Tafuta

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Wahamiaji Lesvos

Papa ametaja tunu na amali za jamii zinazosigana kiasi kwamba, leo hii Bahari ya Mediterrania imekuwa ni Bahari ya Kifo. Mwaliko wa kujenga na kudumisha Injili ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kuna haja ya kukuza na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na uhuru ili kuvuka mipaka ya hofu na migawanyiko isiyokuwa na mvuto wala mashiko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 4 hadi Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Huu ni ujumbe makini hasa katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 vinavyotishia maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Ugiriki ni nchi ambayo ilitikiswa sana na myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa na inakabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo, changamoto na fursa zinazowakabili wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa sehemu mbalimbali za dunia.

Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 5 Desemba 2021amesafiri kutoka mjini Athene na kuelekea Kisiwani Lesvos kwenye Kambi ya Kuwapokea na Kuwatambua Wakimbizi na Wahamiaji na hapo amepokelewa na viongozi wa Serikali na Kanisa kwenye Uwanja wa Ndege wa Mytilene. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amekazia kuhusu: utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji na kwamba, hii ni changamoto inayopaswa kushughuliwa na wote. Miaka mitano imegota, lakini hali ya wakimbizi na wahamiaji inazidi kuwa mbaya zaidi kila kukicha, kiasi kwamba, haya ni mazingira ambayo hayafai kwa maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu ametaja pia tunu na amali za jamii zinazosigana kiasi kwamba, leo hii Bahari ya Mediterrania imekuwa ni Bahari ya Kifo: “Mare mortuum”, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha Injili ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kukuza na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na uhuru ili kuvuka mipaka ya hofu na migawanyiko isiyokuwa na mvuto wala mashiko. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto inayopaswa kushughuliwa na wote kama yalivyo pia maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwamba, licha ya Jumuiya ya Kimataifa kuchelewa kutekeleza sera na mikakati ya mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini kwa sasa dalili za matumaini zinaanza kujitokeza. Lakini kwa wakimbizi na wahamiaji, changamoto hii imewekwa kando, ingawa maisha ya watu yanawekwa rehani, amani na utulivu viko mashakani. Ni kwa njia ya upatanisho wa kweli na maskini, maendeleo kwa siku za usoni yanaweza kupatikana. Pale maskini wanaposukumizwa pembezoni mwa jamii, amani iko mashakani! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, utashi imara wa kustahi utu wa watu wengine na mataifa mengine, pamoja na uzingativu thabiti wa udugu wa kibinadamu ni vya lazima kabisa katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Rej. GS, 78.

Huu ni wakati wa kuona ukweli kwa macho makavu na kuwajibika kikamilifu bila kuwarushia wengine changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Kinachozingatiwa hapa ni utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi kuwa kama kipimo kwa mambo yote. Miaka mitano imegota tangu viongozi wakuu wa Makanisa walipotembelea Kisiwa cha Lesvos na kujionea hali halisi ya wakimbizi na wahamiaji, lakini hali bado imebaki vile vile kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashuruku wadau wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Kwa hakika nchi ya Ugiriki imeelemewa na wimbi kubwa la wakimbizi na inaonekana kana kwamba, kwa baadhi ya nchi za Ulaya hili si tatizo linalowahusu. Inasikitisha kuona kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanaishi katika mazingira yasiyofaa kabisa na badala yake, serikali zinaomba fedha kwa ajili ya kujenga kuta za nyaya za umeme ili kudhibiti wimbi la wakimbizi.

Ni kweli kabisa kuna watu wameathirika kwa ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa lakini ujenzi wa kuta za umeme si suluhu ya matatizo yanayomkabili manadamu. Jambo la msingi ni kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, utekelezaji wa utawala wa sheria pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu,  heshima na haki msingi za binadamu. Maisha ya mwanadamu yako hatarini, pale ambapo utu na heshima yake vimewekwa rehani. Kuna tunu na amali za kijamii zinazosigana na kukinzana mintarafu jamii, ulinzi na usalama, mshikamano na udugu wa kibinadamu; vipaumbele vya jamii mahalia na vipaumbele vya kimataifa. Jambo la msingi ni kuangalia ukweli wa mambo kwa kusoma alama za nyakati. Vifo vya watoto waliofariki dunia kwenye ufuko wa Bahari ya Mediterrania, iwe ni changamoto kwamba, Bahari ya Mediterrania imegeukwa kuwa “Bahari ya Kifo, Mare mortuum”. Badala ya kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni uwanja wa vita na utamaduni uliojeruhiwa badala ya kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu. Fumbo la Umwilisho liwe ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kukuza moyo wa upendo na ukarimu, ili hatimaye, kuwa ni Wasamaria wema, katika huduma ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Huduma ya Mama Kanisa inapaswa kuwepo mahali ambapo kuna mateso na mahangaiko ya binadamu, kwa kuangalia kwa macho ya moyo. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wanawake wajawazito aliokumbana na kifo, huku wakiwa wamebeba mimba ya vichanga wao. Bikira Maria Mama wa Mungu awasaidie watu kuona na kuthamini utu na heshima ya binadamu, tayari kuwaendea na kukutana na wote wanaoteseka. Mara baada ya hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Sala ya Malaika wa Bwana Kisiwani Lesvos.

Wahamiaji Lesvos
05 December 2021, 16:52

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >