Tafuta

2022.10.03 Lampedusa, Comitato 3 ottobre

Jumuiya ya Mt.Egidio yahimiza juhudi za uokoaji kufuatia mkasa wa boti ya wahamiaji!

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ilitoa wito wa kujitolea kwa upya katika shughuli za uokoaji na njia salama za uhamiaji kufuatia na mkasa mwingine wa wahamiaji katika Bahari ya Mediterania hivi karibuni.

Linda Bordoni na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao Makuu yake jijini Roma imeelezea huzuni kubwa kufuatia mkasa wa hivi karibuni wa Meli ya wahamiaji katika Bahari ya Mediterania, na kurudia wito wake wa sera iliyoboreshwa na ya kibinadamu zaidi kuhusu shughuli za uokoaji na njia salama kwa watu walio katika mazingira magumu. Wito wake unakuja huku zaidi ya watu 70 wakiripotiwa kupoteza maisha yao wakati chombo chao kilipozama pwani ya Libya siku ya Jumamosi  Kuu,  tarehe 4 Aprili 2026.

Mkasa huo, ambao ulitokea usiku wa Mkesha wa  Pasaka, ulijulikana tu baada ya manusura kadhaa kuokolewa. Walisema boti hiyo ilikuwa imeondoka Jajoura nchini Libya ikiwa na watu wapatao 105 ndani yake na ni  watu 32 pekee waliothibitishwa kunusurika. Mkasa huo wa Meli unafuatia baada ya mkasa mwingine kama huo Juma lililopita, ambapo wahamiaji 19 wa Afghanistan, akiwemo mtoto mchanga, walifariki katika Bahari ya Aegean karibu na Bodrum, Uturuki. Kulingana na Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM, inasemakana wahamiaji 683 hivi wamepoteza maisha yao au wamepotea tangu mwanzo wa 2026.

Wito  wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio

Katika taarifa, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ilitoa rambirambi zake kwa familia za waathiriwa, ikikumbuka kwamba mkasa huu wa hivi karibuni unaongeza mfululizo wa ajali za Meli za hivi karibuni katika ufukwe wa Sicilia na Bahari ya Aegean. Ilionya dhidi ya kuongezeka kwa kutojali, ikibainisha kuwa matukio kama hayo yana hatari ya kupunguzwa hadi takwimu tu. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pia ilirejea wito wake kwa taasisi za kitaifa na Ulaya kuimarisha juhudi za utafutaji na uokoaji katika bahari ya Mediterania. "Kujitolea zaidi kunahitajika ili kuokoa maisha ya wale walio hatarini baharini," ilisema.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ilisisitiza umuhimu wa kuongeza njia za kawaida za kibinadamu kwa wahamiaji ambazo zinahakikisha kupita salama na kisheria na kutoa michakato ya ujumuishaji, ikiwa ni pamoja na uandikishaji wa shule kwa watoto, kujifunza lugha na fursa za kazi. Pia ilisisitiza hitaji la majibu yaliyopangwa kwa wale wanaokimbia migogoro, ikisisitiza mipango inayokuza ujumuishaji. Mpango wa mkondo ya  kibinadamu ambao Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeuendeleza katika muongo mmoja uliopita, pamoja na mashirika washirika, hadi sasa umewawezesha zaidi ya watu 8,500 walio katika mazingira magumu kufika Ulaya salama.

JUMUIYA YA MT. EGIDIO

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

 

 

08 Aprili 2026, 11:57