Tafuta

Kipindi cha Majilio: Kesheni Bwana Anakuja: Kiini cha Matumaini

Ujumbe: “Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu” huu ndio msingi wa matumaini ya Kikristo wakati wote. Jambo la msingi kwa waamini ni kutambua jinsi ambavyo Kristo Yesu atakavyokuja kuwahukumu wazima na wafu na jinsi ya kumtambua na hatimaye, kumpokea atakapokuja. Amkeni uzingizini, vaeni silaha za mwanga: haki, ukweli, amani na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Majilio ni kipindi cha upendo, matumaini, furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. “Kwa kuadhimisha kila mwaka liturujia ya majilio, Kanisa linahuisha kule kumngojea Masiha, likijiweka katika ushirika wa maandalizi marefu ya ujio wa kwanza wa mwokozi, waamini wakiamsha upya tamaa ya ujio wake wa pili.” (KKK 524). Dominika tarehe 27 Novemba 2022, Mama Kanisa ameanza Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa, kama sehemu ya Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga angavu na uwepo wake unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Mama Kanisa huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima, anapolikunjua Fumbo la Kristo Yesu, tangu Fumbo la Umwilisho na Pasaka hadi kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana Yesu, kuwahukumu wazima na wafu. Na kwa njia hii, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111.

Kipindi cha Majilio: Basi kesheni, Bwana anakuja: kiini cha matumaini
Kipindi cha Majilio: Basi kesheni, Bwana anakuja: kiini cha matumaini

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa anasema, huu ndio ujumbe makini: “Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu” huu ndio msingi wa matumaini ya Kikristo wakati wa raha, shida na mahangaiko mbalimbali ya maisha. Jambo la msingi kwa waamini ni kutambua jinsi ambavyo Kristo Yesu atakavyokuja kuwahukumu wazima na wafu na jinsi ya kumtambua na hatimaye, kumpokea atakapokuja. Huu ni wakati wa kuamka katika usingizi na kuzivaa silaha za mwanga. Waamini wamezoea kusikia kwamba, Kristo Yesu yuko, anatembea na kuzungumza pamoja na waja wake. Lakini kwa bahati mbaya, waamini wengi hawatambua uwepo wake, wengine wanataka kuona miujiza na matendo makuu, kama ishara ya uwepo wake kati pamoja na waja wake. Lakini Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake akisema, “Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.” Mt 24: 37-44.

Majilio ni kipindi cha imani, matumaini, mapendo na amani
Majilio ni kipindi cha imani, matumaini, mapendo na amani

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kristo Yesu kila siku anakuja katika uhalisia wa maisha ya waja wake, katika hali ya kawaida pasi na makuu, katika furaha, huzuni na majonzi, Kristo Yesu anawaita, anazungumza na kuwaongoza katika matendo mema. Ili kuweza kumtambua Kristo Yesu anapokuja kwa waja wake, kuna umuhimu wa kukesha na kuwa makini, ili asijewakuta hawajajiandaa bado. Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliwahi kusema, “ninaogopa sana Kristo Yesu akapita bila ya kumtambua” kama ilivyokuwa watu wa nyakati za Nuhu kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue. Kwa wale waliokuwa makini wakikesha, waliweza kutambua uwepo wa Kristo Yesu kati yao. Kumbe, Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa kuamka. Huu ni wakati wa kuamka katika usingizi na kuzivaa silaha za mwanga., kwa kuwa makini na kuendelea kukesha bila kuchoka, hadi atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Bikira Maria Mama wa Majilio aliyetambua Ujio wa Mungu katika hali ya unyenyekevu, akauficha Umungu wake katika maisha Kijijini Nazareti na kumpokea tumboni mwake, kama Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja waje awasaidie wao pia kujiandaa vyema kumtambua na kumpokea ajapo!

Papa Majilio
27 November 2022, 15:06

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >