Tafuta

FILE PHOTO: Soldiers from Burkina Faso patrol on the road of Gorgadji in the Sahel region, Burkina Faso

Chad:Mashambulizi ya Anga ya Chad dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram

Mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Chad dhidi ya washukiwa wa kijihadi wa Boko Haram kando ya Ziwa Chad yameripotiwa kuwaua raia kadhaa,wakiwemo wavuvi waliokamatwa katika mzozo huo.Mashambuliziyameongeza ukosefu wa usalama katika eneo hilo tangu mwanzo mwa Mei.Papa Leo XIV mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu alitoa wito kuingilia kati kuhusu mashambulizi haya..

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Ndege za jeshi la Chad zilianzisha mfululizo wa mashambulizi ya anga kuanzia tarehe 8 Mei 2026  dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram wanaofanya kazi karibu na Ziwa Chad, eneo linaloshirikiwa na Chad, Nigeria, na Niger. Kulingana na ripoti za ndani, kwa mujibu wa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, mabomu hayo yalishambulia maeneo ambapo wavuvi walikuwa wameendelea kufanya kazi kwa ruhusa ya vikundi vya kijihadi vinavyodhibiti sehemu za ziwa. Wavuvi kadhaa wanaaminika kuuawa wakati wa mashambulizi hayo, huku wengine 40 hawajulikani walipo.

Papa Leo XIV aliwakikishia ukaribu wake

Baba Mtakatifu  Leo XIV alionesha  wasi wasi  kuhusu Eneo la Sahel (Chad na Mali) na kutia moyo  mara baada ya sala ya Malkia wa Mbingu, akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume, kwa kuwageukia waamini na mahujaji waliotoka pande za dunia wakiwa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 10 Mei 2026. Papa Leo alisema:  “Kaka na dada wapendwa, nimepokea kwa wasiwasi kuhusu habari za ongezeko la vurugu katika eneo la Sahel, hasa Chad na Mali, zilizokumbwa na mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni. Papa Leo XIV aliendelea: “Nawahakikishia maombi yangu kwa ajili ya waathiriwa na ukaribu wangu na wote wanaoteseka.Ninatumaini aina zote za vurugu zitaisha na kuhimiza kila juhudi kwa ajili ya amani na maendeleo katika nchi hiyo pendwa.”

Kwa  njia hiyo , Operesheni ya kijeshi ilizinduliwa kujibu shambulio la wanajihadi la Mei 4 ambapo wanajeshi 23 wa Chad walipoteza maisha yao. Kwa mujibu wa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, Siku mbili tu baadaye, mapigano mengine ya vurugu kando ya ziwa yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 27, wakiwemo wanajeshi 11 na wapiganaji 16 wa wanajihadi. Bonde la Ziwa Chad kwa muda mrefu limetumika kama ngome ya Boko Haram na makundi mengine yenye msimamo mkali, ambayo shughuli zake zimevuruga jamii kote katika eneo hilo kwa miaka mingi.

Vurugu zinazochochewa na zaidi ya ujihadi

Zaidi ya tishio linalosababishwa na makundi yenye msimamo mkali, eneo la Ziwa Chad linaendelea kukabiliwa na migogoro ya kina inayohusiana na matumizi ya ardhi, malisho ya mifugo, na mvutano wa kikabila. Sehemu kubwa za kusini, kati, na mashariki mwa Chad zimekuwa na vurugu ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, na kuchangia pakubwa ukosefu wa usalama nchini. Wanachama wa kabila la Zaghawa wameshutumiwa na jamii za wenyeji kwa kuiba mifugo katika eneo la ziwa, ikidaiwa kuwa chini ya ulinzi wa wanajeshi wenye ushawishi. Ripoti zinaonyesha kwamba baadhi ya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Chad yanaweza yasiwe yamehusishwa tu na shughuli za wanajihadi bali pia kulipiza kisasi na wafugaji wa eneo hilo ambao ng'ombe zao zimechukuliwa.

Hata hivyo wachambuzi wanakadiria kwamba kati ya 2021 na 2024, migogoro iliyowahusisha wakulima na wafugaji ilisababisha vifo zaidi ya 1,000 na karibu majeraha 2,000 kote Chad, ikifichua ukubwa wa mgogoro unaoathiri jamii za vijijini. Kadri shughuli za kijeshi zinavyoendelea kuzunguka Ziwa Chad, hofu inabaki kuwa kubwa kwamba raia walionaswa kati ya vikundi vyenye silaha na vikosi vya usalama wataendelea kubeba mzigo mzito zaidi wa mgogoro huo.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

12 Mei 2026, 16:01