Tafuta

Papa wakati wa sala ya Malaika wa Bwana huko Castel Gandolfo tarehe 15 Agosti 2026. Papa wakati wa sala ya Malaika wa Bwana huko Castel Gandolfo tarehe 15 Agosti 2026.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV:Kupalizwa kwa Maria ni kukumbusha Wakristo uzima wa milele pamoja na Mungu

Kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana katika Sherehe ya Kupalizwa kwa Maria Mbinguni,Agosti 15 Papa Leo XIV akiwa katika Lango la Nyumba ya Kipapa huko Castel Gandolfo alitafakari taswira za kiutamaduni za Watu wa Mungu katika Kupalizwa kwa Bikira Maria: “Kupalizwa kwa Maria kunaonesha hatima yetu ya milele.Mfano huu unaoakisi ukweli kwamba Maria alichukuliwa mwilini na roho katika uadilifu wa nafsi yake."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kupalizwa mbinguni kwa Maria ni Sherehe yenye umuhimu mkubwa, kwa ajili ya taalimungu Katoliki  na kwa ajili ya uchaji wa watu; ambapo kiukweli, ni sherehe inayohusishwa sana katika Jumuiya nyingi, hasa pale ambapo Kanisa Kuu au Kanisa la Parokia limetengwa kwa ajili ya Kupalizwa  Bikira Maria. Ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV alifafanua wakati wa Tafakari yake kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana katika Sherehe za Kupalizwa Mbinguni kwa Bikira Maria, tarehe 15 Agosti 2026, akiwa katika Lango Kuu la Nyumba ya Kipapa huko Castel Gandolfo.

Ibada za Mama Maria,Kulala na kupaliza

Papa Leo XIV alieleza kuwa ili kutafakari fumbo hili la imani, tunaweza kugeukia mifano miwili ya sanamu ambayo wasanii wameionesha kwa karne nyingi. Akianza kudadavua alisema " ya kwanza, ya zamani zaidi, na ya pekee kwa karibu milenia, ni ile ya "kulala" kwa Mama wa Mungu: Anaonekana ameegemea kwenye jeneza, amelala katika kifo; karibu naye wapo  Mitume, wakimheshimu, wakiwa katika sala; katikati, aliyesimama, ni Yesu mfufuka, akiwa ameshika roho ya Maria mikononi mwake, kama mtoto mchanga. Alikuja kumchukua pamoja naye kwa utukufu wa Mungu, "mbinguni," kama tunavyosema kwa mfano. Hakika, Bwana alitimiza kwa Mama yake kile alichoahidi kwa marafiki zake wote: "Nitakapokenda kwa Baba na kuwaandalia makao, nitakuja tena niwachukue kwangu" (Yh 14:3).

PAPA HUKO CASTEL GANDOLFO
PAPA HUKO CASTEL GANDOLFO   (@VATICAN MEDIA)

Kristo alikufa na kufufuka

Mfano huu wa kwanza unaakisi ukweli mkuu Papa alisema: "ni Kristo, aliyekufa na kufufuka, ambaye anatuongoza kwenye lengo ambalo tumekuwa tukikusudiwa kila wakati yaani: uzima wa milele. Hili ndilo vizazi na vizazi vya waamini vimefikiria, walipokuwa wakisali mbele ya sanamu za Kulala kwa Maria, na ambalo linaweza kuonekana huko Roma, katika picha nzuri kubwa iliyo karibu na Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu (Santa Maria Maggiore.)

WAAMINI WAKISIKILIZA TAFAKARI
WAAMINI WAKISIKILIZA TAFAKARI   (@VATICAN MEDIA)

Ishara kuu ilonekana Mbinguni

Picha za hivi karibuni zaidi, ambazo zilitokea baadaye Magharibi, badala yake  Papa alisema "zinatuonesha Bikira Maria akiwa na umbo kamili mbinguni, akiwa amefunikwa na nuru, mara nyingi akiwa amezungukwa na malaika na watakatifu." Hapa, mwili mtukufu wa Mama uko katikati, kulingana na kile tunachosoma katika Kitabu cha Ufunuo: "Ishara kubwa ilionekana mbinguni: mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili kichwani mwake" (Ufu. 12:1). Baadhi ya wasanii wamechanganya mipango hiyo miwili, inayoonesha Bikira mtakatifu juu na kaburi lake tupu, mara nyingi likiwa limejaa maua ya rangi nyingi, chini, huku Mitume wakimtazama mbinguni.

Ukweli wa Mama Maria kupaa katika mwili na roho

Mfano huu wa pili unaakisi ukweli kwamba Maria alichukuliwa mwili na roho, yaani, katika uadilifu wa nafsi yake. Mwanamke huyo ambaye duniani alitoa mwili na damu kwa Neno aliyefanyika mwili na kumfuata kwa umoja kamili katika sadaka  ya upendo, alivutwa kwake milele katika utukufu.

PAPA AKIWABARIKI WAAMINI
PAPA AKIWABARIKI WAAMINI   (@Vatican Media)

Picha hii inatafakarisha hatima yetu

Kwa hivyo, Papa alisisitiza taswira hii pia inaturuhusu kutafakari hatima yetu ya mwisho. Ukamilifu wa maisha, ambao tunausifu kwa furaha katika Maria leo, pia unatungojea mwishoni mwa wakati, wakati, kama Mtakatifu Paulo asemavyo, Kristo Mfufuka "atabadilisha miili yetu ya unyonge ili ifananishwe na mwili wake wa utukufu" (Flp 3:21), akivika kile kinachoharibika kwa kutoharibika na kile kinachokufa kwa kutokufa (taz. 1 Kor 15:54). Kisha, miili yetu ikiwa imebadilishwa kwa upendo wa Mkombozi, tutaishi milele, katika sherehe isiyoisha. Tumsifu Bwana, ambaye amefanya mambo makuu katika Mama yake na Mama yetu Mtakatifu sana," Papa Leo XIV alihitimisha.

TAFAKARI YA PAPA KABLA YA SALA AGOSTI 15

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

15 Agosti 2026, 12:29