Tafuta

Mzee Cleopa David Msuya amefariki dunia tarehe 7 Mei 2025 Jijini Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwake Usangi, Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro: Ni shujaa wa Tanzania katika huduma kwa umma. Mzee Cleopa David Msuya amefariki dunia tarehe 7 Mei 2025 Jijini Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwake Usangi, Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro: Ni shujaa wa Tanzania katika huduma kwa umma. 

Hayati Cleopa David Msuya: Shujaa wa Tanzania Katika Huduma

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Cleopa Msuya aliyezikwa Mei 13 mwaka huu 2025 ametajwa kuwa ni Kiongozi na Mwanasiasa aliyejipambanua kulitumikia taifa la Tanzania hasa katika kukuza uchumi ambapo alishika nyadhifa hizo katika kipindi kigumu cha uchumi. Hakuwa mtaalam wa masuala ya fedha na uchumi, lakini aliyafahamu mambo haya, ukijitahidi kujifunza jambo kwa bidii utalijua tu!

Na Sarah Pelaji- Vatican

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Cleopa Msuya aliyezikwa Mei 13 mwaka huu 2025 ametajwa kuwa ni Kiongozi na Mwanasiasa aliyejipambanua kulitumikia taifa hasa katika kukuza uchumi ambapo alishika nyadhifa hizo katika kipindi kigumu cha uchumi. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hasan aliyeshiriki maziko hayo yaliyofanyika Usangi Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro ameeleza kuwa, Tangu tarehe 7 Mei alipofariki Msuya hadi siku ya maziko yake, mengi yamekuwa yakisemwa juu yake hasa na wale walioishi nao na kufanya kazi pamoja naye. Amewapa pole wanafamilia, wananchi wa Mwanga na viongozi wote wa serikali kwa kuondokewa na Baba, Kiongozi na shujaa wa Tanzania. “Yote yasemwayo nimeyasikia vizuri nami ninasema kuwa mzee wetu atakumbukwa vizuri kwa kuwahudumia watanzania tangu mwaka 1956 alipoajiriwa hadi 2000 alipostaafu siasa na utumishi wa umma. Wakati wote huo hakuwahi kuwa na faragha ya maisha yake binafsi bali maisha ya kutumikia Watanzania.

Hayati Mzee Cleopa David Msuya alijipambanua kwa huduma
Hayati Mzee Cleopa David Msuya alijipambanua kwa huduma

Aliweka rekodi mbili ya kuwa Waziri wa Fedha kwa kipindi kirefu zaidi kwa vipindi tofauti na nyakati ngumu yaani mwaka 1972 -1975, mwaka 1983-1985 na mwaka 1985-1990. Pili licha ya kushika nafsi kubwa za juu kwa pamoja yaani Makamu wa Rais na wakati huo huo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania japo kwa muda mfupi wa miezi 11 lakini yeye ndiye mtanzania wa Mwisho kushika nafasi hiyo kwani Tanzania iliingia katika mfumo wa vyama vingi ambapo Makamu wa Rais walipatikana kupitia Mgombea Mwenza,” amesema Rais Samia. Katika mengi atakayokumbukwa ni pamoja na kutafuta fedha kuunga mkono harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.  Akiwa Katibu Mkuu wa Fedha alikuwa na wajibu wa kutenga bajeti kwaajili ya kusaidia harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika. Alikuwa miongoni wa viongozi walioenda China kutafuta fedha kutekeleza mradi mkubwa wa Reli ya Tazara uliosaidia harakati za ukombozi na ambao umeendelea kutunufaisha kiuchumi hadi sasa.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akiomboleza kifo cha Mzee Msuya
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akiomboleza kifo cha Mzee Msuya

Rais Samia ameeleza jinsi Mzee Msuya alivyoshiriki harakati za mapinduzi ya mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi ili kuruhu uchumi wa soko na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi. Kilikuwa kipindi kigumu cha kukabiliana na upinzani na shinikizo kutoka kwa wafadhili wa kimataifa wanasiasa nchini, wafanya biashara wazawa na wasioa wazawa wengine wakiyaunga mkono na wengine wakiyapinga kwasababu tofauti tofauti. “Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Msuya kwa Taifa nzima. Tulimpenda mzalendo huyu na mwanahalisi wa Tanzania. Tulimpenda sana lakini Mungu amempenda zaidi. Tukumbuke maneno kutoka Maandiko Matakatifu katika Kitabu cha 1 Wathesalonike 5:16-22 inayotutaka kuwa na shukrani kwa Mungu katika kila jambo maana hayo ni mapenzi ya Mungu katika kwenu Kristo Yesu. Ninatoa pole kwa wanamwanga na watanzania wote kwa ujumla kwa kuondokewa na mpendwa wao. Amekuwa mtetezi mzuri wa maendeleo ya mwanga mpaka mkampa heshima ya Baba wa Mwanga,” Rais Samia amesema.

Askofu mkuu Alex Malasusa akiongoza Ibada ya Mazishi ya Mzee Msuya
Askofu mkuu Alex Malasusa akiongoza Ibada ya Mazishi ya Mzee Msuya

Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete amesema aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya hakuwa binadamu wa kawaida kwani alikuwa Waziri mvumilivu, mbunifu, mchapa kazi aliyejitoa kulitumikia taifa kwa uzalendo mkubwa. Amesema jambo ambalo kamwe hatalisahau kutoka kwa Hayati Mzee Msuya ni tukio lililotokea tarehe 13 Machi mwaka 1990 ambapo Rais Mwinyi alivunja Baraza la Mawaziri. Yeye pamoja na mawaziri wenzake wakakosa usafiri wa kurudi ofisini. “Tulipotoka nje hakukuwa na magari na kwa sababu pale tulikuwa tumeshasimamishwa unaogopa hata kuingia ofisi yoyote kupiga simu ikabidi tutembee kwa miguu kutoka Ikulu mpaka barabarani kutafuta magari ya kutupeleka ofisini kwetu. “Nashukuru wakati ule mitandao ilikuwa bado vinginevyo ingekuwa picha nzuri sana… hadi leo picha zingekuwa zinarejewa. Bahati nzuri Ofisi ya Mzee Msuya ilikuwa karibu pale na Ikulu (Wizara ya Fedha), basi tukatembea mpaka ofisini kwake akatupa magari ya kuturudisha ofisini,” alieleza. Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Sokoine (Edward) alipougua na kwenda kwa matibabu. Aliporudi Mwalimu (Julius Nyerere, Rais wa Kwanza) akamwambia ampishe na yeye (Msuya) akarudi kuwa waziri wa kawaida, Waziri wa Fedha. Hii ilikuwa inataka moyo, ni jambo la kujifunza… huyu mzee ni mtu wa aina yake,” alisema Kikwete. Alisema, amejifunza mengi kutoka kwa Msuya kwani alikuwa baba na mwalimu wake aliyemsaidia mambo mengi kwenye safari yake ya uongozi, ikiwamo kumwelekeza namna ya kwenda kuzungumza na wafadhili Paris, Ufaransa warudi kuifadhili Tanzania mwaka 1994 alipoteuliwa Waziri wa Fedha chini ya Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi.

Baadhi ya viongozi walioshiriki kwenye mazishi ya Mzee Msuya
Baadhi ya viongozi walioshiriki kwenye mazishi ya Mzee Msuya

Alimsifu, Mzee Cleopa David Msuya kuwa alikuwa kiongozi aliyejaliwa kuwa na akili kubwa, mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza na kulifafanua jambo gumu na kulifanya lieleweke na kuwa rahisi hata kwa mtu ambaye siyo mtaalamu wa uchumi.  Hakuwa mtaalamu wa uchumi na fedha kwa kusomea, lakini aliyafahamu mambo ya uchumi na fedha vizuri sana na ndiyo maana amewahi kuteuliwa Waziri wa Fedha mara mbili wakati wa Nyerere na mara moja wakati wa Mwinyi. Lakini aliyafahamu vizuri sana mambo ya uchumi na fedha kama mchumi mbobezi. Hiyo ilitokana na namna alivyojipambanua na kuwa na nia. Hilo ndilo la kujifunza kutoka kwake kwamba ukijitahidi kujifunza jambo utajua” alisema Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika Awamu ya Pili chini ya Rais Mwinyi. Amesema Msuya alipokuwa Waziri wa Fedha alisimamia vizuri uchumi wa nchi katika vipindi vigumu ambapo kwanza nchi ilikumbwa na uhaba mkubwa wa bidhaa madukani, uhaba wa fedha za kigeni, sababu uchumi ulikuwa umedumaa ukaenda hasi (negative). Pia kulikuwa na changamoto upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji, barabara. Msuya kama Waziri wa Fedha alikuwa na juhudi na uwezo mkubwa za kuzuia mambo yasiharibike zaidi wakati wa mtikisiko wa uchumi Kitaifa.

Mchango wa Msuya
14 Mei 2025, 17:39