) serikali, mashirika ya kiraia, wataalam na wanaharakati kutoka ulimwenguni kote wameendelea na mkutano ili kukubaliana juu ya hatua na uwekezaji ambao unaweza kumaliza umaskini wa wanawake na kuendeleza usawa wa kijinsia.

Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Majaji Wanawake duniani yalifanyika  kwa mara ya kwanza tarehe 10 Machi 2022, ambao yakiakisi Haki katika Mtazamo wa Kijinsia. Umoja wa Mataifa tangu wakati huo umeendelea kuadhimisha siku hiyo kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kuhakikisha usawa wa kijinsia na kushughulikia masuala ya uadilifu wa mahakama yanayohusiana na jinsia. kwa njia hiyo mkutano ukiendelea jijini New York Marekani, nchini Kenya Selina Jerobon wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kupitia video iliyoandaliwa na washirika wao wa Redio Domus alikutana na Pamela Achieng, Hakimu katika mahakama ya Ngong iliyo katika Kaunti ya Kajiado ambaye alianza kuelezea ni kwa nini kama mwanamke aliamua kuingia katika tasnia hiyo.

Hakimu Pamela Achieng wa Kenya

“Nilivutiwa sana kuingia katika masomo ya sheria kwa sababu babangu mzazi ni Mwanasheria. Pia niligundua kwamba wanasheria wengi ni wanaume na wanawake ni wachache sana, na kwa kufikiria tu hilo likanipatia changamoto chaya kwa sababu niliona kwamba kama mwanaume anaweza kufanya kazi zinazotambulika hasa za kutetea haki za raia katika mahakama kwanini mwanamke asiweze? Na sasa nimejikuta kwamba mimi ni mmoja wa wanawake ambao wamefaulu kuingia katika tasnia ambayo imesalia kuwa na wanaume wengi kwa muda mrefu”  

Swali la mwandishi: Kama Hakimu mwanamke, mnafanya nini kuhakikisha wanawake wote wanapata kujua haki zao na kesi zao kuwasilishwa na kusikilizwa kwa usawa katika mahakama?

Bi Achieng alijibu: “Mosi, mimi ni mwanachama wa chama cha kimataifa cha majaji wanawake inayoungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la wanawake UN Women, na ninajivunia kwamba tulipatiwa siku hii ya Majaji wanawake. Cha pili ni kwamba kesi nyingi za dhuluma kwa wanawake na unyanyasaji kwa upande wa umiliki wa shamba wakati wanafiwa na waume wao, na mara kwa mara tunatilia mkazo mambo hayo na kuenda vijijini kufundisha wanawake na jiamii kuhusu haki zao na kuhamasisha jamii ili ziweze kukomesha ukatili huo au unyanyasaji wa kijinsia. Kama Hakimu kesi zikiletwa mbele ya mahakama kazi zetu ni kuhakikisha kila mtu anapata kusikilizwa kwa haki na kuzingatia usawa wa kijinsia.”

Kwa kuzingatia kwamba tasnia hii imegubikwa na mfumo dume, Pamela alitoa ujumbe wa kutia moyo wasichana shuleni ili waweze kujiamini na kuingia katika masomo ya uanasheria na hatimaye kuchangia kuongezeka kwa mahakimu au majaji wanawake. Bi Achieng alisema:“Kwanza kabisa Jaji Mkuu wakati huu nchini Kenya ni mwanamke.  Huu ni mfano kubwa ambao umeanza kuchochea wasichana shuleni kuona kwamba pia wao wanaweza kama Jaji Mkuu ameweza. Pia kwa sasa Kenya tunao majaji au mahakimu wanawake wengi, kwa hivyo ni mfano Chanya, wasichana wanaweza.”

Hakima Pamela Achieng
20 March 2024, 09:49