Tafuta

Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipomtembelea Papa Francisko mnamo tarehe 12 Februari 2024. Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipomtembelea Papa Francisko mnamo tarehe 12 Februari 2024.  (Vatican Media)

Zanzibar:Serikali yahimiza katika mwezi wa Ramadhani kutenda mema na uvumilivu kidini!

Zanzibar ni nchi yenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini ambapo Uislamu na Ukristo uliiingia mapema kuwa sehemu muhimu ya utamaduni uliodumu kwa karne nyingi.Serikali inawahimiza wananchi kujizuia kwa namna yoyote ile kuingilia uhuru wa mtu binafsi katika kuabudu.Ni taarifa kutoka msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar uliochapishwa tarehe 30 Machi 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Hivi karibuni imeonekana video ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii, mtu mmoja akishambuliwa na kupigwa kwa sababu ya kula chakula huko Zanzibar, kwa siku hizi ambapo Ndugu zetu wanaendelea na mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, suala ambalo kwa wengi limeibua hisia kali ya kitendo hicho hasa ile ya kutokuheshimu na kukiuka misingi mikuu ya uhuru binafsi wa dini. Ni katika muktadha huo ambapo Msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameandika Taarifa kwa vyombo vya habari juu ya “Msimamo wa Serikali ya Zanzibar  kuhusu uvumilivu wa kidini”.

Zanzibar ni Nchi yenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini 

 

Ifuatayo ni taarifa kamili iliyochapishwa tarehe 30 Machi 2024: “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imehimiza katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kutenda mema na kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi. Zanzibar ni nchi yenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini ambapo Uislamu na Ukristo uliiingia mapema kuwa sehemu muhimu ya utamaduni uliodumu kwa karne nyingi. Hii inatufundisha kuhusu ustaarabu wa Wazanzibari kuvumiliana kidini na ndio msingi wa mshikamano miongoni mwetu. Serakali inalaani vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kufanyika sehemu mbalimbali Zanzibar, kadhia hiyo ni kinyume na misingi ya kuvumiliana katika imani za kidini. Aidha, Serikali inawahimiza wananchi kujizuia kwa namna yoyote ile kuingilia uhuru mtu binafsi katika kuabudu. Ikumbukwe Zanzibar inaongozwa kwa Katiba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mamlaka ya kuilinda Katiba ya nchi na watu wake, hivyo hatua yoyote ile yenye kuhatarisha Umoja, Amani na Mshikamano haitavumiliwa. Serikali itaendelea kulinda haki na uhuru wa mtu kuabudu kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Hivyo, tuendelee kudumisha amani na upendo kama mafundisho ya dini zetu yanavyotutaka, tofauti zetu za kidini zisiwe chanzo cha kuvuruga amani, umoja na mshikamano. Taarifa hiyo imesainiwa na "Charles Hilary, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar.”

Kila mtu anastahili kuwa na uhuru na mawazo,wa imani na uchaguzi wa mambo ya dini

Ndugu msomaji wa makala hii, hata hivyo “Kifungu cha  19 cha Katiba ya Zanzibar cha 1984 kinabainisha kuwa “1 Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, wa imani na wa uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa kubadilisha dini au imani yake. (2) Bila ya kuathiri sheria zinazohusika kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa huru na jambo la hiari ya mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za Mamlaka ya nchi. (3) Kila palipotajwa neno “dini” katika kifungu hiki ifahamike kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.”

Hakuna mtu atakayezuiwa kufurahia uhuru wake wa kuchanganyikana

Na katika kifungu kinachofuata cha Katiba kinabainisha kuwa “20.(1) Isipokuwa kwa hiari yake, hakuna mtu atakayezuiwa kufurahia uhuru wake wa kuchanganyika au kujiunga yaani haki yake ya kuchanganyika na kujihusisha atakavyo na watu wengine na hasa kuunda au kuwa mwanachama wa vyama vya wafanyakazi, vyama vya haki za binadamu au vyama vyengine kwa faida yake na ambavyo vimekubaliwa kisheria.”

Kudumisha amani ulimwenguni kote

Hata hivyo ikumbukwe hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan wa Jumhuri ya Muungno wa Tanzania alikutana na Papa Francisko  tarehe 12 Februari 2024 mjini Vatican na katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, waliridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania;  vile vile kuelezea mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafanikio  ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii kwa ujumla pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa. Baadaye, katika mazungumzo na Sekretarieti ya Vatican  walijielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania na pia kujikita katika masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita kwenye kudumisha amani ulimwenguni kote.

Taarifa kwa vyombo vya habari Zanzibar:kuwa na uvumilivu wa kidini
30 March 2024, 14:24