Tafuta

Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu: Hukumu ya Mwisho: Matendo ya Huruma

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 26 Novemba 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amegusia kuhusu hukumu ya mwisho na kwamba, kipimo ni matendo ya huruma, yaani upendo; Marafiki wa kweli wa Kristo Yesu ni wale waliojipambanua kwa huduma kwa maskini na kwamba, upendo umwilishwe katika huduma. Tafakari imesomwa na Monsinyo Paolo Luca Braida.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika tarehe 26 Novemba 2023 Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo; yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12. Huu ni: Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu anasema chimbuko la matumaini ya Kikristo linabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka; Mashuhuda wa matumaini; Matumaini yanayong’ara katikati ya usiku wa giza; Umuhimu wa kukoleza matumaini kwa kuwasha mwenge wa matumaini. Hii ni Sherehe inayokazia matendo ya huruma kiroho na kimwili ambayo kimsingi ni: Ushauri kwa wenye shaka, kuwafundisha wajinga, kuwaonya wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuvumilia wasumbufu pamoja na kuwaombea walio hai na wafu na kwamba, hii ni fursa ya kuwa karibu na wale wanaojisikia kuwa mbali na Kanisa au kusukumizwa pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa! Matendo ya huruma kimwili ni: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu; kuwavika walio uchi; kuwakaribisha wasiokuwa na makazi; kuwatembelea wagonjwa; kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu! Matendo ya huruma kimwili ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa tangu mwanzo. Hii ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Waamini wakifuatilia Sala ya Malaika wa Bwana
Waamini wakifuatilia Sala ya Malaika wa Bwana

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 26 Novemba 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amegusia kuhusu hukumu ya mwisho na kwamba, kipimo ni matendo ya huruma, yaani upendo; Marafiki wa kweli wa Kristo Yesu ni wale waliojipambanua kwa huduma kwa maskini na kwamba, upendo umwilishwe katika huduma. Mwinjili Mathayo anaweka mbele ya macho ya waamini siku ile ya hukumu ya mwisho, Mataifa yote yatakusanyika mbele zake na hapo wale marafiki wa Mfalme watajipambanua kwa matendo yao ya huruma yaliyomwilishwa katika upendo. Baba Mtakatifu Francisko kutokana na changamoto ya afya, tafakari yake imesomwa na Monsinyo Paolo Luca Braida, Kiongozi mkuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican.

Hukumu ya Mwisho: Matendo ya huruma: kiroho na kimwili
Hukumu ya Mwisho: Matendo ya huruma: kiroho na kimwili

Baba Mtakatifu Francisko anasema, marafiki hawa si wale waliomsaidia Mfalme kuteka na kutwaa maeneo, kushinda vita au kuonekana mkuu kati ya watawala wa ulimwengu huu, waliomsaidia kuwa mtu tajiri na maarufu kadiri ya vigezo vya dunia. Lakini marafiki wa kweli wa Mfalme ni wale ambao Mfalme mwenyewe anawatambua kuwa ni maskini na kujitambulisha pamoja nao kama mwenye njaa, mwenye kiu, mgeni, uchi, mgonjwa na kifungoni. Kadiri walivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zake walio wadogo walimtendea Kristo Yesu. Rej. Mt 25: 40. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa hakika Mfalme yuko makini na matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo: yaani baa la njaa linavyopekenya utu, heshima na haki zake msingi; Ukosefu wa makazi bora, magonjwa na wafungwa magerezani. Watu wasiokuwa na makazi maalum wamo mitaani na wanakutana na waamini kila kukicha. Kuhusu magonjwa na kufungwa gerezani ni mambo yanayofahamika vyema.

Monsinyo Paolo Luca Braida amesoma tafakari ya Malaika wa Bwana
Monsinyo Paolo Luca Braida amesoma tafakari ya Malaika wa Bwana

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wamebarikiwa wale wote wanaomwilisha matendo ya huruma katika huduma ya upendo, kwa kuwapatia maskini chakula pamoja na kuwanywesha; kwa kuwavika, kwa kuwakarimia, kwa kuwatembelea na kuwa majirani wema. Mahali penye mateso na mahangaiko panahitaji msaada na kwamba, huduma ya mapendo ndiyo utambulisho wa marafiki wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika: Ukaribu, huruma na upole mambo msingi yanayoganga na kutibu madonda ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa tafakari yake amewakumbusha waamini kwamba, Ufalme wa Kristo unafumbatwa katika huruma, nguvu yake ya kutawala iko katika upendo. Je, waamini wanajisikia kuwa ni marafiki zake Kristo Yesu? Lakini wanaweza kuwa kweli ni marafiki wa Kristo Yesu ikiwa kama watatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Bikira Maria Malkia wa mbingu na nchi awasaidie waamini kumpenda zaidi Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu pamoja na kuwapenda maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Yesu Mfalme wa Ulimwengu

 

26 November 2023, 14:02

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >