Tafuta

Papa Leo XIV Masharti ya Kumfuasa Kristo Yesu: Kujitenga, Kupoteza na Ukarimu

Papa Leo XIV: Masharti ya kumfuas Yesu ili kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: Kweli na uzima, huu ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Huu ni mwaliko kwa waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujenga na kudumisha upendo, unaoweza kuzaa matunda na kwamba, upendo huu unahitaji kuzingatia mambo makuu matatu: kujitenga, kupoteza, mambo yanayosimikwa katika ukarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1829.

Fadhila Kuu: Busara, Haki, Nguvu na Kiasi
Fadhila Kuu: Busara, Haki, Nguvu na Kiasi   (@Vatican Media)

Kuna fadhila tatu za Kimungu zinaweka msingi, zinahuisha, na kuainisha utendaji: imani, matumaini na mapendo. “Fadhila za kibinadamu zinapatikana kwa njia ya malezi, matendo ya makusudi, udumifu kwa njia za juhudi zinazorudiwa-rudiwa. Nazo zahuishwa, zatakaswa na kuinuliwa na neema ya Mungu, kuunda tabia na kurahisisha kutenda mema. Hizi ni amana ya uwepo na tendo la Roho Mtakatifu katika nguvu ya binadamu. Rej. KKK 1812-1829. Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake Dominika tarehe 28 Juni 2026 anasema, Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 13 ya Mwaka A wa Kanisa inaweka mbele ya macho ya waamini masharti muhimu ya kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na hivyo kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: Kweli na uzima, huu ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Huu ni mwaliko kwa waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujenga na kudumisha upendo, unaoweza kuzaa matunda na kwamba, upendo huu unahitaji kwa mwamini kujikana nafsi na kuendelea kumfuasa Kristo Yesu kwa kuzingatia mambo makuu matatu: kujitenga, kupoteza, mambo yanayosimikwa katika ukarimu.

Masharti ya Kumfuasa Kristo Yesu: Kujitenga, Kupoteza na Ukarimu
Masharti ya Kumfuasa Kristo Yesu: Kujitenga, Kupoteza na Ukarimu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kujitenga: “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.” Mt 10:37-39. Kabla ya Kristo Yesu kuwatuma wafuasi wake kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu anawataka kwanza kabisa kujitenga na uhusiano unaoweza kuwakwamisha kiasi cha kushindwa kufikia utimilifu wa upendo, unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Kwa wanandoa wanaweza kuishi kwa amani na utulivu wanapojitenga na familia zao za asili, ili kujenga na kudumisha uhusiano wa ndoa na ujenzi wa familia, lengo ni kuwafanya waamini kukomaa na hatimaye, kuwa ni watu wenye furaha ya kweli, tayari kutembea kwa miguu yao wenyewe, tayari kupandikiza mbegu itakayotoa matunda ajaa kama anavyosema Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa.

Kujitenga ni muhimu sana kama sehemu ya sharti la kumfuasa Yesu.
Kujitenga ni muhimu sana kama sehemu ya sharti la kumfuasa Yesu.   (@Vatican Media)

Kwa maneno mengine Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo ni kama kupoteza na kwamba, upendo wa kweli unaweza kuzaa matunda, ikiwa tu upendo huu utakuwa ni sadaka, kwa kutoa nafasi kwa wengine, kwa kutoa muda, ili kumsikiliza jirani yako; ni mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kusaidia kuleta faraja, amani na utulivu katika madhira yanayomsibu binadamu; kunahitaji upendo wa dhati na mbinu madhubuti kama vile kusikiliza bila kuhukumu, kutoa msaada kwa vitendo, na kujenga matumaini. Mambo haya ni madogo lakini huleta mabadiliko makubwa katika ustawi wa jamii na utu wa mtu aliyelemewa na shida na hivyo inakuwa ni chemchemi ya upendo unaoweza kuzaa furaha. Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuukumbatia na kuambata Msalaba, kielelezo cha juu kabisa cha sadaka; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Kwa njia hii, mwamini anapojisadaka bila ya kujibakiza anakuwa chemchemi ya maisha mapya katika uhusiano na jirani zake.

Upendo umwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu.
Upendo umwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu.   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, upendo unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku, kama kumpatia mtu mwenye kiu kikombe cha maji baridi. Kristo Yesu anawaalika na kuwatuma wafuasi wake kuonesha uhitaji, ili kuibua fadhila ya ukarimu kwa wale watakaokutana nao katika maisha na utume wao na Kristo Yesu mwenyewe anasema: “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.” Mt 10:40. Upendo wa Kristo daima unamwilishwa katika ukarimu kwa jirani. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kumwomba Bikira Maria aliyempenda Mwanaye wa pekee, akafahamu hata namna ya “kumpoteza” awasaidie waamini ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wanyenyekevu na wenye furaha ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Papa Leo XIV Ukarimu

 

28 Juni 2026, 14:25

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >