Tafuta

2026.07.06 Askofu Mkuu  Inácio Saúre, wa Jimbo Kuu la Nampula na Rais wa Msumbiji(CEM)na Papa Leo XIV. 2026.07.06 Askofu Mkuu Inácio Saúre, wa Jimbo Kuu la Nampula na Rais wa Msumbiji(CEM)na Papa Leo XIV. 

Msumbiji,Maaskofu Wakutana na Papa Leo XIV baaada ya kuuawa kwa Askofu Osório

"Askofu Osório aliuawa kwa sababu alipenda maisha.Yeye ni shahidi wa imani na Kanisa la mashahidi ni Kanisa imara na thabiti."Mwezi mmoja baada ya kuuawa kwa Askofu wa Quelimane,Rais wa Baraza la Maaskofu,Askofu Mkuu Saure,alisimulia mkutano wake na Papa Leo XIV. "Baba Mtakatifu anafuatilia jambo hili kwa karibu na anatoa wito wa mkasa huu kubadilishwa kuwa njia ya matumaini."

Na Padre Bernardo Suate – Vatican.

Mwezi mmoja baada ya kifo cha Askofu Osório Afonso, Askofu wa Jimbo la Quelimane, ambaye aliuawa nyumbani kwake, Rais wa Baraza la  Maaskofu wa Msumbiji (CEM), Askofu Mkuu  Inácio Saure, Makamu Rais, Askofu Mkuu João Carlos, na Askofu Mkuu Mstaafu wa Beira, Askofu Mkuu Claudio Dalla Zuanna, walikutana na Papa Leo XIV na mihimili mingine ya Vatican. Katika mahojiano, Maaskofu waliripoti kwamba Baba Mtakatifu alionesha ukaribu na mshikamano wake si kupitia maandishi yake au taarifa zake za umma tu,  bali pia "kupitia kile tulichokiona wakati wa mkutano na Baba Mtakatifu: tuligundua kwamba anajua vyema ukweli tunaoupata nchini Msumbiji."


Kwa huzuni kubwa na wasiwasi mkubwa

Kanisa nchini Msumbiji limekuwa likipitia tukio hili la kusikitisha kwa huzuni kubwa na wasiwasi mkubwa tangu habari za mauaji hayo zilipoenea asubuhi ya tarehe 6  Juni 2026. Baraza  la Maaskofu pia limemteua Askofu wa Alto Molócuè, Askofu Estevão Ângelo Fernando, kama sehemu ya marejeo ya kufuatilia kwa karibu hali katika Jimbo la Quelimane, kama ilivyoelezwa na Maaskofu katika mahojiano hayo. Hata hivyo, Rais wa Baraza la Maaskofu alielezea masikitiko yake kwamba, hadi leo hii, bado hakuna toleo rasmi la matukio hayo. "Kilichowekwa wazi ni kwamba Askofu aliuawa kwa risasi, sio kwa bastola rahisi, bali kwa silaha kubwa, silaha ya kivita. Baada ya mauaji hayo, chansela wa  Jimbo, mshirika wa karibu wa Askofu, alikamatwa; Padre mwingine,  Celso, alikamatwa naye baadaye, na simu za mkononi za Askofu Osório na Askofu Estevão Ângelo Fernando, msimamizi aliyeteuliwa kuwa Msimamizi wa kitume wa Quelimane, zilishikiliwa."

I vescovi mozambicani con Papa Leone XIV

Maaskofu wa Msumbiji na Papa Leone XIV

Ni muhimu kutoa mwanga kuhusu wahusika, wachochezi, na nia ya uhalifu huo

Kama Askofu Mkuu Inácio Saure alivyosisitiza, jambo zima kwa sasa liko mikononi mwa SERNIC (Huduma ya Kitaifa ya Upelelezi wa Jinai), na "sisi, kama Kanisa, hatujapokea taarifa yoyote rasmi kuhusu kinachoendelea." Kwa hivyo maswali ya msingi hayajajibiwa: Ni nani hasa aliyemuua Askofu Osório, aliyeamuru uhalifu huo, na ni nini kilikuwa chanzo cha mauaji hayo? Maaskofu pia walielekeza umakini kwenye uvumi uliosambaa katika siku za hivi karibuni kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uchunguzi huo, ambao kulingana na uhalifu huo unahusishwa na matatizo ya ndani ndani ya utwala wa Kanisa, kana kwamba ni jambo la kikanisa pekee.


Kwa upande wa Askofu Mkuu João Carlos, Askofu Mkuu wa Maputo, alibainisha kuwa amewahuzunisha sana watu wote, ambao wanaendelea kuuliza "inawezekanaje mchungaji kuuawa nyumbani kwake," huku akisisitiza kwamba kila mtu anatarajia neno la matumaini kutoka kwa Kanisa. Makamu rais wa Baraza la Maaskofu Msumbiji( CEM) pia alibainisha kuwa nchini Msumbiji, mara nyingi hutokea kwamba, wakati uchunguzi bado unaendelea, baadhi ya vyombo vya habari huanza kueneza uvumi na dhana zisizo na msingi, na kuathiri utafutaji wa ukweli usio na lengo na wa amani.

Changamoto za ndani ndani ya Kanisa na uhitaji wa uchunguzi unaoaminika

Kulingana na Askofu wa Msumbiji, kifo cha Askofu Osório pia kimeakisi kuwepo kwa matatizo ya ndani ambayo Kanisa lazima lishughulikie kwa uchunguzi mkubwa wa dhamiri. Miongoni mwa changamoto kuu ni uthabiti kati ya kile kinachotangazwa na kile kinachoishi kiukweli na baadhi ya mapadre na watu waliowekwa wakfu. Maaskofu pia wanaashiria jambo la watu wenye ushawishi wa kifedha wanaounga mkono wagombea upadre kwa kujionesha kama "mababa wa Mungu," hatimaye wakishawishi matendo ya mapadre  wa siku zijazo na, wakati mwingine, hata wale ambao tayari wamewekwa wakfu.

I vescovi mozambicani con Papa Leone XIV

Maaskofu wa Msumbiji na Papa Leone XIV

Changamoto ya Kutafuta Ukweli

Wakipitia historia ya hivi karibuni ya Msumbiji, maaskofu wanakumbuka kwa uchungu kwamba uchunguzi kuhusu mauaji ya wanasiasa mashuhuri, maafisa wa ngazi za juu wa serikali, na waandishi wa habari "karibu haufichui ukweli wote." Ukweli ungefafanua ni nani aliyefanya uhalifu huo, ni nani aliyeuanzisha, na ni jukumu gani la jinai wanalokabiliana nalo wahalifu—sharti muhimu kwa upatanisho wa kweli wa kijamii. Hata hivyo, matumaini hayapaswi kupotea. Kwa Askofu Mkuu Saure, ziara ya Roma ilitumika hasa kuthibitisha kwamba "tunataka kuhisi kuungwa mkono kikweli na Kanisa lote, ili Kanisa lote liweze kutafuta majibu ya kuaminika, kulingana na ukweli, kuhusu jambo hili."

Pale dhambi ilipozidi, neema ilizidi kuongezeka

Katika msiba wa kifo cha Askofu Mkuu Osório, Maaskofu wa Msumbiji tayari wanaona njia ya kufuata, ikiimarishwa hasa na mkutano wao na Kiti Kitakatifu. "Tumegundua kuwa Kiti Kitakatifu, Papa, na washirika wake wote wanaamini kwamba Msumbiji inaweza kukua kutoka katika ukweli huu mchungu," alisema Askofu Mkuu João Carlos wa Maputo. "Pia tunaweza kuelewa vyema jinsi uovu unavyofanya kazi miongoni mwetu na, hasa kwa sababu hii, kujifunza kuuzuia na kuibuka imara kutokana nao."

Monsignor Osório Citora Afonso, vescovo di Quelimane

Askofu Osório Citora Afonso, aliyekuwa askofu wa Quelimane

Urithi wa Askofu Osório

Kwa maaskofu wa Msumbiji, hatua inayofuata itakuwa kushirikisha uzoefu wao jijini  Roma na Baraza zima la Maaskofu, wakiendelea na safari ambayo tayari imefanywa katika kutafuta ukweli, matumaini, upatanisho, na utakaso, ili kuponya jeraha hilo. Hii ni safari ambayo haiwezi kufanywa peke yake, bali pamoja, katika roho ya sinodi, kupitia mipango itakayoendelezwa katika majimbo mbalimbali, hivyo kuendeleza urithi ulioachwa na Askofu Osório: ule wa mchungaji halisi aliyetumia maisha yake kutangaza Injili kwa watu wote wenye mapenzi mema.

Askofu Osório ni shahidi wa imani."

Hatimaye, Askofu Inácio Saure alitangaza kwamba "Askofu Osório aliuawa kwa sababu alipenda maisha. Yeye ni shahidi wa imani, na Kanisa la mashahidi ni Kanisa imara na thabiti. Hivyo, Kanisa nchini Msumbiji linapitia tukio hili: kwa maumivu makubwa, lakini pia kwa matumaini makubwa. Kwa sababu, hatimaye, mauaji ya kishahidi ndiyo yanayoimarisha Kanisa: husababisha mateso, lakini yanalifanya Kanisa kuwa na nguvu zaidi."

Misa baada ya siku 30 za kifo cha Askofu Osorio

Jimbo la Quelimane liliadhimisha  Misa ya Ukumbusho ya siku ya thelathini tangu kifo cha kusikitisha cha Askofu Osório Citora. Misa Takatifu ilifanyika saa kumi na mbili jioni katika Kanisa Kuu la Quelimane ikiongozwa na Msimamizi wa Kitume, Askofu Estevão Ângelo Fernando. Katika ujumbe uliotolewa kupitia Ofisi ya Uratibu wa Kichungaji ya Jimbo, Askofu Fernando aliwaalika waamini wote kushiriki katika misa hiyo ya ukumbusho. Kwa kutambua ukubwa wa Jimbo, pia aliwahimiza Parokia zilizo mbali na Kanisa kuu kujiunga kiroho kwa kuadhimisha Misa hiyo hiyo katika jamuiya zao, na kuwa pamoja kwa sala kwa ukumbusho huu.

Wasiwasi kuhusu uvumi

Maandalizi   yakiendelea pia, Jimbo lilielezea wasiwasi wake kuhusu usambazaji wa ripoti kuhusu hali ya kifo cha Askofu Citora. Tarehe 4 Julai 2026, Jimbo lilitoa "Barua rasmi ya Kukataa," iliyosainiwa na Askofu Fernando na Baraza la Washauri, ikilaani uchapishaji wa taarifa ambazo, kwa maoni yake, zinahatarisha usiri wa uchunguzi unaoendelea. Taarifa hiyo ilikosoa ripoti zinazosambazwa kupitia baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambayo inadaiwa kufichua maelezo ya uchunguzi na kuwasilisha hitimisho kabla ya uchunguzi rasmi kukamilika. Kulingana na Jimbo, uvumi kama huo una hatari ya kushawishi maoni ya umma na kuingilia utawala sahihi wa haki.

Wajibu wa uhuru wa vyombo vya habari

Huku ikithibitisha tena kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari, Jimbo  lilisisitiza kwamba uhuru huu lazima utekelezwe kwa weledo na utaalamu, uwajibikaji wa kimaadili, na heshima kwa mchakato wa kisheria. "Kanisa Katoliki linatetea uhuru wa vyombo vya habari," taarifa hiyo ilibainisha, "lakini linakumbuka kwamba lazima utekelezwe kwa maadili, usahihi na uwajibikaji, bila kujibadilisha na mahakama au kutoa hukumu za umma kabla ya uamuzi halali kisheria." Jimbo pia ilitoa wito kwa mamlaka za umma kuchunguza wale wote wanaovunja usiri ambao huenda ulitokea wakati wa uchunguzi na kuwasihi waandishi wa habari, mashirika ya vyombo vya habari, na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.

Kusubiri haki kwa matumaini

Waamini walipokusanyika kumkumbuka Askofu Osório Citora, Jimbo linaendelea kuhimiza maombi, umoja, na uaminifu katika mchakato wa mahakama. Viongozi wa kanisa wamewataka Wakatoliki kuepukana na uvumi na kuwapa mamlaka za kisheria muda na uhuru unaohitajika kukamilisha kazi yao. Misa ya ukumbusho haikuheshimu tu maisha na huduma ya marehemu Askofu lakini pia ilitumika kama wakati wa mshikamano kwa Kanisa mahalia linapotafuta uponyaji, haki, na amani baada ya msiba mkubwa. Kupitia sala na uvumilivu, Jimbo linatamani kwamba ukweli utaibuka na kwamba haki itatolewa kwa haki na uadilifu.

MAASKOFU MSUMBIJI NA PAPA LEO XIV

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

10 Julai 2026, 10:43