Tafuta

2026.07.04 Ziara ya Papa Leo XIV huko Lampedusa Julai 4 2026.07.04 Ziara ya Papa Leo XIV huko Lampedusa Julai 4 

UNHCR:Ziara ya Papa Leo XIV huko Lampedusa inatoa wito wa uwajibikaji wa pamoja!

Kabla ya ziara ya Papa Leo XIV huko Lampedusa,Julai 4,Afisa Mawasiliano wa UNHCR,Filippo Ungaro alisema uwepo wa Papa unatoa ukumbusho wenye nguvu kwamba "uhamiaji lazima ushughulikiwe kwa mshikamano,uwajibikaji wa pamoja na kujitolea bila kuyumba kwa ajili ya heshima na ulinzi wa kila mwanadamu."

Na Alessandro Guarasci na Linda Bordoni

Huku Papa Leo XIV akijiandaa kutembelea kisiwa cha Lampedusa cha Mediterania siku ya Jumamosi tarehe 4 Julai 2026, mahali ambapo kwa muda mrefu panahusishwa na msiba na matumaini, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, linasema uwepo wake una ujumbe wenye nguvu kwa ulimwengu unaozidi kuzingatia mipaka badala ya watu Lampedusa, kisiwa cha kusini kabisa mwa Italia, kwa miongo kadhaa kimesimama kwenye njia panda za uhamiaji kutoka Afrika Kaskazini hadi Ulaya. Kwa wakimbizi na wahamiaji wengi wanaokimbia vita, mateso, umaskini na ukosefu wa utulivu, kimekuwa mahali pa kwanza pa usalama baada ya vivuko vya hatari  baharini. Lakini pia ni mahali palipoakisiwa na hasara kubwa, ambapo maelfu wameangamia katika maji yanayokizunguka kisiwa hicho.

Mahali pa huzuni na mahali pa matumaini

Kwa Filippo Ungaro, Afisa Mawasiliano wa UNHCR, ziara ya Papa Leo XIV inakuja wakati muhimu katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu uhamiaji. “UNHCR, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, linakaribisha ziara ya Papa Leo XIV huko Lampedusa mnamo tarehe 4 Julai, 2026.” Alisema hayo kwa vyombo vya habari vya Radio Vatican, akiongeza kuwa “Lampedusa inasalia kuwa moja ya alama zenye nguvu zaidi za njia za kati za Mediterania. Ni mahali pa kuwasili, mahali pa huzuni, na mahali pa matumaini.” Ungaro alibainisha kuwa maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wamepata usalama kisiwani baada ya kuvumilia “safari mbaya ya kuvuka bahari,” huku wengine wengi kama vile wanawake, watoto na wanaume wakipoteza maisha yao wakati wakijaribu kufika fukweni.

Katika muktadha huo, alisema, uwepo wa Papa unazungumza kwa nguvu maalum. "Uwepo wa Papa Leo unatuma ujumbe wazi wakati ambapo mjadala wa kisiasa wa kimataifa kuhusu uhamiaji mara nyingi hujikita katika ulinzi wa mipaka na kuzuia, badala ya ulinzi wa watu na jukumu la pamoja la kusimamia uhamiaji," alisema. Ziara hiyo bila shaka inakumbuka ishara ya kinabii iliyotolewa na Papa Francisko mnamo Julai 2013, wakati Lampedusa ikawa mahali pa ziara yake ya kwanza ya kichungaji nje ya Roma. Katika tukio hilo, alilaani kile alichokiita "utandawazi wa kutojali" mbele ya mateso ya wahamiaji na wakimbizi.

Haja ya kujitolea upya kisiasa

Zaidi ya muongo mmoja baadaye, Ungaro anaamini changamoto zinabaki kuwa za dharura na zinahitaji kujitolea upya kisiasa. Alipoulizwa ni mabadiliko gani yanayohitajika ili kuhakikisha kwamba heshima ya wahamiaji na wakimbizi inaheshimiwa kikamilifu, alielekeza kwenye hitaji la kusawazisha usimamizi mzuri wa uhamiaji na ulinzi wa kweli kwa wale wanaokimbia hatari. "Umoja wa Ulaya lazima uweze kuchanganya usimamizi mzuri wa mtiririko wa uhamiaji na ulinzi halisi wa wale wanaokimbia vita, mateso na ukiukwaji wa haki za binadamu," alisema.

Mkataba wa EU kuhusu Uhamiaji na Hifadhi

Ungaro alirejelea Mkataba wa EU kuhusu Uhamiaji na Hifadhi uliopitishwa hivi karibuni, akibainisha kuwa unatoa fursa za uratibu mkubwa miongoni mwa Nchi Wanachama. "Mkataba wa EU una uwezo wa kuleta uboreshaji mkubwa miongoni mwa Nchi Wanachama katika usimamizi wa wageni wanaowasili na katika maombi ya ulinzi wa kimataifa," alielezea. "Lakini changamoto kuu inabaki kuwa utekelezaji wake thabiti na wa kiutendaji." Alisisitiza kwamba zaidi ya mifumo ya kisheria, swali hatimaye linahitaji utashi wa kisiasa na kujitolea zaidi kwa mshikamano wa kimataifa. “Jambo lingine ni hitaji la kutoa msaada mkubwa zaidi kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi wengi duniani,” Ungaro alisema, akibainisha kuwa karibu asilimia sabini ya wakimbizi wanahifadhiwa na mataifa yenye kipato cha chini na cha kati. Kwa maana hiyo, alihitimisha, “tunahitaji ushiriki mkubwa wa majukumu katika usimamizi wa mtiririko wa uhamiaji.”

Imesasishwa Ijumaa tarehe 3 Julai 2026 saa 4.00 asubuhi na Angella Rwezaula.

ZIARA YA YA PAPA LAMPEDUSA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

03 Julai 2026, 10:04