Tafuta

Vifo vinazidi kuongezeka kwa ebola huko vurugu zikiendelea. Vifo vinazidi kuongezeka kwa ebola huko vurugu zikiendelea.  (AFP or licensors)

Mkuu wa WHO atoa wito wa kusitisha mapigano huku Ebola ikisambaa DRC

Kufuatia na mgongano wa vita na magonjwa hasa Ituri huko DRC yanavuruga mipango ya kudhibiti mlipuko wa Ebolo na ni vigumu kuhudumia wagonjwa huku mabomu yakilipuka.Kwa njia hiyo kuna tishio na kazi ya kusambaa kwa Ebola ikiwa hali inaendelea hivyo.Dharura imetolewa na Mkuu wa WHO.

Umoja wa Mataifa

Ongezeko la vurugu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, linakwamisha juhudi za kudhibiti mlipuko wa Ebola, hivyo tunasihi pande zinazokinzana zisitishe mapigano. Ni wito wa dharura wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus kwa makundi yaliyojihami eneo hilo ambako ndiko mlipuko wa 17 wa Ebola umeripotiwa na hadi sasa watu 105 wamethibitishwa kuambukizwa aina ya virusi vya Bundibugyo visivyo na tiba wala chanjo na kati yao  10 wamepoteza maisha.

WHO ni shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, ambalo Mkuu wake huyo kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter alisema akionya  kwamba kuongezeka kwa vurugu kunadhoofisha juhudi za kudhibiti mlipuko unaokua kwa kasi hususan jimboni Ituri ambako ndiko kitovu cha mlipuko wa sasa.

Vita na ugonjwa vinashindana

Alisema kinachoendelea sasa ni mgongano wa kihistoria katiya magonjwa na mizozo akisema kwamba mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo “unazidi kasi ya mwitikio.” Dkt. Tedros amekumbusha kuwa virusi vya Ebola vya Bundibugyo havina chanjo wala matibabu yaliyothibitishwa, hivyo “kukomesha maambukizi kunategemea kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa usaidizi wa kibinadamu.” Hata hivyo wahudumu wa afya wanasema mapigano yanayoendelea kati ya makundi yenye silaha mashariki mwa DRC yamesababisha watu wengi kukimbia makazi yao, na kuwalazimu walio katika hatari ya kuambukizwa kuingia katika kambi za wakimbizi zenye msongamano mkubwa ambako virusi vinaweza kuenea haraka.

Maisha ya raia na wahudumu wa afya hatarini

Kutokuwa na usalama pia kumevuruga mitandao ya ufuatiliaji na kufunga njia muhimu zinazotumiwa na timu za matibabu kufuatilia waliokutana na wagonjwa na kuwaweka waliothibitishwa kuambukizwa katika maeneo ya kutengwa. “Wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele wanahatarisha maisha yao, huku mashambulizi dhidi ya vituo vya afya yakifanya kufuatilia wagonjwa na watu waliokutana nao kuwa karibu haiwezekani,” alisema Mkuu wa WHO.

“Hatuwezi kujenga imani ya jamii au kuwaweka wagonjwa katika maeneo ya kutengwa wakati mabomu yanaporushwa,” alisema akiongeza kuwa, “tunaomba mpatie kipaumbele uhai wa binadamu kuliko kitu kingine chochote.”

Ingawa hivyo video ya WHO nchini DRC iliyochapishwa ukurasa wa  X inaonesha wafanyakazi wakiendelea na ujenzi wa vituo vya matibabu dhidi ya Ebola huko Bunia, mji mkuu wa Ituri, ujenzi unaofanyika kwa usaidizi wa serikali ya Uingereza na Mfuko wa Gates. WHO imeonya kwamba mlipuko huo unaendelea kusambaa kijiografia, huku kukiwa na ushahidi wa maambukizi yanayoendelea kuvuka mipaka.

Mlipuko wa sasa umejikita katika jimbo la Ituri na umeenea katika kanda 11 za afya, huku wagonjwa wakiritipotiwa pia jimboni Kivu Kaskazini — ikiwemo Butembo na Goma — pamoja na Kivu Kusini, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF). Maafisa wa afya wanasema virusi hivyo vya Bundibugyo ambavyo kwa mara ya kwanza viliripotiwa DRC mwaka 2007, vinaendelea kusambaa kupitia makundi ya kifamilia na vituo vya afya, huku maambukizi yakihusishwa na kuwahudumia wagonjwa, mikusanyiko ya kifamilia na taratibu zisizo salama za mazishi.

Imesasishwa tarehe 28 Mei 2026 saa 8.45 alasiri na Angella Rwezaula - Vatican.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

28 Mei 2026, 14:50