Mabingwa wa Kombe la Dunia Kwa Mwaka 2026: Timu ya Taifa ya Hispania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo wa XIV katika Waraka wake wa Kitume kuhusu: Thamani ya michezo anakazia kuhusu: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika malezi na majiundo; Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi; Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo na hivyo michezo ikawa ni fursa ya kujenga na kudumisha amani; ukuaji wa udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vita, kinzani na mipasuko ni dalili za kushindwa kwa ubinadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Dunia ina kiu ya amani kumbe, kuna haja ya kutumia nyenzo zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Tunu msingi za michezo katika majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10. Mama Kanisa hana budi kutekeleza dhamana na utume wake hapa ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika michezo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuhusu utaratibu kwa wanariadha: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.” 1Kor 9:24-25.
Hiki ni kielelezo cha mashindano ya kiroho; na kwamba Binadamu ni umoja wa mwili, roho na nafsi na hivyo Mama Kanisa anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya mwanadamu kama mambo muhimu sana katika kuhubiri na kufundisha. Ni katika muktadha huu, Kikosi mashuhuri cha Timu ya Taifa ya Hispania kimefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa 2026 baada ya kuibuka kidedea kwa bao 1- 0 dhidi ya Argentina katika mtanange wa fainali uliochezwa Dominika tarehe 19 Julai 2026. Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa huku timu zote zikionesha kiwango cha juu tangu dakika za mwanzo.
Dakika 90 za mchezo zilimalizika bila timu yoyote kupata bao, na hivyo kuamuriwa kuongezwa muda wa nyongeza. Katika dakika ya 106 ya muda wa nyongeza, mshambuliaji Ferran Torres aliifungia Hispania bao la ushindi lililowafanya mashabiki wake kushangilia na kuipa timu hiyo taji la pili la Kombe la Dunia katika historia yake. Kombe la kwanza katika miaka ya hivi karibuni ni mwaka 2010. Argentina ilijitahidi kusaka bao la kusawazisha lakini ilishindwa kuzitumia nafasi ilizopata. Ushindi huo umeifanya Hispania kuandika historia nyingine kubwa katika soka la dunia, huku Argentina ikimaliza mashindano haya kwa kuwa ni mshindi wa pili.
Katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Mwaka 2026, mgawo wa fedha ulikuwa kama ifuatavyo: Bingwa ambaye kwa sasa ni Timu ya Taifa ya Hispania imejipatia shilingi bilioni 135; Mshindi wa Pili ambaye ni Argentina imepokea kiasi cha Shilingi bilioni 89.1. Uingereza imeishinda Ufaransa na kutwaa nafasi ya 3 kwenye Kombe la Dunia la FIFA la Mwaka 2026 katika ushindi wa kihistoria wa 6-4 kwenye Uwanja wa Miami nchini Marekani na hivyo kujipatia shilingi bilioni 78.3. Nafasi ya nne imechukuliwa na Ufaransa ambayo imejipatia bilioni 72.9. Kwa timu ambazo zimeingia Robo Fainali zimejipatia shilingi bilioni 51.3 na zile ambazo zimeingia Hatua ya 16 Bora zimjipatia kiasi cha bilioni 40.5. Timu ambazo zimefanikiwa kuingia hatua ya 32 Bora zimejipatia bilioni 29 na zile ambazo zimeingia hatua za makundi zimejipatia bilioni 24 na timu ambayo imefuzu kushiriki imejipatia bilioni 4.05.