Papa Leo XIV: Tafakari Jumatatu ya Oktava ya Pasaka: Mashuhuda wa Imani

Baba Mtakatifu Leo XIV nasema, leo waamini wanatakiwa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuchagua simulizi la wale wanawake waliokutana na Kristo Mfufuka wakatangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya kifo; kaburi wazi ni chemchemi ya maisha mapya na kwamba, kifo kimeshindwa au simulizi lililotolewa na wale Askari waliopewa fedha nyingi wakaambiwa waseme ya kwamba, “Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba.” Mt 28: 12-13.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 6 Aprili 2026 Mama Kanisa ameadhimisha Jumatatu ya Oktava ya Pasaka. Hii pia ni Siku ya Malaika, kwani ni ile Siku ambayo Malaika alikutana na wale wanawake waliokwenda kaburini alfajiri na mapema, siku ya kwanza ya juma. Walipotazama waliona kuwa lile jiwe limekwisha kuviringishwa, wakaingia, wakamwona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe. “Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.” Mk 16:6-7. Kwa hakika wanawake hawa walikuwa na furaha kubwa isiyokuwa na kifani kuhusu Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, kiasi cha kuondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari.

Waamini ni mashuhuda wa imani katika Ufufuko wa Yesu
Waamini ni mashuhuda wa imani katika Ufufuko wa Yesu   (@Vatican Media)

Hii ndiyo furaha inayobubujika kutoka moyoni mwa mwamini baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka na hiyo inakuwa ni changamoto ya kutoka mbio kwenda kutangaza na kushuhudia kile walichoshuhudia kwa macho yao. Wale Mitume waliokuwa wamegubikwa kwa woga, hofu na wasiwasi wanageuka kuwa ni mashujaa na jasiri; watu waliosimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; wanageuka kuwa ni mashuhuda wa matumaini dhidi ya habari za kughushi. Huu ni mwanzo wa siku mpya ambayo Kristo Mfufuka amewatayarishia waja wake na kwamba, Liturujua ya Neno la Mungu inashangilia kuingizwa kwa kazi nzima ya uumbaji katika mpango wa ukombozi na kwamba, kwa njia ya Jina Takatifu la Kristo Yesu, hali ya kukata tamaa imeondolewa.

Sala ya Malkia wa Mbingu: Kipindi cha Pasaka
Sala ya Malkia wa Mbingu: Kipindi cha Pasaka   (ANSA)

Hii ni sehemu ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican, Jumatatu, Oktava ya Pasaka, tarehe 6 Aprili 2026. Anasema, leo waamini wanatakiwa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuchagua simulizi la wale wanawake waliokutana na Kristo Mfufuka wakatangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya kifo; kaburi wazi ni chemchemi ya maisha mapya na kwamba, kifo kimeshindwa au simulizi lililotolewa na wale Askari waliopewa fedha nyingi wakaambiwa waseme ya kwamba, “Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba.” Mt 28: 12-13.

Papa Leo XIV Akiongoza Sala ya Malkia wa Mbingu
Papa Leo XIV Akiongoza Sala ya Malkia wa Mbingu   (@Vatican Media)

Katika simulizi la Askari ukweli unafunikwa na habari za kughushi “fake news” yaani hizi ni habari za uwongo, uzushi, na shutuma zisizo na msingi. Licha ya vikwazo vyote hivi, ukweli unaendelea kuonekana na wala haubaki tena kuwa ni siri na hivyo kufukuzilia mbali giza lililokuwa linaufunika ukweli. Kristo anapenda kuwaambia waja wake hata leo hii: “Msiogope; nendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.” Mt 28:10. Kristo Yesu mwenyewe anakuwa ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa Ulimwenguni kote. Pasaka ya Bwana ni Pasaka ya waamini na binadamu kwa sababu Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni Mwana wa Mungu ambaye aliyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa binadamu na ndivyo anavyoweka huru yaliyopita kutoka kwenye mwisho wa uharibifu na vivyo hivyo ujumbe wa Pasaka unakomboa maisha ya baadaye ya mwanadamu kutoka kaburini.

Furaha ya waamini kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao
Furaha ya waamini kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao   (Vatican Media)

Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashuhudia na kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia: Injili iwafikie hasa watu wanaoendelea kuteseka kwa vita; wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanaoteseka, kudhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; watoto wanaokosa fursa za elimu na matibabu. Kwa kutangaza na kushuhudia kwa maneno na matendo ujumbe wa Pasaka ya Bwana maana yake ni kutoa sauti ya matumaini, inayowezwa kusiginwa mikononi mwa watesi wao! Daima Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa na kushuhudiwa inaendelea kuondoa “mawingu ya nyakati zote.”

Malkia wa Mbingu 2026
06 Aprili 2026, 15:15

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >