Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Kwa Mwaka 2026
Na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania, - Paris, Ufaransa.
Kaulimbiu ya Siku ya Kiswahili Duniani iliyoadhimishwa rasmi tarehe 7 Julai 2026 ni "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Kiuchumi Duniani." Kaulimbiu hii inalenga kuonesha jinsi lugha ya Kiswahili ilivyo daraja la kuleta maendeleo na kuunganisha Mataifa. Waziri mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuna haja ya kutafuta mbinu mpya ya kukieneza Kiswahili baada ya kuwa kimepata hadhi ya kimataifa. “Kadiri Kiswahili kinavyoendelea kupata hadhi ya kimataifa, ni muhimu sasa kuanza kutazama hatua inayofuata ya kukieneza duniani. Mataifa mengi yamefanikiwa kueneza lugha na utamaduni wao kupitia vituo vya utamaduni vilivyoanzishwa katika nchi mbalimbali duniani,” amesema. Ametoa wito huo Jumanne, Julai 7, 2026 wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria kilele cha Maadhimisho ya Tano ya Siku ya Kiswahili Duniani kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za Makao makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO jijini Paris, Ufaransa. “Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kupitia elimu, tafiti, uchapishaji, tafsiri, teknolojia za kidijiti na diplomasia ya lugha. Tutaendelea kushirikiana na UNESCO, nchi mbalimbali, vyuo vikuu, taasisi za Kimataifa na wadau mbalimbali katika kuendeleza lugha hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema sasa hivi Kiswahili kimeshatambulika kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC “East African Community” na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika “Southern African Development Community” SADC. “Kiswahili ndiyo utambulisho wetu wana Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mtu akiongea Kiswahili anajulikana kuwa anatokea Tanzania, Burundi, DRC au Sudan Kusini. Na pia kimekuwa moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU),” amesema. “Si hivyo tu, sasa hivi Kiswahili kinatambulika kuwa ni lugha rasmi ya mikutano mikubwa ya UNESCO kutokana na pendekezo lililopitishwa kwa kaulimoja Novemba, 2025 wakati wa Mkutano Mkuu wa 43 wa UNESCO, uliofanyika Samarkand, Uzbekistan.” Amesema kwa mujibu wa wataalamu wa lugha, Kiswahili kinazungumzwa na watu kati ya milioni 300 hadi milioni 500 na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kutokana na matumizi yake katika elimu, biashara, vyombo vya habari, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii. “Hali hiyo inaonesha kwamba Kiswahili siyo mali ya Watanzania pekee bali ni urithi wa Afrika na zawadi ya Afrika na dunia. Kiswahili kinaunganisha watu, Kiswahili kinaunganisha biashara, Kiswahili kinaunganisha jamii,” amesisitiza.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Prof. Khaled El-Enany aliwaeleza washiriki wa maadhimisho hayo kwamba shirika lake limesaidia kufadhili uandaaji wa kamusi ya Kifaransa kwenda Kiswahili. “Mbali na matumizi ya kawaida kwa watalii au watu wanaojifunza lugha, tunatarajia kwamba uwepo wa kamusi hiyo na nyaraka nyingine kutasaidia kuongeza fursa kwa walimu na wanafunzi wanaojifunza Kifaransa na Kiswahili,” amesema. Amesema uzuri wa Kiswahili ni lugha ambayo imekuwa ikiendelea kukua na kuvuka mipaka bila kupoteza uasili wake na imeunganisha watu bila kulazimika kuvuka mipaka ya nchi zao. Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alisema Tanzania ina lugha za makabila zaidi ya 150 katika maeneo mbalimbali lakini wananchi wake wameweza kuunganishwa na lugha moja ya Kiswahili. Alisema wakati jijini Paris, Ufaransa wakiadhimisha kilele cha maadhimisho hayo na kongamano la pili lililoandaliwa na UNESCO kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, nchi nyingine tatu za Uingereza, Algeria na Burundi nazo pia leo zimeadhimisha makongamano kama hayo. Awali, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Bw. Saidi Othman Yakub alisema maadhimisho hayo ya tano ambayo yanafanyika sambamba na Kongamano la Pili la Siku ya Kiswahili Duniani, yamevutia washiriki zaidi ya 300 kutoka nchi 16 duniani. Amezitaja nchi hizo kuwa ni Comoro, Tanzania, Ujerumani, Marekani, Canada, Uingereza, Italia, Luxembourg, Sweden, Ubelgiji, Austria, Uturuki, Misri, Kenya, Uganda na wengi kutoka Tanzania. “Tangu tarehe 4 Julai hadi leo tarehe 7 Julai, 2026 tumeshuhudia shughuli mbalimbali zilizolenga kuendeleza na kukitangaza Kiswahili duniani. Shughuli hizo zilijumuisha matembezi ya hamasa katika mitaa maarufu ya Jiji la Paris, hafla za vyakula vya Kiswahili kwa Diaspora, kongamano kuhusu nafasi ya Kiswahili katika biashara na uchumi, semina na warsha mbalimbali hapa UNESCO. Amesema waliandaa pia tamasha la Usiku wa Mswahili lililofanyika chini ya Mnara wa Eiffel kandokando ya Mto Seine, maonesho ya filamu na chakula pamoja na kazi za Kiswahili.
Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba amewaalika wafanyabiashara kutoka Ufaransa kuwekeza nchini Tanzania kwani ina fursa ya kutengeneza ajira, kuhamisha ujuzi na kujenga uchumi wa viwanda kwa faida ya nchi zote mbili. “Leo tumefanya mjadala wa kibiashara na sote tumeshuhudia makubaliano yakisainiwa baina ya Tanzania Private Sector Foundation na International Chamber of Commerce (ICC). Makubaliano haya siyo tu mkataba wa kawaida bali ni daraja la kutupeleka kwenye mafanikio makubwa huko mbele,” amesema. Waziri Mkuu ametoa wito huo Jumatatu, Julai 6, 2026 wakati akizungumza na washiriki wa mjadala wa kibiashara baina ya Tanzania na Ufaransa (Tanzania-France Business Roundtable) uliofanyika kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania jijini Paris, Ufaransa. “Kwa hiyo ninawahimiza wafanyabiashara wa Ufaransa mtumie vyema fursa hii ya kipekee. Maamuzi yatakayofanywa leo ndiyo yatakayoamua mwelekeo wa sekta za uchumi za kesho kwa nchi zetu. Wale watakaowekeza nchini Tanzania hivi sasa, hawatakuwa tu sehemu ya mageuzi ya uchumi wetu, bali watakuwa washirika wa thamani katika kujenga moja ya uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi barani Afrika kwa vizazi vijavyo.”
Dkt. Mwigulu amesema Ufaransa inao utaalamu wa hali ya juu na wa kiwango cha kimataifa katika teknolojia, uhandisi, nishati, miundombinu, viwanda, masuala ya fedha, na huduma za afya. “Kwa upande wake, Tanzania inao utulivu wa kisiasa, nafasi yake ya kijiografia imekaa kimkakati, inazo rasilimali nyingi za asili, fursa shindani za uwekezaji, usimamizi thabiti wa uchumi pamoja na nguvukazi ya vijana wengi na yenye ari kubwa barani Afrika.” Amesema maeneo hayo yana nguvu na yanakamilishana kwani katika umoja wake yanajenga fursa za kipekee za kukuza maendeleo endelevu na ustawi wenye manufaa ya pande zote mbili. “Tunapoanza kwa ujasiri kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali yetu itaendelea kuwa thabiti katika kuhakikisha kunakuwepo mazingira yanayotabirika, yenye uwazi na rafiki kwa biashara, ambapo uwekezaji unalindwa, ushirikiano unathaminiwa, na mafanikio yanawanufaisha wadau wote,” amesisitiza. Waziri Mkuu pia alishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Chama cha Kimataifa cha Biashara cha Ufanransa (ICC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ambapo Mtendaji Mkuu wa TPSF, Bw. Deo Massawe alibadilishana hati hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa ICC, Bw. Julian Kassum.
Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, aliwaeleza washiriki wa mjadala huo kwamba kitendo kilichofanyika leo kinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inasisitiza ushiriki wa sekta binafsi kwa asilimia 70 katika kuchochea maendeleo ya uchumi. Kwa upande wake, Rais wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula alisema Tanzania ipo katika nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha mageuzi ya uchumi barani Afrika chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Kwa miaka mingi, Ufaransa imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika uwekezaji. Hata hivyo, kwa sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika kujenga ushirikiano wa muda mrefu utakaokuza uhamishaji wa teknolojia, kukuza sekta ya utalii, huduma za kifedha pamoja na uchumi wa kidijitali. TPSF iko tayari kuwezesha ushirikiano huo kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Ufaransa,” alisema. Baadhi ya kampuni za Ufaransa zilizoshiriki mjadala huo zinajihusisha na usimamizi wa nishati ya jua (ikiwemo mifumo ya taa za barabarani), usafirishaji, maji, nishati, ujenzi, viwanda, mazingira na ufugaji wa viumbe maji (ikiwemo uzalishaji wa mwani wa baharini). Kampuni nyingine ni waendeshaji wa huduma za satelaiti wanaotoa suluhisho bunifu kwa huduma za utangazaji wa sauti na picha, intaneti ya kasi (broadband), huduma za data, usafiri wa baharini na anga. Aidha, kulikuwa na wazalishaji wa mabomba maalumu yanayotumika katika sekta ya mafuta na gesi. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde; Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi; Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Balozi Saidi Othman Yakubu; Mtendaji Mkuu wa MEDEF International, Bw. Philippe Gautier; Rais wa Baraza la Biashara la Ufaransa na Afrika Mashariki, Bi. Celine Gouveia; pamoja na wajumbe kutoka sekta binafsi ya Tanzania na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ufaransa.