Tafuta

Juma la Mkutano wa Baraza Kuu la  80 la Umoja wa Mataifa(UNGA80) 23-30 Septemba 2025 huko New York Marekani. Juma la Mkutano wa Baraza Kuu la 80 la Umoja wa Mataifa(UNGA80) 23-30 Septemba 2025 huko New York Marekani.  (ANSA)

Baraza Kuu(UNGA80):"Bora Pamoja:Miaka 80 na Zaidi kwa Amani,Maendeleo na Haki za Binadamu"

Jukwaa limewekwa tayari kwa ajili ya Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,kuanzia tarehe 23–30 Septemba 2025.Mkutano huu unaongozwa na kaulimbiu:“Bora Pamoja:Miaka 80 na Zaidi kwa Amani,Maendeleo na Haki za Binadamu,”ikiwa ni hatua muhimu inayofanyika katikati ya changamoto kubwa duniani na wito wa dharura wa kuchukua hatua mpya za ushirikiano wa kimataifa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Hatimaye, tuko katika Juma la Mkutano wa Baraza Kuu la  80 la Umoja wa Mataifa kwa kifupi UNGA80. Kwa mujibu wa taarifa ya wandaaji wa Umoja wa Mataifa limebainisha kwamba “Mjadala wa Ngazi ya Juu unaanza rasmi tarehe 22 Septemba 2025 kwa siku nzima ya mikutano ya kilele na maadhimisho, ikiwemo kumbukumbu ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, tukio la wakati wa Malengo ya Maendeleo Endelevu au SDG Moment na kutimia miaka 30 tangu Mkutano wa Dunia wa Beijing kuhusu wanawake. Viongozi pia watashiriki kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Suluhisho la amani kwa suala la Palestina na utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili.”

Kwa njia hiyo kuanzia tarehe 23 hadi 29 Septemba 2025, macho na masikio ya dunia yatageukia jukwaa maarufu lenye marumaru ya kijani ndani ya Ukumbi wa Baraza Kuu, ambapo marais, mawaziri wakuu na wafalme watawasilisha taarifa za kitaifa, wakibainisha dira zao kuhusu amani, maendeleo, haki za binadamu na hatua za pamoja wakati huu wa changamoto zinazoongezeka duniani. Ajenda pia itahusisha mkutano wa kilele unaofanyika kila baada ya miaka miwili kuhusu ufadhili wa maendeleo endelevu, Mkutano wa Tabianchi, uzinduzi wa Mazungumzo ya kimataifa kuhusu Usimamizi wa Akili Unde(AI,) Hatua za dunia kuhusu magonjwa yasiyoambukiza NDCs na afya ya akili, pamoja na hali ya Waislamu Warohingya na wengine walio wachache nchini Myanmar.

Ripoti yao ya mwaka 2025, ya tathimini ya masuala ya kijinsia Gender Snapshot

Katika miongo mitatu tangu Azimio la Beijing kuhusu haki za wanawake lilipopitishwa na mataifa ya dunia huko China, hatua kubwa zimepigwa lakini wanawake na wasichana bado wanakabiliwa na viwango visivyokubalika vya ukatili na ubaguzi. Katika siku za kuelekea kumbukumbu ya Jumatatu 22 Septemba 2025, UN Women, shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake inalosimamia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, na Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (DESA) walitoa tahadhari, kuwa hakuna lengo lolote la usawa wa kijinsia lililo katika mstari wa utekelezaji.

Ripoti yenye kichwa Gender Snapshot

Ripoti yao ya mwaka 2025, ya tathimini ya masuala ya kijinsia Gender Snapshot, inaonya kuwa asilimia 10 ya wanawake wanaishi katika umasikini uliokithiri na kwamba wanawake na wasichana milioni 351 bado wanaweza kubaki humo kwenye umasikini kufikia mwaka 2030. Kwa maelezo zaidi bonyeza hapa: https://www.unwomen.org/en/resources/gender-snapshot?gad_source=1

Milioni 708 wametengwa kutoka katika soko la ajira

Takribani wanawake milioni 708 wametengwa kutoka katika soko la ajira kwa sababu ya kazi za malezi zisizolipwa. Hata wale wanaofanya kazi wanasukumwa kwenye ajira za malipo duni. Wanawake wanatengwa katika umiliki wa ardhi, huduma za kifedha, na kazi zenye staha na wananyimwa zana muhimu za kustawi linasema shirika la UN Women. Na, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unaendelea, mmoja kati ya wanawake watatu wanakumbana na ukatili wa kimwili au wa kingono katika maisha yake. Aidha, wanawake milioni 676 wanaishi ndani ya kilomita 50 kutoka eneo la migogoro ikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu miaka ya 1990. Katika baadhi ya nchi, mafanikio yaliyopatikana kwa tabu yanatishiwa na upinzani usio wa kawaida dhidi ya haki za wanawake na kupungua kwa fursa za kiraia. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka hatua kubwa iliyowekwa na Mkutano wa Nne wa Dunia kuhusu Wanawake uliofanyika Beijing mwaka 1995, na kwa nini unachukuliwa kuwa moja ya nyakati muhimu zaidi katika kusongesha usawa wa kijinsia. Tukio hilo lilipelekea kupitishwa kwa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji, mpango ulio na hatua mahsusi katika maeneo muhimu kama vile umasikini, elimu, ukatili, wanawake katika migogoro ya kivita, na ushiriki wa madaraka.

Katika Ulinzi wa Amani, wanawake ni washiriki

Serikali kutoka nchi 189 zilitangaza kwa kauli moja kwamba usawa kati ya wanawake na wanaume ni suala la haki za binadamu na sharti la kufanikisha haki za kijamii, pamoja na sharti muhimu la maendeleo na amani. Leo, kuna ulinzi zaidi wa kisheria kwa wanawake na wasichana duniani kote, sheria 1,583 zinazoshughulikia ukatili wa kijinsia zimetungwa katika nchi 193, ikilinganishwa na nchi 12 pekee mwaka 1995. Zaidi ya nchi 100 pia zimefunza polisi kusaidia waathirika wa ukatili. Katika sehemu za kazi, sheria zinazopiga marufuku ubaguzi wa kijinsia zimeenea, na kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake. Huduma mpya zimeibuka kupunguza mzigo wa kazi za malezi zisizolipwa, na pengo la kijinsia limekuwa likifunzwa katika ngazi zote za elimu. Katika ujenzi wa amani, sasa kuna mipango ya kitaifa 112 kuhusu wanawake, amani na usalama duniani kote, ikilinganishwa na mipango 19 pekee mwaka 2010. Katika hafla ya ngazi ya juu Septemba 22, wawakilishi wa Nchi Wanachama, mashirika ya kiraia, taasisi za kitaaluma, na sekta binafsi watajadili jinsi ya kuharakisha utekelezaji wa Azimio la Beijing na kutafuta rasilimali za utekelezaji.

Kuwekeza kwa wanawake kuna maana ya kuwekeza katika jamii nzima

Kwa UN Women, kuwekeza kwa wanawake kunamaanisha kuwekeza katika jamii nzima, iwapo serikali zitachukua hatua mara moja, umasikini uliokithiri miongoni mwa wanawake unaweza kupunguzwa kutoka asilimia 9.2 hadi asilimia 2.7 kufikia mwaka 2050, hatua ambayo ingeongeza uchumi wa dunia kwa thamani ya dola trilioni 342 kufikia mwaka huo. Hata hivyo, wito wa kuongeza rasilimali kufanikisha usawa unakuja wakati ambapo nchi nyingi zinapunguza ufadhili kwa mipango hii na ukusanyaji wa takwimu. Ni nusu pekee ya wizara za wanawake na taasisi za usawa wa kijinsia zenye rasilimali za kutosha. Kwa Sarah Hendriks wa UN Women, hili ni suala la utashi wa kisiasa, huku mifumo ikiweka kipaumbele vita badala ya haki na usawa. “Tunaishi sasa katika dunia inayotumia dola trilioni 2.7 kila mwaka kwa silaha na bado inashindwa kufikia dola bilioni 320 zinazohitajika kusongesha na kufanikisha usawa wa kijinsia na haki za wanawake,” amesisitiza.

Mwisho wa Juma uchaguzi wa Katibu Mkuu wa UN kuanzia 2027

Mkutano wa ngazi ya juu utaongozwa na Annalena Baerbock, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tangu mapema Septemba na mwanamke wa tano pekee kushika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa Umoja huo miaka 80 iliyopita. Mwisho wa Juma la  Mjadala Mkuu Baerbock ataongoza pia uchaguzi wa mtu atakayekalia nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2027: licha ya shinikizo endelevu na linaloongezeka kutoka pande mbalimbali, ambapo hajawahi kuwa mwanamke katika nafasi hiyo. Duniani kote, wanawake bado wametengwa katika madaraka na maamuzi, wanashikilia chini ya asilimia 27 ya viti vya bunge na asilimia 30 ya nafasi za uongozi. Nchi 113 hazijawahi kuwa na Kiongozi wa nchi mwanamke. Ikiwa kasi ya maendeleo haitabadilika, usawa wa kijinsia katika uongozi utachukua karne moja kufanikishwa.

22 Septemba 2025, 10:50