Dkt Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais Tanzania Atangaza Kujiuzulu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake, huku akieleza kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina. Katika taarifa kwa umma iliyotolewa, tarehe 25 Agosti 2026, Dkt. Nchimbi amesema ameamua kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais pamoja na kujiondoa katika utumishi wa umma, kuanzia Septemba 4, 2026 na kwamba pamoja na kustaafu siasa na utumishi wa umma, ataendelea kuwa ni raia mwema wa Tanzania. Amenukuu kifungu cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutimiza ahadi yake ya kujiuzulu ikiwa kungehitajika mabadiliko.
Taarifa yake inasomeka hivi: “Leo tarehe 25 Agosti 2026, nimemwandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumjulisha kuwa nimeamua kustaafu siasa na utumishi wa umma. Hivyo, nitajiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuzingatia Ibara ya 50(2)(c) ikisomwa kwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba, kuanzia tarehe 04 Septemba 2026. Tarehe 27 Agosti 2025, nilimuahidi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa nitamsaidia yeye na Nchi yetu kwa uwezo wangu wote na kwa uaminifu. Pia, nilimuhakikishia kuwa siku yoyote akiona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, nitaachia nafasi hii. Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu. Kipekee, namshukuru Mhe. Rais na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa imani yao kwangu. Natumia nafasi hii pia kuwashukuru Watanzania wote kwa ushirikiano mkubwa mlionipa wakati wote niliokuwa katika utumishi wa umma. Nawahakikishia kuwa nitaendelea kuwa raia mwema wa Tanzania.”
Itakumbukwa kwamba, Dkt. Nchimbi aliteuliwa kuwa mgombea mwenza kwa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 Agosti 2025. Baadaye jioni, taarifa kutoka Ikulu iliyoandikwa na Dkt. Moses M. Kusiluka. Katibu mkuu kiongozi imesema kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 25 Agosti 2026 amepokea barua ya ombi la kujiuzulu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuanzia tarehe 4 Septemba, 2026. Mheshimiwa Rais ameridhia ombi hilo. Taratibu za Kikatiba za kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano mwingine zinachukuliwa.