Tafuta

Maandamano ya vijana wakati wa uchaguzi nchini Tanzania umesababisha majeruhi na vifo. Maandamano ya vijana wakati wa uchaguzi nchini Tanzania umesababisha majeruhi na vifo. 

UN,Guterres,aonesha wasiwasi kufuatia vurugu,vifo na vizuizi nchini Tanzania

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa UN,mjini New York tarehe 31 Oktoba 2025,Katibu Mkuu alilaani vikali vifo na majeruhi nchini Tanzania kufutia na maandamano yaliyoibuka tangu Oktoba 29 na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika.Katibu alielezea "umuhimu mkubwa wa kulinda haki za msingi,hasa haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza,ikiwemo upatikanaji wa taarifa.”

Habari kutoka Umoja wa Mataifa(UN).

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres, alielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali nchini Tanzania kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, na  ripoti za vifo na majeruhi wakati wa maandamano. Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Stephanie Dujarric, mjini New York tarehe 31 Oktoba 2025, Katibu Mkuu alilaani vikali vifo hivyo na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika.

“Katibu Mkuu anasisitiza umuhimu mkubwa wa kulinda haki za msingi, hasa haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza, ikiwemo upatikanaji wa taarifa,” taarifa hiyo imesema.  “Anatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi kamili na usio na upendeleo kuhusu madai yote ya matumizi ya nguvu kupita kiasi.” Aidha, Katibu Mkuu alisema amesikitishwa sana na taarifa za watu waliotoweshwa na wale waliokamatwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huo.  Aliitaka serikali ya Tanzania kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa kwa wote walioko kizuizini, kuhakikisha usalama wao, na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.

Bwana Guterres pia aliwataka wadau wote nchini Tanzania kuwa na subira, kukataa vurugu, na kushiriki katika mazungumzo jumuishi na ya kujenga ili kushughulikia malalamiko na kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama. “Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi zote zinazolenga kukuza mazungumzo, kuimarisha utawala wa kidemokrasia, na kuendeleza amani endelevu nchini Tanzania,” taarifa hiyo imehitimisha.

Kauli ya ofisi ya UN ya Haki za binadamu kufuatia vurugu nchini Tanzania baada ya uchaguzi mkuu

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu imeeleza wasiwasi mkubwa kufuatia vifo na majeruhi vilivyotokea katika maandamano yanayohusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba. Msemaji wa OHCHR, Seif Magango, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswiss kwa njia ya video kutokea Nairobi, nchini Kenya alisema ofisi hiyo imepokea taarifa za kuaminika zikionesha kuwa watu wasiopungua 10 wameuawa katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Morogoro, kufuatia hatua za vyombo vya usalama kutumia risasi na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Magango alisema kuwa marufuku ya kutotoka nje iliwekwa  nchini kote, huku mtandao wa intaneti ukiwa umepunguzwa kwa kiwango kikubwa tangu kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, bila sababu rasmi kutolewa na mamlaka.“ Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi au yasiyo ya lazima, ikiwemo silaha za moto, dhidi ya waandamanaji, na badala yake kufanya kila juhudi kupunguza mvutano uliopo. Waandamanaji nao wanapaswa kuonyesha nia ya amani katika maandamano yao,” amesema Magango.

OHCHR imeitaka Serikali kuzingatia sheria za Kimataifa za Haki za binadamu

OHCHR pia imeitaka serikali ya Tanzania kuzingatia wajibu wake chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kurejesha huduma ya intaneti mara moja na kuhakikisha wananchi wanatimiza haki zao za uhuru wa kujieleza, kushirikiana na kukusanyika kwa amani. “Kukandamiza mawasiliano kutazidisha kukosekana kwa imani ya umma katika mchakato wa uchaguzi,” ameongeza msemaji huyo. Magango amebainisha kuwa vurugu hizo za baada ya uchaguzi zinakuja baada ya kampeni zilizogubikwa na madai ya kukamatwa kiholela kwa viongozi wa upinzani, wakiwemo mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, na naibu wake, pamoja na taarifa za watu kutoweka kwa lazima, akiwemo balozi wa zamani wa Tanzania nchini Cuba.

OHCHR imesisitiza kwamba watu wote waliokamatwa kiholela wanapaswa kuachiliwa mara moja bila masharti, na wale wanaoshikiliwa kwa mujibu wa sheria wapewe haki kamili za mchakato wa haki na kesi ya haki. Zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa mamlaka nchini kuhakikisha uchunguzi wa haraka, huru na wa kina unafanyika kuhusu visa vyote vya vurugu vinavyohusiana na uchaguzi, na kwamba wote waliohusika na ukiukwaji wa haki wanachukuliwa hatua za kisheria.

01 Novemba 2025, 10:28