Papa Leo XIV: Mfano wa Mpanzi: Mbegu Ni Neno la Mungu! Ardhi Ni Nyoyo za Waamini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa na hasa Injili ya Mathayo 13:1-23 inazungumzia kuhusu Injili ya Mpanzi, juu ya mwenendo wa Neno la Mungu na athari zake katika maisha ya mwamini, hili Neno ambalo Mwenyezi Mungu amelitupa katika udongo wa maisha ya mwamini kwa imani na ukarimu mkubwa. Udongo unawakilisha: Moyo wa mwamini, ni ulimwengu, ni jumuiya na Kanisa kama kusanyiko la watu wa Mungu. Ni Neno linalovutia na kugusa hisia za wasikilizaji wake; hii ni mbegu ya huruma, upendo, imani na matumaini thabiti. Ni mbegu ambayo Mwenyezi Mungu anaipandikiza katika hali mbalimbali za maisha ya mwanadamu, ili kwa wakati wake iweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mbegu ya Neno la Mungu ina nguvu ya ajabu!
Hii ni sehemu ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa iliyofanywa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, akasadaka maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu; ni mbegu kutoka kwa Baba wa milele inayoendelea kupandikizwa sehemu mbalimbali za dunia, ni chembe ya ngano, ambayo ikifa, hutoa mazao mengi. Rej. Yn 12:24. Lakini mbegu hii, wakati mwingi inakumbana na “kisiki cha mpingo”, ardhi kavu, isiyokuwa na rutuba; wakati mwingine inakumbana na udongo wenye mawe, miamba na miiba. Lakini mbegu ya Neno la Mungu wakati mwingine inaangukia kwenye udongo mzuri na hapo muujiza wa huruma na upendo, uweza kumwilishwa katika maisha ya waamini. Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma, kamwe hakosi kupandikiza mbegu ya Neno lake kwa sababu anatambua fika kwamba, hili ni Neno lenye nguvu. Rej. 2K 12:9-10.
Baba Mtakatifu Leo XIV akifanya rejea kuhusu "mbegu" ya Neno la Mungu, anasema: Mtakatifu Yohane Chrysostom anauliza: "Je, hili linaweza kuwa ni jambo la busara kupanda mbegu kati ya miiba, kwenye ardhi yenye miamba, au barabarani? Kwa upande wa mbegu na udongo wa kawaida, jambo hilo halingekuwa la busara; lakini kwa upande wa roho za watu na mafundisho, ni jambo la kusifiwa kabisa kwa sababu mikononi mwa Mwenyezi Mungu inawezekana kabisa kwamba "ardhi yenye miamba ikabadilishwa na kuwa udongo wenye rutuba; kwamba njia isikanyagwe tena au kuachwa wazi kwa kila mpita-njia, ili hatimaye iwe ardhi yenye rutuba; kwamba miiba iondolewe na mbegu ipate usalama kamili. Hii inaonesha kwamba, ukarimu wa Mungu umesimikwa katika hekima na busara, yeye anaona ndani ya kila moyo wa mwanadamu fursa ya wema, ambao wakati mwingine, mwamini mwenyewe hawezi kuutambua. Kumbe, Mwenyezi Mungu anafahamu fika aina ya udongo wa mioyo ya waamini wake, kamwe haachi kuwaamini na kuwathamini kwa jinsi walivyo; ili wawweze kukua na ukomavu wao siku kwa siku, ikiwa kama watajiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa imani.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ni katika ukarimu na imani; unyenyekevu na utayari wa moyo ambavyo mbegu hiyo hupokelewa navyo na hivyo matunda ya Roho Mtakatifu hukua ndani ya waamini na kuenea. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anafundisha kuwa matunda hayo: Ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Gal 5: 22-23. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuazimia katika kipindi hiki cha Likizo ya Kiangazi, kutenga nafasi ya kusikiliza, kusoma, na kulitafakari Neno la Mungu. Hiki ni kipindi cha mapumziko na burudani; lakini pia ni nyakati zenye maana sana, ikiwa kama waamini watatunza ukimya na kujikita katika sala, ili hatimaye, likizo itakapomalizika waweze kurejea tena katika shughuli zao za kila siku, huku wakiwa wamepyaishwa kiroho na kimwili, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, huku wakiwa na uwezo zaidi wa kuchangia katika ujenzi na ukuaji wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria Malkia wa Mitume na Nyota ya Uinjilishaji, awasaidie katika kutekeleza mambo hayo msingi katika maisha na utume wa Kanisa.