Papa Leo XIV: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Kristo Yesu Tumaini Letu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Kristo Yesu baada ya kusema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka kama zinavyoshuhudia hali mpya na za kimungu ambazo tokea hapo umebaki nazo daima. Lakini kile kipindi cha siku arobaini ambako alizoea kula na kunywa pamoja na wafuasi wake, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa mbinguni, utukufu wake bado ulifunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Tokeo la mwisho la Yesu linakamilika na kuingia bila kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu uliojionesha katika sura ya wingu na mbingu (Lk 24:51) ambako tangu hapo ameketi kuume kwa Mungu. Kwa namna moja tofauti kabisa na ya pekee atajionesha kwa Paulo “kama mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake” katika tokeo la mwisho lililomfanya kuwa Mtume. Hali iliyofunikwa ya utukufu wa Kristo Mfufuka kipindi hiki inaonekana katika maneno yake ya fumbo kwa Mariamu Magdalena: “Sijapata kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu.” Yn 20:17 Hii inaonesha tofauti ya kujidhihirisha kati ya utukufu wa Kristo Mfufuka na ule wa Kristo aliyetukuzwa kuume kwa Baba. Tukio ambalo kwa upande mmoja ni la kihistoria na bora sana linaloonesha kupita toka upande mmoja kwenda upande mwingine. Lakini yote yanabaki yakiwa yameungana kabisa na lile la kwanza yaani kushuka kutoka mbinguni kulikotekelezwa katika Fumbo la Umwilisho. Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba wa milele. Kristo Yesu peke yake ameweza kumfungulia mwanadamu njia hii “ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu na kwamba, akiisha inuliwa juu ya nchi atawavuta wote kwake.” Huku ni kuinuliwa juu ya Msalaba ambako huonesha na kutangaza kuinuliwa kwa kupaa mbinguni. Huo ndio mwanzo wake.
Huko mbinguni Kristo Yesu anatekeleza Ukuhani wake daima, Yeye ni kiini na mtendaji mkuu wa Liturujia inayomheshimu Baba wa mbinguni. Kristo Yesu ameketi kuume kwa Baba, maana yake: ameketi katika utukufu na heshima ya Kimungu, ambaye Yeye aliyekuwako kama Mwana wa Mungu kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili, baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa. Kuanzia hapo Mitume wamekuwa ni mashuhuda wa Ufalme usiokuwa na mwisho. Kupaa kwa Kristo Yesu mbinguni ni alama Dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya Mungu, ambako toka huko atarudi Rej. Mdo 1:11, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu Rej. Kol 3:3. Kristo Yesu kichwa cha Kanisa, anatutangulia katika Ufalme mtukufu wa Baba ili nasi, viungo vya huo mwili, tuishi katika tumaini la kuwa siku moja pamoja naye milele. Kristo Yesu akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya hekalu la mbingu, anasali daima kwa ajili yetu kama mshenga anayetuhakikishia kumiminwa kwa daima Roho Mtakatifu. Rej. KKK 659-667.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Dominika tarehe 17 Mei 2026, wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia mintarafu matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika kukuza na kudumisha mawasiliano yanayoheshimu, kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu na ukweli kanuni elekezi ya kila uvumbuzi wa kiteknolojia unaofanywa na mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, uvumbuzi wa teknolojia, hasa matumizi ya teknolojia ya akili unde, inamhudumia binadamu badala ya kuchukua nafasi au kupunguza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, nyuso na sauti za binadamu ni za kipekee, sifa bainifu za kila mtu; zinafichua utambulisho wa mtu mwenyewe usioweza kurudiwa na ni vipengele vinavyobainisha vya kila kukutana na wengine.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Dominika tarehe 17 Mei 2026 Maandiko Matakatifu yanaonesha kwamba, Kristo Mfufuka alipaa kwenda mbinguni, hali ambayo inaweza kuwafanya waamini kudhani kwamba, hili ni tukio ambalo liko mbali sana na maisha yao. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, waamini wameunganishwa na Kristo Yesu kama viungo vya kichwa, katika mwili mmoja na hivyo kupaa kwake mbinguni kunawavuta waamini ili kuelekea kwenye ushirika kamili na Baba wa milele. Mtakatifu Augustino anasema ukweli kwamba, Kristo Yesu amewatangulia mbele, hili tumaini la kuweza kushiriki. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, maisha yote ya Kristo Yesu ni harakati ya kupaa, kukumbatia na kuhusisha, kwa njia ya ubinadamu wake, ulimwengu mzima umeweza kuinuliwa na ubinadamu kukombolewa kutoka katika hali yake ya dhambi, na hivyo kupata mwanga, msamaha, na matumaini, mahali ambapo kulikuwa na giza, ukosefu wa haki, na hali ya kukata tamaa, hadi kufikia ushindi wa uhakika wa Pasaka, ambapo Mwana wa Mungu kwa kufa kwake aliharibu kifo na kwa kufufuka kwake amewakirimia wanadamu maisha mapya. Kumbe, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni kifungo hai ambacho kinawavuta waamini kuelekea kwenye utukufu wa mbinguni; kinapanua upeo wa waamini hata katika maisha haya na kuleta njia ya kufikiri, hisia na kutenda karibu zaidi na kipimo cha Moyo Mtakatifu wa Mungu.Kwa Kristo Yesu kupaa kwake kwenda mbinguni amewaonesha waamini njia ya kwenda kwa Baba yake wa milele. Rej. Yn 14:1-6.
Katika Kristo Yesu, waamini wanapata kutoka ndani mwake zawadi ya maisha, katika mifano na mafundisho yake mintarafu maisha na utume wa Bikira Maria sanjari na ya watakatifu wa Mungu; watu ambao Mama Kanisa anapenda kuwaweka mbele ya macho ya waamini kama mfano bora wa kuigwa, kwani hawa ni kama “Mlango wa jirani” na kwamba, siku zote za maisha yao watu wa Mungu wanajitahidi kuishi kwa dhati kabisa tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, pamoja nao, kwa msaada wao na shukrani kwa sala zao, waamini pia wanaweza kujifunza kupaa siku baada ya siku kuelekea mbinguni, huku waamini wakilifanya kuwa ni lengo la mawazo yao kama anavyosema Mtakatifu Paulo: “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Yote haya yanapaswa kumwilishwa katika matendo na kwa njia ya msaada wa Mwenyezi Mungu, kile ambacho wamesikia na kuona yasaidie kufanya maisha ya utakatifu kila wakati kuwa karibu nao zaidi, ili hatimaye, waweze kukuza ndani mwao maisha ya kimungu ndani mwao ; kuwavuta juu ili kuelekea kwa Baba wa milele, sanjari na kueneza ulimwenguni pote matunda ya thamani ya ushirika na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anamwomba Bikira Maria Malkingi wa Mbingu, aweze kuwasaidia kwani yeye kila wakati anawaangazia njia sanjari la kuwaongoza.