Papa kwa wahanga wa kimbunga huko Asia.Novemba 1 Newman atatangazwa kuwa Mwalimu wa Kanisa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Misa Takatifu, na kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 28 Septemba 2028, Baba Mtakatifu aliyeadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya Jubilei ya Makatekista kutoka Ulimwenguni kote, alisema, “Ninatoa salamu zangu za dhati kwenu nyote mlioshiriki katika maadhimisho ya Jubilei hii maalumu kwa makatekista, hasa wale mliowekwa wakfu leo hii kwa ajili ya huduma hii. Na pamoja nanyi, ningependa kutoa matashi yangu moto moto kwa ajili ya huduma njema kwa makatekista katika Kanisa kote ulimwenguni.” Papa aliongeza kusema “Asante kwa huduma yenu kwa Kanisa! Na tuwaombee hasa wale wanaofanya kazi katika mazingira magumu sana. Mungu awabariki nyote!”
Salamu kwa mahujaji
Papa kisha aliwasalimia “mahujaji wa Jimbo la Vicenza pamoja na Askofu wao na vikundi vingine vya waamini kutoka nchi mbalimbali. “
Maafa ya asili barani Asia
Mawazo ya Baba Mtakatifu aidha aligeukia picha nyingine ya maafa ya asili duniani na kwamba “Katika siku za hivi karibuni, kimbunga kikali sana kimepiga maeneo kadhaa ya Asia, hasa Ufilipino, kisiwa cha Taiwan, jiji la Hong Kong, mkoa wa Guangdong, na Vietnam. Niko karibu na watu walioathiriwa, hasa maskini zaidi, na ninawaombea waathiriwa, waliopotea, familia nyingi zilizohamishwa, watu wengi ambao wameteseka, na pia kwa waokoaji na mamlaka ya kiraia.” Papa aliomba msada kwa ajili yao na kusema kuwa “ Ninawaalika watu wote kumwamini Mungu na kuonesha mshikamano. Mungu atupe nguvu na ujasiri wa kushinda kila dhiki.”
Kardinali Newman kuwa Mwalimu wa Kanisa
Papa alisema:“Nina furaha kutangaza kwamba mnamo tarehe 1 Novemba, katika muktadha wa Jubilei ya Ulimwengu wa Elimu, nitamkabidhi Mtakatifu John Henry Newman dhamana ya Mwalimu wa Kanisa, ambaye walichangia kwa dhati katika kufanywa upya kwa Taalimungu na kuelewa mafundisho ya Kikristo katika maendeleo yake yote.”
Ikumbukwe hivi karibuni, Papa Leo XIV, tarehe 31 Julai 2025 alilidhia maoni ya Kikao cha Mkutano Mkuu wa Makardinali, Maaskofu na Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu kuhusu Jina la kupewa Mwalimu wa Kanisa la Ulimwengu ambapo Kardinali Newman atapewe hivi karibuni. Na tarehe ilikuwa bado haijapangwa na hatimaye Papa Leo XIV ameitangaza!
Maombezi ya Bikira Maria
Kwa kuhitimisha alisema “Na sasa tunajikabidhi kwa maombezi ya Bikira Maria. Yeye, ambaye alikuwa mama na mfuasi wa kwanza wa Yesu, aimarishe dhamana ya Kanisa katika kutangaza imani leo.”
