Karibu watoto 60 wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa nchini Lebano
Na Sr. Christine Masivo,CPS –Vatican.
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) lilisema kwamba watoto wapatao 59 waliripotiwa kuuawa au kujeruhiwa nchini Lebanon hivi karibuni licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano tarehe 17 Aprili 2026. Kulingana na Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon, watoto wapatao 23 wameuawa na 93 wamejeruhiwa tangu mapigano kuanza. Tangu tarehe 2 Machi 2026, jumla ya watoto 200 wameripotiwa kuuawa na 806 wamejeruhiwa. UNICEF ilisema takwimu hizo zinafikia karibu watoto 14 wanauawa au kujeruhiwa kila siku. Shirika hilo lilitoa wito kwa pande zote kuwalinda watoto, kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, na kuchukua hatua zote muhimu ili kuhakikisha kusitisha mapigano kunadumu.
Mkurugenzi wa Kanda wa UNICEF wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Edouard Beigbeder, alisema watoto wanapaswa "kurudi madarasani, kucheza na marafiki, na kupona kutokana na miezi ya hofu na msukosuko." "Hata hivyo, ukweli unaonekana kuwa tofauti sana," alisema. "Mashambulizi yanayoendelea yanaua na kuwajeruhi watoto, yanaongeza hatari ya kupata majeraha na kuacha matokeo mabaya ambayo yanaweza kudumu maisha yote."
UNICEF ilikadiria watoto 770,000 wanapitia dhiki kubwa kutokana na kukabiliwa na vurugu mara kwa mara, hasara na kuhamishwa. Shirika hilo lilisema watoto na walezi wameripoti dalili zinazohusiana na msongo wa mawazo na huzuni, ikiwa ni pamoja na hofu, ndoto mbaya, kukosa usingizi na kukata tamaa. Lilionya kwamba bila afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia, watoto wengi wana hatari ya kupata matatizo ya kisaikolojia ya muda mrefu. UNICEF ilisema uwekezaji wa haraka katika afya ya akili na huduma za kisaikolojia unahitajika ili kuwasaidia watoto kupona kutokana na athari za mzozo.