Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Wasimamizi wa Mji wa Roma

Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Watakatifu Petro na Paulo ni Wasimamizi na Waombezi wa Mji wa Roma, Sherehe inayounganisha umoja wa imani na Injili ya upendo kwa Kanisa la Roma na kwa Makanisa yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Ni watakatifu waliomshuhudia Kristo Yesu kwa maisha na Neno walilolitangaza duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Sherehe ya Watakatifu Petro aliyeteuliwa na Kristo Yesu kuwa Mchungaji mkuu wa Kondoo wake na Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa; wote wawili ni Miamba wa imani ya Kanisa, Jumatatu tarehe 29 Juni 2026, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, akabariki Pallio Takatifu na kuwavisha Maaskofu wakuu wapya 35 walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2025-2026. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Watakatifu Petro na Paulo ni Wasimamizi na Waombezi wa Mji wa Roma, Sherehe inayounganisha umoja wa imani na Injili ya upendo kwa Kanisa la Roma na kwa Makanisa yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni Mitume waliofunga Agano Jipya na la Milele kwa kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo amewavisha Maaskofu wakuu Pallio.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo amewavisha Maaskofu wakuu Pallio.   (@Vatican Media)

Ni kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na Neno la Mungu walilolitangaza na kulishuhudia, wakaonesha kwamba, Injili ya Kristo kwa hakika ni chachu ya mabadiliko; ni chanzo cha maarifa mapya ya kumfahamu Mwenyezi Mungu, tayari kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwanzo mpya kwa waamini kugundua na kutambua kwamba fadhila ya nguvu si kwa ajili ya kuwatala na kuwamiliki wengine, bali inapaswa kuelekeza kwa ajili ya kuhudumia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hata leo hii katika Ulimwengu mamboleo, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka, anendelea kung’ra katika shuhuda mbalimbali zinazotolewa na waamini wake, kiasi cha kuwafikia watu sehemu mbalimbali za maisha. Mchakato huu unatendeka kwa njia ya sauti zao za kibinadamu, ufunuo wa nyuso zao mambo yanayotekelezwa kwa dhati kabisa na wale waliokubali kuteuliwa na Kristo Yesu ili waweze kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajumbe wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Papa Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, 29 Juni 2026
Papa Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, 29 Juni 2026   (ANSA)

Utume wa Petro na Paulo unabubujika kutoka katika maisha na utume wa Kristo Yesu na kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaaminisha waja wake utume huu, kwa sababu kama wadhambi wamesamehewa dhambi zao na kwamba, historia ya maisha yao, neema, baraka na nguvu vinajidhihirisha katika ile nguvu ya kubadilisha ubaya kuwa ni wema. Watakatifu Petro na Paulo ni watu waliokuwa na tofauti kubwa katika maisha na utume wao. Walikuwa na asili tofauti, malezi, makuzi na majiundo yao yalitofautiana kwa kina na mapana. Ni watau waliokuwa na tabia tofauti kabisa, kabla ya kuitwa na Kristo Yesu na hata baada ya kupewa dhamana na majukumu ya kutekeleza. Lakini yote haya ni tisa, kumi ni kwamba, wote wawili wamefundwa na kuunganishwa na Kristo Yesu, na wakawa ni vyombo na mashuhuda wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika utofauti wao, lakini yote ni Habari Njema ya Wokovu.

Mtakatifu Petro na Mt. Paulo walitumwaa kutangaza na kushuhudia Injili
Mtakatifu Petro na Mt. Paulo walitumwaa kutangaza na kushuhudia Injili   (@Vatican Media)

Watakatifu Petro na Paulo katika Baraza la Mitume wa Yesu walionekana kuwa ni mashuhuda wa umoja na ushirika na kwamba, wakiwa mjini Roma, wameshiriki kutangaza na kushuhudia Sakramenti ya Maisha ya Kimungu. Ushuhuda wa maisha yao angavu umewafanya Wakristo kujipambanua kuwa ni watu wa huduma, umoja na upatanisho na wala si kwa ajili ya uchu wa madaraka ya kutaka kuwatala wengine. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kwa maombezi ya watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, wawasaidie waamini kuelewa maana ya Ukatoliki wao, watambue na kuthamini Injili ya huduma inayosimikwa kwa watu kukutana na hivyo kujiepusha na mambo yanayoleta mtafaruku na mgawanyiko; wakristo waendelee kujielekeza katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini katika ukweli na uwazi. Bikira Maria Malkia wa Mitune, aendelee kuwalinda watu watakatifu wa Mungu waliko mjini Roma na sehemu mbalimbali za dunia.

Sherehe ya Mitume
29 Juni 2026, 15:48

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >