Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani: Tasnia ya Habari, Msingi wa Maendeleo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani kuanzia tarehe 24 hadi 28 Machi 2026 limenogeshwa na kauli mbiu: Tasnia ya Habari, Msingi wa Maendeleo ya Kiswahili Duniani na kufunguliwa rasmi na Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akisindikizwa na Mheshimiwa Paul Christian Makonda, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Jumla ya watu 843 wameshiriki katika Kongamano hili. Waswahili wanasema fikra zinapokutana huzaa mawazo na kwamba, Kongamano hili hufanyika kila baada ya miaka miwili na kwa mara ya kwanza liliasisiwa na Dkt. Muhammed Seif Khatibu, tarehe 29 Novemba 2006, wakati huo akiwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo. Alizaliwa tarehe 10 Januari 1951 na kufariki dunia tarehe 15 Februari 2021 huko Unguja, Zanzibar. Kumbe, anakumbukwa kwa mchango wake katika kukuza na kusambaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania na kwamba, amefariki dunia, akiwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, (BAKIZA.) Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO tarehe 23 Novemba, 2021 lilitangaza rasmi kwamba, tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Maadhimisho Kiswahili Duniani, MASIKIDU. Lugha kama chombo cha amani, umoja, ustawi na maendeleo ya wengi; Lugha kama nyenzo ya: utulivu, uadilifu, ukweli na haki katika ujenzi wa mustakabali wa Kitaifa na Kimataifa, katika kukuza na kudumisha: heshima, uvumilivu, huruma na wala si ukatili. Hatua hii inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza Afrika kutambulika na Umoja wa Mataifa na chenye siku maalumu ya kuadhimishwa. Kiswahili hadi sasa tayari kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika SADC, na Bunge la Afrika na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani na kwamba, idadi yao inakadiriwa kuwa ni zaidi ya watu milioni 500.
Kazi inaendelea vyema kutangaza lugha adhimu na aushi ya Kiswahili duniani na kwamba, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA ni mlinzi, kisima, mgodi wa Tanzania na shuhuda wa kudumu katika kusikiliza, kujifunza na kudumisha Lugha ya Kiswahili Barani Afrika. Mkutano huu umeadhimishiwa Jijini Arusha: Mahali ambapo Tanzania ilipitisha Azimio la Arusha kunako Mwaka 1967; Arusha ni Kitovu cha diplomasia ya Afrika na Utalii duniani. Hii ni changamoto na fursa kwa Lugha ya Kiswahili kwenda sanjari na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia inayobeba na kudumisha lugha, diplomasia, uchumi, ustawi na maendeleo ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kuwa makini na tamaduni, ustaraarbu, historia na usuli wa lugha ya Kiswahili, ili kukuza na kudumisha utamaduni, haki, amani na ushirikiano. Kwa hakika mchango wa Tasnia ya habari ni mkubwa, lakini kuna haja ya kuwa makini zaidi na utumiaji wa teknolojia ya Akili Unde, ili kuongeza maudhui na wala si kupotosha, ili kuweza kufikisha ujumbe kwa usahihi na ubora zaidi. Kumbe kuna haja ya kuwa na matumizi sahihi na sanifu ili kulinda na kudumisha lugha ya Kiswahili. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema lugha ya Kiswahili inaendelea kuimarika kimataifa na kuwa mhimili wa utambulisho wa Afrika pamoja na chombo muhimu cha kukuza diplomasia, elimu na maendeleo. Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo alipohutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama tarehe 20 Februari 2026, yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Jijini Paris, Ufaransa ambapo aliwakilisha Serikali ya Tanzania. Alikazia kwamba, zaidi ya watu milioni 500 duniani wanazungumza Kiswahili, jambo linalothibitisha nafasi yake kama lugha ya kimkakati katika diplomasia na uchumi wa Kimataifa.
Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali imeanza mazungumzo na UNESCO pamoja na Uongozi wa Kampuni Mama inayomiliki Faceebok, Instagram na WhatsApp (META) ili Lugha ya Kiswahili itambulike rasmi kwenye Majukwaa ya Kimtandao na kuwawezesha vijana wanaotengeneza maudhui kwa lugha hiyo walipwe malipo makubwa kulingana na kazi zao. Amesema hayo wakati wa Kongamano la 5 la Idhaa za Kiswahili duniani, ambapo amebainisha kuwa licha ya maudhui ya Lugha ya Kiswahili hususani ya Tanzania kuwa mazuri na kupata watazamaji wengi lakini warushaji maudhui hayo wanalipwa kidogo kutokana na lugha hiyo kutokuwa rasmi kwenye majukwaa ya mitandao hiyo ukilinganisha na Lugha ya Kiingereza: "Leo hii unamkuta Mtu wa Tanzania ana “followers” zaidi ya milioni 3, akipost wanaotazama ni wengi ila hapati pesa kupitia Instagram, Facebook, TikTok hawawalipi kwa sababu Kiswahili bado watu wa META na wenye majukwaa ya mitandao Duniani hawajakitambua Kiswahili kama lugha rasmi” alisisitiza Mhe. Makonda. Kiswahili kiwe ni bidhaa ya kupeleka upendo sehemu mbalimbali za dunia. Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika hotuba yake ya ufunguzi amewapongeza: walumbi, washititi, wanagenzi na wajuvi wa lugha adhimu na aushi ya Kiswahili kwa kukuza, kudumisha sanjari na kuimarisha lugha ya Kiswahili kama mhimili wa kuimarisha elimu, demokrasia, ubunifu wa kidigiti; kukuza maudhui na tehema katika sekta binafsi na watumishi wa umma. Amewataka watu wote hawa kuwa walinzi wa rasilimali na miundombinu, ili kukuza na kudumisha haki na amani; uaminifu, uzalendo, ili hatimaye kuweza kupata ustawi, maendeleo na mafanikio, kwani amani na maendeleo endelevu ni chanda na pete.
Mada zilizowasilishwa katika Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani ni pamoja na: Mchango wa Idhaa za Kiswahili katika maendeleo ya Lugha ya Kiswahili na kujenga utangamano wa kijamii. Idhaa hizi zimechangia katika: Ukuaji; ongezeko la misamihati; Ongezeko la mawanda ya Lugha ya Kiswahili katika: sekta ya: afya, uchumi na sheria na hivyo kuongeza ukubalifu wa lugha na kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaotumia lugha ya Kiswahili na kwamba, UNESCO imeitambua Lugha ya Kiswahili katika mawasiliano ya Kimataifa na hivyo kukoleza mtangamano wa kijamii. Changamoto zinazoikabili lugha ya Kiswahili ni pamoja: kuchanganya lugha, udondoshaji wa lugha; upungufu wa rasilimali watu na fedha; miundo mbinu sanjari na wataalamu wa lugha. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika lugha ili kuwapata wataalam wa lugha watakaotoa elimu fasaha na sanifu pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanatumia vitendea kazi vya lugha; fasiri ya idhaa; Radio Mtandao viimarishwe kwani maendeleo na mafanikio ni mambo yanayokamilishana katika tasnia ya habari.
Mada ya Pili ilikuwa ni tathmini ya Makosa ya Lugha na nafasi ya Uhariri katika Idhaa za Kiswahili duniani. Hapa nafasi ya Mhariri ilitiliwa mkazo kwani makosa ni changamoto katika mabadiliko ya lugha: Kisarufi, kimatamshi, kimantiki na katika tafsiri: ya Neno na Tafsiri sisi. Kumbe uhariri makini ni msingi wa maendeleo ya lugha duniani. Mhariri ni mlinda mlango mkuu wa makosa ya kisarufi na kimantiki na kwamba, kozi ya lugha ya Kiswahili iwe ni lazima kwa wanahabari. Mada ya tatu ilihusu: Uchambuzi wa makosa ya matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika vipindi vya watoto. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watoto wanapewa malezi na makuzi bora pamoja na kuwa na miongozo ya matangazo ya watoto inayozingatia utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika katika ujumla wake. Maudhui ya watoto yazingatie: umri, mazingira na senteso ziwe fupi. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika mafunzo kwa waongozaji wa vipindi vya watoto. Watangazaji wajiendeleze, na wafanye tafiti ili kuitendea haki dhamana waliyokabidhiwa.
Mada ya Nne ilikuwa ni kuhusu: Tafsiri na ukalimani katika taarifa za vyombo vya habari kama msingi wa maendeleo ya Kiswahili duniani. Tafsiri na ukalimani ni taaluma muhimu zinazowezesha mawasiliano kati ya lugha tofauti. Tafsiri ni mchakato wa kuhamisha matini ya maandishi kutoka lugha moja kwenda nyingine (k.m., Kiingereza kwenda Kiswahili), huku Ukalimani ukihusu uhamishaji wa ujumbe wa mazungumzo ya mdomo papo kwa hapo. Taaluma hizi zinahusisha uchambuzi wa kiutamaduni na kimuktadha ili kuhakikisha maana sahihi inafikishwa: Hapa kuna lugha ya kunenwa na lugha ya alama: Kuna tafsiri ya habari: Manukuu; Ubandikishaji wa sauti, Uchopezi sauti pamoja na tafsiri ya kidijitali. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika lugha ya Kiswahili kwa mafano: Mfumuko wa bei, uchumi wa kidijitali, uchumi wa bluu; Ndege zisizo na rubani “Drones,” Uhalifu wa mtandaoni, UVIKO-19; Vitakasa mikono, Barakoa n.k. Kimsingi kumekuwepo na upanuzi wa mawanda ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya Maarifa; kama bidhaa; pamoja na Matumizi ya majukwaa ya Kidigitali Changamoto kubwa ni hatari ya kubomoka kwa lugha, jambo la msingi ni kuendelea kujikita katika ubora wa habari, kutoa ajira kwa wataalam wa lugha sanjari na kuimarisha uhariri pamoja na kubainisha istilahi. Watengenezaji wa maudhui kidigitali na ukuaji wa teknolojia lazima ujiepushe na makosa ya kimantiki na kisarufi, kumbe, mafunzo ni muhimu katika kufasiri habari.
Mada ya tano ilikuwa ni Nafasi ya Tasnia ya Habari katika Uundaji, Uenezaji na Matumizi ya Istilahi za Kiswahili. Hapa kumetolewa changamoto, mamlaka ya matumizi ya istilahi mpya; majukwaa ya mitandao ya kijamii; walimu wa lugha fasaha na sanifu pamoja na wachafuzi wa lugha wanaobadili maana na desturi ya lugha ya Kiswahili. Mkazo ni matumizi sahihi ya Kiswahili fasihi na sanifu kadiri ya utamaduni wa Waswahili. Na mada ya Sita ilihusu: Makosa yaliyozoeleka kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili, changamoto kwa Waswahili ni kulumba kwa Kiswahili. Tanzania, pamoja na Kenya na Uganda, itakuwa mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kuanzia tarehe19 Juni hadi tarehe 18 Julai 2027. Mashindano haya, ya 36, yatafanyika katika viwanja kadhaa nchini Tanzania, vikiwemo vya: Benjamin Mkapa, Samia Suluhu Hassan, Dodoma, na Amaan, yakionesha ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mhe. Paul Makonda, amesema, hii ni fursa kwa Tanzania kukuza uchumi, kujenga ndoto za vijana wa kizazi kipya sanjari na kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Maazimio yaliyotolewa kwenye Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani kuanzia tarehe 24 hadi 28 Machi 2026 lililonogeshwa na kauli mbiu: Tasnia ya Habari, Msingi wa Maendeleo ya Kiswahili Duniani yatatekelezwa kwa vitendo na Wizara husika pamoja na Taasisi za Lugha ya Kiswahili ili kuhakikisha kwamba, lugha ya Kiswahili inapiga hatua kubwa zaidi.
Hatimaye, washititi na walumbi wa Lugha ya Kiswahili, walipata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha, uhifadhi wa eneo hili ulianza tangu mwaka 1907, kama eneo la kufugia ng’ombe, mwaka 1960 eneo la Kasoko ya Ngurudoto lilitangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa ikijulikana kama Hifadhi ya Taifa Ngurudoto, lakini baadae ilibadilishwa jina na kuitwa Hifadhi ya Taifa Arusha, ikiwa na jumla ya Kilometa za mraba 322. Hii ilikuwa ni fursa kwa washititi na walumbi wa lugha ya Kiswahili kujamiana kwa karibu zaidi wakati wa kutembelea vivutio vya utalii. Kati ya maneno yaliyobaki katika akili na nyoyo za washiriki hawa ni: Kujamiana katika maana yake chanya; Kunyandua na Kuchotoa! Kwa habari zaidi, tukutane tena Mwaka 2028 kwani muda unaenda matiti.