Tafuta

Mwakilishi wa Jimbo Kuu la Mwanza akipokea Tuzo kwa niaba ya Kituo cha Makumbusho ya Kisukuma Bujora 2025. Mwakilishi wa Jimbo Kuu la Mwanza akipokea Tuzo kwa niaba ya Kituo cha Makumbusho ya Kisukuma Bujora 2025. 

Tanzania:Makumbusho ya Kisukuma Bujora,Mwanza yatwaa Tuzo!

Kituo cha Makumbusho ya Kisuma Bujora kinachoongozwa na Jimbo Kuu la Mwanza,Tanzania kimeshinda tuzo ya "Kituo Bora cha Utalii"katika Shindano la“Tuzo za Serengeti,"tarehe 31 Januari 2026.Makumbusho ya Kisukuma Bujora yalianzishwa rasmi mwaka 1968 katika kijiji cha Kisesa,Mwanza na mmisionari Mkanada Padre David Clement ikiwa ni namna ya kuwavuta watu katika imani kwa njia ya utamadunisho.

Na Pd.Barnabas Ntulugu Mathias – Jimbo Kuu, Mwanza-Tanzania.

Makumbusho ya Kisukuma Bujora ambayo yako chini ya Jimbo Kuu la Mwanza nchini Tanzania yaliyoanzishwa ili kuhifadhi na kukuza utamaduni wa Wasukuma tarehe 31 Januari 2026 yameshinda tuzo ya "Kituo Bora cha Utalii Kitaifa" kwa upande wa vituo,  katika Shindano la “Serengeti Awards, ” Tuzo za Serengeti. Shindano hilo limeanza kwa mara ya kwanza likiwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mgeni rasmi katika Tuzo hizo alikuwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dk. Mwigulu Nchemba.  Sambamba na tuzo hiyo, Tamasha la Ekaristi la Bulabo, ambalo pia limekuwa likiandaliwa na Parokia ya Bujora na Makumbusho ya Bujora liliingia katika kupigiwa kura kama moja ya matamasha bora nchini Tanzania.

Tuzo ya Kituo cha Bujora, Mwanza nchini Tanzania
Tuzo ya Kituo cha Bujora, Mwanza nchini Tanzania

Historia

Jimbo Kuu la Mwanza katika historia yake ya imani, iliinjilishwa  na Wamisionari wa Afrika (White Fathers). Kwa mara ya kwanza, Wamisionari hawa walifika Mwanza kunako tarehe 23 Desemba 1878 katika kijiji kimoja kinachoitwa Malya (Parokia ya Malya kwa sasa na kituo cha hija). Walishangaa kusikia jina hilo kwa sababu lilifanana na Maria hata wakasema, watu hawa wana imani sana mpaka jina la kijiji limepewa kwa heshima ya Bikira Maria bila kujua kuwa kwa Wasukuma Malya maana yake ni kula/ulaji. Sababu kubwa ilikuwa ni kupumzika kutokana na uchovu wa safari pia ikiwa ni maandalizi ya adhimisho la Noeli ambapo walisali mkesha na siku yenyewe ya sherehe. Hii ikaweka alama isiyofutika kwamba kwa mara ya kwanza Misa iliadhimishwa katika Kanda ya Ziwa na viunga vyake.

Tamaduni za  kisukuma nchini Tanzania na imani

Picha ikionesha yaliyomo katika kituo hicho

Tamaduni za kisukuma nchini Tanzania na imani 

Baada ya hapo waliendelea na safari mpaka eneo la Kageye(Magu) ambapo kulikuwa na Bandari ndogo ya kuvusha watumwa. Hapo wamisionari walikuwa wakitafuta njia kuelekea Uganda na walifanikiwa kufika huko kunako tarehe 17 Februari 1879. Madhulumu ya Kabaka na changamoto zingine ziliwafanya wafikirie tena kurudi Mwanza. Safari yao, ilikamilika kunako mwaka 1883 walipotulia rasmi katika eneo la Bukumbi (Parokia na kituo cha hija kwa sasa). Bukumbi ikawa Makao makuu (Kanisa kuu) la Vikarieti ya Nyanza ikibeba maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Musoma, Kagera yote, Rwanda, Burundi na Uganda Kusini  na ndiyo maana kunako mwaka 1885 (Septemba au Oktoba), Watakatifu Mashahidi wa Uganda walikuja kumtembelea Askofu wao kabla ya kurudi na kuuawa.

Tuzo ya Kituo bora cha Makumbusho huko Bujora, Mwanza
Tuzo ya Kituo bora cha Makumbusho huko Bujora, Mwanza

Wasukuma: Watu wenye Msimamo wa Imani zao

Baada ya utulivu na neema ya Roho Mtakatifu ikiwaongoza, waliweza kufungua misheni nyingi. Maeneo mengi hasa ya Buhaya na Ukerewe, Wamisionari walipokelewa kwa moyo sana isipokuwa katika eneo la Usukuma. Mapokeo yanaeleza kuwa, walikuwa radhi kuwapa wamisionari vyakula, maeneo ya kuishi na kila aina ya ukarimu isipokuwa kusali na kuacha msimamo wa imani zao. Hii iliwapa changamoto wamisionari kiasi kwamba wakafikiria wafanye nini?

Mwanzoni mwa miaka ya 1950, wamisionari walifaulu kupata misheni nyingine ya Bujora (Kisesa) ndipo yaliyopo makumbusho ya Kisukuma. Kwa sababu walikuwa wamejua utamadani kwa Wasukuma na walitaka kufanana nayo kwa kila hali ili kusudi kuleta utamadunisho. Mwanzilishi wa kwanza alikuwa ni Padre David Clement “Fumbuka” aliyekuwa Paroko wa kwanza wa Bujora.

Mapokezi ya Tuzo ya Kituo cha makumbusho ya Bujora,Mwanza
Mapokezi ya Tuzo ya Kituo cha makumbusho ya Bujora,Mwanza

Yeye pamoja na kuanzisha Makumbusho haya alipata wazo la kuunganisha sherehe ya mavuno ya Wasukuma na imani. Kipindi cha mwezi June hadi wa Julai, kiutamaduni Wasukuma walikuwa wanafanya matendo ya kurudisha shukrani kwa mtemi kwa kupeleka vyakula na asilimia kadhaa ya mavuno “kushosha nsikule” kama ilivyokuwa inajulikana kwa lugha yao, kwa sababu kabla yake, mtemi alikuwa akibariki mbegu na mashamba kabla ya kuanza kilimo. Hivyo walitakiwa kutoa shukrani hiyo. Pia, ilikuwa sehemu ya kwenda kuweka hakiba ili njaa ikija, watu wa utemi huo wapatiwe chakula kutoka kwenye hazina kuu ya utawala(tunaweza kufikiria au kufananisha huko Misiri - Mwanzo 42:1-25).

Nyumba ya kitemi yenye taarifa za uongozi katika tawala mbalimbali

Makumbusho ya Kisukuma Bujora: 1968

Makumbusho ya Kisukuma Bujora yalianzishwa rasmi mwaka 1968 katika kijiji cha Kisesa, Mwanza, na mmisionari Mkanada Padre David Clement ikiwa ni namna ya kuwavuta watu katika imani kwa njia ya utamadunisho. Kadhalika, ilikuwa ni njia ya kutunza historia, mila, desturi na mfumo mzima wa Maisha ya msukuma.Tofauti na mifano mingi ya makumbusho ya kikoloni barani Afrika, makumbusho haya yalianzishwa kama mradi wa kijamii uliolenga kunufaisha jamii ya Wasukuma wenyewe na vizazi vijavyo, badala ya kuwaonyesha watalii tu vitu vya kale kama kujifunza.

Nyumba yenye taarifa za makundi ya ngoma ya Bagalu na Bagika

Malengo ya Makumbusho

Lengo kuu la makumbusho haya ni kuhifadhi, kukuza, na kusherehekea sanaa na utamaduni wa Wasukuma, kabila kubwa zaidi nchini Tanzania. Malengo mahususi ni pamoja na: Kutoa mazingira ya kufundisha na kujifunza ambapo wazee wa Kisukuma wanawafundisha vizazi vichanga historia na sanaa za jadi. Pia, Kutunza na kuonesha masalia na kazi za sanaa kutoka nyakati za watemi wa Kisukuma na vyama vya ngoma. Makumbusho yanaweza kuhakikisha utamaduni unabaki hai kupitia shughuli kama vile mashindano ya ngoma, badala ya kuweka vitu kama "vitu vilivyokufa" kwenye kabati za maonyesho.

Vitu vinavyotunzwa na kupatikana

Katika Makumbusho ya Kisukuma Bujora, vitu vinavyotunzwa vimegawanywa katika sehemu kuu tano zinazowakilisha maisha, imani, na teknolojia ya Wasukuma:

Zana na Teknolojia

Vifaa vya Uhunzi: Maonyesho ya jinsi majirani zao Walongo walivyofanya kazi ya chuma, ikiwemo mifuo (bellows) ya kutoa upepo, nyundo za mawe, na majembe ya asili.

Zana za Kazi: Zana za kilimo, uwindaji (kama pinde na mishale), na uvuvi. Vifaa vya Nyumbani: Vyungu vya udongo, vikapu, na vyombo vya kupikia vilivyotengenezwa kwa mkono.

Vitu vya Kitemi na Utawala

Ngoma za Kifalme: Mkusanyiko mkubwa wa ngoma za asili kutoka himaya mbalimbali za machifu wa Kisukuma.

Viti vya Enzi: Viti vilivyotumiwa na machifu (Ntemi) wakati wa utawala wao.

Mavazi ya Kifalme: Ngao, mikuki, na ushanga uliotumiwa na viongozi wa kijadi.

Tiba na Kiutamaduni

Kuna nyumba ya Mganga (Iduku): Jengo lililojengwa kwa mfumo wa kienyeji ambalo ndani yake mna vifaa vya waganga wa jadi.

Vifaa vya Tiba: kuna vibuyu vya dawa, pembe za kinga, manyoya ya ndege, na vifaa vya uganga na ramli

Sanaa na Burudani

Mavazi ya Ngoma: Mavazi ya kipekee yanayotumiwa na vyama vya ngoma kama Bagika na Bagalu.

Zana za Sanaa: Vinyago vya mbao na shanga zenye nakshi zinazoonyesha ubunifu wa Wasukuma.

Wanyama Hai: Kuna banda la nyoka (chatu) wanaotumiwa na wachezaji wa ngoma wakati wa maonyesho.

Usanifu wa Majengo wa Kiutamaduni

Nyumba za Jadi: Mfano wa kambi au makazi ya familia ya Kisukuma (homestead) yanayoonesha mgawanyo wa vyumba na maisha ya kila siku.

Kanisa la Bujora

 Kanisa la Bujora: Jengo la kipekee lililojengwa kwa mtindo wa nyumba ya asili ya Kisukuma, likiwa na mchanganyiko wa alama za Kikristo na tamaduni za wenyeji.

19 Februari 2026, 11:20