Tafuta

Bendera ya Umoja wa Afrika Bendera ya Umoja wa Afrika  (Copyright (c) 2021 Flag World)

Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya UA kujengwa Uganda!

Wakati inaadhimishwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Kimataifa,tarehe6 hadi 7 Julai 2026 katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris,nchini Ufaransa,Umoja wa Afrika(UA) umetangaza kuwa"Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Umoja wa Afrika yatajengwa nchini Uganda."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani 2026 yaliyofanyika katika Makao Makuu ya UNESCO, jijini Paris, Ufaransa tarehe 6 na 7 Julai,  yaliwakutanisha viongozi wa serikali, mabalozi, wataalamu wa lugha, wanazuoni, wasanii na wadau wa Kiswahili kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kusherehekea, kuendeleza na kukuza lugha ya Kiswahili kama lugha ya kimataifa. Kiswahili na lugha nyingine ni amali, rasilimali na nyenzo zinazohitaji kutunzwa na kukuzwa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya bnadamu, kama ilivyp lugha nyingine nyingi za kimataifa.

Lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki na kwingineko

Afrika ya Mashariki ina bahati kubwa kuwa na Kiswahili, ambacho ni mojawapo ya rasilimali muhimu ya eneo lake. Si lazima rasilimali ziwe mafuta, almasi, na misitu pekee. Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili ulimwenguni kote  inakisiwa kuwa kati ya watu milioni 150 na 250.  Ramani ya lugha inaonesha kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha kumi na moja zenye wazungumzaji wengi zaidi barani Afrika. Kiswahili ndicho kinashikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa na takribani zaidi ya wazungumzaji milioni 150 barani Afrika (wengi wao wakiwa wenyeji wa Afrika Mashariki). Lugha nyingine Afrika zenye wasemaji wengi ni Amharic, Kioromo , pamoja na Kiarabu (Afrika kaskazini). Katika Afrika ya Magharibi, tuna Kiyoruba na Igbo.

Kujivunia lugha ya Kiswahili

Katika eneo la Afrika ya Kusini tuna Kizulu na Kishona. Kati ya lugha hizi zote, Kiswahili kimeungwa mkono na wataalamu wengi kuwa lingua franca ya Afrika. Kutokana na umaarufu wa Kiswahili, mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuimarisha uundaji na utekelezaji wa sera murua zitakazofanikisha michakato ya ubidhaishaji wake kwa minajili ya kujitajirisha kiuchumi – yanavyofanya mataifa mengine kuhusu lugha zao. Nchini Tanzania hatuna budi kumkubuka Mwalimu Nyerere aliyekuwa na maono mapana kuhusiana na lugha na kuunganisha Taifa kwa lugha moja ya Kiswahili. Ni lazima kujivunie lugha hii kama mama na lugha yetu ya Afrika.

Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Umoja wa Afrika Kujengwa Uganda(UN)

Katika tovuti ya Umoja wa Mataifa (UN) imeandika juu ya fursa nyingine ya Kiswahili. Wakati inaadhimishwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Ulimwenguni kwa mwaka 2026 katika Makao Makuu ya UNESCO, Paris Ufaransa, tukio jingine muhimu lilifanyika la kutangazwa ujenzi wa Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Umoja wa Afrika nchini Uganda. Tukio hili lilielezwa na Makamishina wa Kamisheni ya Kiswahili  ya Umoja wa frika walizungumza na wandishi wa habari jijini Kampala, Uganda.  "Yeyote atakayesema kwamba Kiswahili kilifia Uganda, basi aongeze kwamba pia kilifufuliwa tena Uganda,” amesema Profesa Pacifique Malonga kutoka Rwanda, ambaye ni Kamishna katika Kamisheni ya Kiswahili ya Muungano wa Afrika, (AU) kwa kifupi ACALAN-Kiswahili Prof. Malonga amesema kauli hiyo baada ya hafla ya kutambulisha Kamisheni hiyo mpya ya Kiswahili ya Muungano wa Afrika iliyofanyika jijini Kampala nchini Uganda.

Sasa ifahamike Kiswahili kinafufuka tena  Uganda

Kwa mujibu wa Prof. Malonga, mipango ya kujenga makao makuu ya ACALAN Kiswahili nchini Uganda ni ishara kuwa lugha ya Kiswahili itaendelea kukua na kuenea zaidi barani Afrika na duniani. "Nakumbuka miaka 15 iliyopita tulipopitisha ACALAN Kiswahili, nilikuwa bado kijana mjini Nairobi. Leo ni siku ya furaha kuona Kiswahili kikiendelea kuenea," alisema. Katibu Mkuu wa ACALAN Kiswahili, Dk. Ronex Kisembo Tendo, alisema Makao Makuu ya kamisheni hiyo yanatarajiwa kujengwa jijini Kampala ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa kamisheni mpya. "Natumaini kwamba Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, atawashawishi marais wenzake kuunga mkono ujenzi wa makao makuu ya ACALAN Kiswahili hapa Uganda," amesema Dk. Kisembo.

Profesa  Mutembei: Vijana jifunzeni lugha ya Kiswahili

Kwa upande wake, Profesa Aldin Mutembei wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye ni Mratibu wa ACALAN Kiswahili, amesema huu ni wakati wa vijana kujifunza Kiswahili kwa mkakati ili wanufaike na fursa zinazozidi kuongezeka barani Afrika na duniani. "SADC, inayoundwa na nchi 16, ilipitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi na lugha ya kazi. Hii ina maana kwamba kijana anaweza kwenda kufundisha Kiswahili Botswana, Namibia na nchi nyingine za ukanda huo," alisema Profesa Mutembei. Na alipoulizwa kwa nini makao makuu ya kamisheni hiyo yanajengwa Uganda badala ya nchi nyingine, Prof. Mutembei amesema viongozi wa kamisheni wanaamini Rais Museveni ameonyesha dhamira ya dhati ya kukuza Kiswahili, jambo linalowapa matumaini ya mafanikio makubwa. "Tunakwenda mahali penye mbolea," amesema. Ameongeza kuwa kama makao hayo yangejengwa Rwanda au Burundi, swali hilo hilo lingeulizwa. Kwa hiyo walichagua eneo ambalo wanaamini litatoa matokeo makubwa zaidi. Kwa mujibu wa Profesa Mutembei, ingawa Tanzania ni kitovu muhimu cha Kiswahili, tayari Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo Zanzibar. "Rais Samia Suluhu Hassan ni mswahili halisi, hivyo tunaona ni muhimu kupata pia kinara mwingine wa kuendeleza Kiswahili katika nchi nyingine kama Uganda," amesisitiza.

Dk. Mutenyo: Kamisheni itafundisha Kiswahili kwa mbinu mbalimbali

Naye Dk. Aidah Mutenyo, Kamishna anayehusika na Elimu na Uhamasishaji, alisema kamisheni hiyo itatoa mafunzo kwa watu katika nyanja mbalimbali sambamba na kuhamasisha ufundishaji wa Kiswahili mashuleni. "Mpango wetu ni kueneza Kiswahili kila mahali. Sisi ni kama wamisionari, na Biblia yetu ni Kiswahili," alisema Dk Mutenyo. Kila mwaka tarehe 7 Julai huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili, iliyoanzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) mwaka 2021 kwa kutambua mchango wa lugha hiyo katika kuimarisha mshikamano, mawasiliano na kuhifadhi pamoja na kubadilishana tamaduni duniani.

Siku ya Kiswahili Kimataifa Julai 7

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

07 Julai 2026, 13:29