Hali ya Rohingya nchini Myanmar,ni hali za kibinadamu ni tete!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kiini cha “dharura hii ni Waislamu wa Rohingya, waliokataliwa uraia wa Myanmar”, kufukuzwa makwao na kulazimishwa kuishi kambini au uhamishoni, kilikuwa ndicho kilifungua Mkutano wa ngazi za juu za Umoja wa Mataifa, ambapo Rais wa Baraza Kuu hilo Bi Annalena Baerbockta , Jumanne tarehe 30 Septemba alijikita kuonesha athari za kuzidi kwa mgogoro wa Myanmar unaotishia kuyumbisha eneo zima. Zaidi ya milioni moja sasa wanaishi kama wakimbizi nchini Bangladesh, huku wengine wengi wakiwa bado wamepoteza makazi au wamekwama pamoja na wachache wengine ndani ya Myanmar chini ya hali ambazo viongozi wa Umoja wa Mataifa wamezieleza kama “mbaya” na “zisizo endelevu.”
Katika Mkutano huo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York umewaleta pamoja maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa, wakuu wa nchi na serikali, kwa lengo la kuhamasisha hatua sambamba na wanaharakati wa Rohingya. Taarifa na ripoti ziliweka wazi hali halisi ya maisha tangu mapinduzi ya kijeshi ya Februari 2021: uandikishaji wa kulazimishwa jeshini, ukatili wa kingono, mashambulizi ya anga, njaa na uhamishaji mkubwa. Mashirika ya kibinadamu yalionya kuwa rasilimali zinaisha, na kuacha wakimbizi wakiwa na utapiamlo na kuwalazimisha wengine kujaribu safari za baharini zenye hatari kubwa. Hali ndani ya jimbo la Rakhine – makazi ya asili ya Rohingya – zilielezwa kuwa mbaya zaidi kwa miongo kadhaa, raia wakiwekwa katikati ya mapigano kati ya jeshi la utawala na makundi ya waasi wa kikabila.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kupitia taarifa iliyosomwa na Agisa Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Courtenay Rattray, alisema mgogoro huu umekanyaga haki za binadamu, heshima na usalama wa mamilioni ya watu na unatishia uthabiti wa kikanda.” Alisisitiza hatua tatu za haraka: kulinda raia kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, na kufufua uwekezaji ili kupunguza mzigo kwa wakimbizi na jamii zinazowapokea. “Suluhisho ya mgogoro huu iko hatimaye ndani ya Myanmar,” ujumbe ulisisitiza, ukitaka kukomeshwa kwa mateso na kutambua kwamba “Rohingya ni raia kamili wa Myanmar.”
Rais wa Baraza Kuu Bi. Baerbock alisisitiza ukubwa wa mateso. “Zaidi ya watu milioni tano wa Rohingya wanaume, wanawake na watoto wanashiriki simulizi hii kwa namna moja au nyingine,” alisema, akibainisha kuwa watoto 800,000 bado hawako shule katika kambi ya Cox’s Bazar, Bangladesh pekee. Ufadhili wa kibinadamu ni mdogo mno, huku mpango wa mwitikio wa 2025 ukiwa umefadhiliwa kwa asilimia 12 pekee. “Hili linatupasa kutuonea aibu,” alitangaza, huku akizihimiza nchi kuongeza misaada na kufuatilia suluhisho la kisiasa litakalowezesha kurejea kwa hiari, salama na kwa kudumu.
Kwa wanaharakati wa Rohingya, ndani ya mkutano huu haukuwa tena wa uhamasishaji tu bali ni dai la haki. Wai Wai Nu, mwanzilishi wa Mtandao wa Amani wa Wanawake wa Myanmar, aliwaambia wajumbe kuwa ukatili haukukoma mwaka 2017, wakati zaidi ya watu 750,000 wa Rohingya walipokimbia ghasia zilizotajwa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo, Zeid Ra’ad Al Hussein, kuwa “mfano halisi wa usafishaji wa kikabila.” “Umeendelea kuwa mbaya zaidi,” amesema, akieleza mauaji, uandikishaji wa kulazimishwa jeshini, ukatili wa kingono na njaa vinavyosababishwa na jeshi la Myanmar pamoja na makundi ya waasi wa kikabila. “Bila hatua, wimbi la wakimbizi wa Rohingya litaendelea hadi pale ambapo hakutabakia tena Mrohingya ndani ya Myanmar,” alionya, akihimiza kuanzishwa kwa njia za kibinadamu za kuvukia mipaka, vikwazo mahsusi na mashtaka kwa makosa ya kikatili.
Rofik Husson, mwanzilishi wa Mtandao wa Amani wa Vijana wa Arakan, alitoa ushuhuda wake wa uhamisho na ghasia, akikumbuka jinsi utawala wa kijeshi ulivyowalazimisha wanaume na wavulana wa Rohingya kuingia jeshini, mara nyingi kama ngao za binadamu. Katika wiki moja pekee, alisema, angalau watu 400 waliuawa. Alieleza kuchomwa kwa vijiji na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, ikiwa ni pamoja na mauaji ya mwezi Mei 2024 yaliyowahamisha watu 200,000 kwa siku moja. “Kumaliza mgogoro wa ukosefu wa usalama wa jamii ya Rohingya ni mtihani kwa Baraza hili na mtihani kwa utu wenyewe,” amewaambia wajumbe, akitaka eneo salama chini ya usimamizi wa kimataifa kaskazini mwa Rakhine.
Kwa mtazamo mpana zaidi, Mjumbe Maalum Julie Bishop alisisitiza kuwa mgogoro wa pande nyingi wa Myanmar hauwezi kutenganishwa na machafuko ya kisiasa yaliyochochewa na mapinduzi ya mwaka 2021. Bila makubaliano ya kusitisha mapigano na mapigano yakienea, alionya kuwa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka huu utazidisha ghasia badala ya kuleta uhalali. “Hakuna njia ya makubaliano kuelekea amani,” amesema, akionya kuwa lawama za kimataifa dhidi ya utawala wa kijeshi zimepungua hata ingawa ukiukwaji unaendelea.
Licha ya simulizi za kutisha, wazungumzaji walisisitiza kwamba suluhisho bado zinawezekana ikiwa uamuzi wa kisiasa utapatikana. Bi. Baerbock amehitimisha hotuba yake kwa kusema: “Watu wa Rohingya wamevumilia miaka minane ya taabu, uhamisho na hali ya kutokuwa na uhakika. Ustahimilivu wao ni wa kipekee. Mwitikio wetu lazima ulingane nao.” Kwa wanaharakati wa Rohingya, ujumbe ulikuwa wazi vilevile: matamko pekee hayatoshi tena. “Haki si jambo la hiari… Ndiyo kizuizi pekee, ndiyo njia pekee ya amani,” amesema Bi. Nu.