Tafuta

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Sakramenti ya Ubatizo: Mlango wa Imani

Tukio la Ubatizo wa Bwana ni ufunuo wa Kristo Yesu kuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu na ni Masiha. Hili ni tukio linalozungumzia pia kuhusu Sakramenti ya Ubatizo, unaowafanya wabatizwa kuwa ni watoto wateule wa Mungu. Kwa njia hii watu wa Mungu wanakirimiwa maisha na uzima wa milele; ni tukio la neema na ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, linalowakirimia watoto wa Mungu upendo unaookoa, mwaliko ni kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, mwanzo wa maisha ya Yesu ya hadhara ni kubatizwa kwake na Yohane Mbatizaji katika mto Yordane. Yohane alihubiri ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi na kundi kubwa la watu walimwendea ili kuweza kubatizwa naye. Na Kristo Yesu anatokea, Yohane Mbatizaji anasita, lakini Kristo Yesu anasisitiza na hatimaye, anabatizwa. Na Roho Mtakatifu anaonekana juu ya Kristo Yesu kama hua na sauti kutoka mbinguni ikisema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu”. Hili ni tukio la ufunuo wa Kristo Yesu kama Mwana wa Mungu na Masiha. Ubatizo ni kielelezo cha Mtumishi anayeteseka. Anakubali ahesabike miongoni mwa wenye dhambi, lakini Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayechukua dhambi ya ulimwengu! Anatanguliza Ubatizo wa kifo cha kumwanga damu, tayari kutimiza haki yote. Mt. 3:15. Ubatizo ni kielelezo cha utii kwa Baba yake wa mbinguni anayependezwa naye na Roho Mtakatifu anakuwa na kubaki juu yake. Kwa Ubatizo wake mbingu zilifunguka na maji kutakaswa kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyeshuka na kukaa juu yake na huo unakuwa ni mwanzo wa uumbaji mpya. Kwa Sakramenti ya Ubatizo, Kristo Yesu anamwingiza Mkristo ndani yake Yeye, ambaye, kwa ubatizo wake, anatanguliza kifo na ufufuko wake. Mkristo anapaswa kuingia katika fumbo hili la unyenyekevu na toba, ashuke katika maji pamoja na Kristo Yesu, ili apande pamoja naye, azaliwe kwa maji na kwa Roho Mtakatifu, ili hatimaye awe ndani ya Mwana, mwana mpendwa wa Baba na kutembea katika maisha mapya. Kwa maneno mengine ni kufa, kuzikwa na kufufuka pamoja na Kristo Yesu! Rej. KKK 535-537.

Ubatizo ni mwanzo wa safari ya utakatifu wa maisha
Ubatizo ni mwanzo wa safari ya utakatifu wa maisha

Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa Dominika tarehe 7 Januari 2024 anaadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana uliofanywa na Yohane Mbatizaji pale Mto Yordani: “Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohane katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Mk 1: 7-11. Yohane Mbatizaji anamtambua Kristo Yesu kwa kusema: “Aliye na nguvu kuliko mimi, Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu, mbingu zikapasuka na sauti ikatoka ikisema, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Tukio la Ubatizo wa Bwana ni ufunuo wa Kristo Yesu kuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu na ni Masiha. Hili ni tukio linalozungumzia pia kuhusu Sakramenti ya Ubatizo, unaowafanya wabatizwa kuwa ni watoto wateule wa Mungu. Kwa njia hii watu wa Mungu wanakirimiwa zawadi ya maisha mapya na uzima wa milele. Hili ni tukio la neema na ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, linalowakirimia watoto wa Mungu upendo unaookoa.

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe tarehe 7 Januari 2024, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana. Anasema: Tunda la Ubatizo, au neema ya Ubatizo ni ukweli wenye utajiri unaojumuisha msamaha wa dhambi ya asili na dhambi zote za binafsi, kuzaliwa katika maisha mapya ambayo kwayo mtu hufanywa mwana wa Baba wa milele, kiungo cha Kristo, hekalu la Roho Mtakatifu. Kwa ukweli huo huo mbatizwa huingizwa katika Kanisa, Mwili wa Kristo na hufanywa mshiriki wa ukuhani wa Kristo Yesu. Rej. KKK 1279. Kwa njia hii Mwenyezi Mungu anafanya maskani nyoyoni mwa waja wake. Kumbe, Ubatizo ni zawadi ya maisha mapya inayomfanya Mbatizwa kuwa ni mwana mpendwa wa Mungu kwa daima. Ndiyo maana anasema Baba Mtakatifu Francisko waamini wanapaswa kukumbuka siku ya ubatizo wao na kufanya sikukuu. Anawahimiza waamini kujibidiisha kuifahamu tarehe ya Ubatizo wao, kwani tangu siku ile ya Ubatizo, Mwenyezi Mungu ameamua kufanya maskani yake ndani mwao. Huu ni mwaliko wa kuwashukuru wazazi na walezi waliowasindikiza hadi kwenye Kisima cha Ubatizo; kwa wahudumu wa Sakramenti ya Ubatizo bila kuwasahau wasimamizi wa Ubatizo pamoja na jumuiya ya waamini iliyowapokea na kuwalea. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama wanatambua zawadi kubwa ya Sakramenti ya Ubatizo waliyopokea? Je, wanatambua katika maisha yao mwanga angavu wa uwepo wa Mungu ambaye anawaangalia kama watoto wake wapendwa? Waamini wanaweza kufanya kumbukumbu hii kwa Ishala ya Msalaba inayoacha chapa ya kudumu ya neema ya Mungu katika maisha yao, Mungu anayewapenda upeo na anatamani kukaa pamoja nao daima! Bikira Maria, Hekalu la Roho Mtakatifu, awasaidie waamini kuadhimisha na kupokea matendo makuu ya Mungu yanayotendeka katika maisha yao!

Ubatizo wa Bwana
07 January 2024, 13:58

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >