Kard.Parolin:Padre Pio ni Mtakatifu wa sasa,pamoja naye,tuombe amani
Isabella H. de Carvalho na Angella Rwezaula - Vatican – Vatican.
Padre Pio wa Pietrelcina ni Mtakatifu wa wakati wetu, mtakatifu wa kisasa, mtu wa kipekee, mpendwa na watu wa nchi nyingi, ambaye anaacha urithi muhimu wa kiroho kwa ulimwengu wa leo; na tukikumbuka maneno yake, 'sala ndiyo silaha bora zaidi tuliyo nayo,' tunaombe zaidi ya yote kwa ajili ya amani. Hivi ndivyo alianza kumfafanua Katibu Mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin akimkumbuka Padre mashuhuri Mkapuchini, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbukumbu yake ya kiliturujia iliyoadhimishwa tarehe 23 Septemba 2025 katika Kanisa la Roma la Mtakatifu Salvatore huko Lauro. Parokia hiyo, ambayo ina makumbusho yenye masalia ya Padre aliyekuwa na madonda, ilikuwa imejaa waamini.
Licha ya mvua kunyesha, waliohudhuria sherehe hizo walijaza Uwanja wa mbele ambao ulikuwa umewekwa viti na vipaza sauti ili kuruhusu kila mtu kufuatilia ibada hiyo. Wawakilishi wengi wa Idara ya Ulinzi wa Raia wa Italia, ambaye mlinzi wake, pia walikuwepo. "Mtakatifu anayefundisha jinsi wakati wetu unahitaji kugundua tena thamani ya hali ya kiroho ya msalaba ili kufungua mioyo yetu, hasa katika Mwaka huu wa Jubilei unaoadhimishwa na tumaini ambalo halikatishi tamaa," Kardinali Parolin alisisitiza.
![]()
Kardinali Parolin wakati wa misa katika siku kuu ya Mtakatifu Padre Pio
Mateso na sala
Wakati wa Misa, Katibu Mkuu wa Vatican aliakisi mambo matatu ya utakatifu wa Padre Pio: mateso, sala, na matukio ya kiroho. Akitoa mfano wa mahubiri ya Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa kutangazwa kwake kuwa Mtakatifu mwaka 2002, Kardinali Parolin alisisitiza umuhimu wa kiroho wa Msalaba alichoishi Mkapuchini mnyenyekevu na jinsi tunavyoweza kujifunza kutoka kwake thamani ya kuokoa ya mateso. Mtakatifu huyo alikuwa na uhusiano wa karibu kati ya mateso na upendo na akatoa maumivu yake ya kimwili na ya kiroho kwa ajili ya wokovu wa roho. Kwa Kardinali Parolin, aliongeza kuwa "kuhani kutoka San Giovanni Rotondo ni mfano wa sala, akionesha jinsi ulivyo ufunguo unaofungua moyo kwa Mungu."
Kwa kusisitiza zaidi alisema "pia alikuwa mtu thabiti sana, ambaye alijua jinsi ya kupima wakati na namna ya kuomba, pia akitoa ushauri wa vitendo kama vile kutoendelea wakati roho na akili haziko tayari." Kadhalika " Si kutia chumvi kusema kwamba Padre Pio anachukua nafasi ya umuhimu mkubwa katika mfululizo wa sala kuu za kiroho cha Kikristo," alisisitiza Kardinali Parolin.
![]()
Mahali palipo na aina za masalia mbalimbali ya Padre Pio katika Kanisa la Mtakatifu Salvatore huko Lauro jijini Roma
Mtakatifu anayedhihirisha Utajiri wa Injili
Hatimaye, Katibu Mkuu wa Vatican aliakisi matukio ya kiroho ya Padre Mkapuchini, kama vile "maono yake, madonda na eneo lake." Alisema kwamba licha ya "kutomuelewa kwa wengi, Mtakatifu Pio alikubali kwa utiifu wa unyenyekevu, kwa usadikisho mkubwa kwamba Mungu angeruhusu ukweli ushinde katika wakati wake, na ndivyo ilivyokuwa wakati Kanisa lilipomtangaza kuwa Mtakatifu." Katika maisha ya watakatifu, utajiri wa Injili unadhihirishwa. Haya ni mapito yenye kung'aa ya Mungu ambayo Yeye Mwenyewe amefuatilia na anaendelea kufuatilia katika historia na hivi ndivyo Padre Pio alivyokuwa, "Kardinali Parolin alihitimisha.
![]()
Kardinali Parolin wakati wa kufika kwa ajili ya Misa ya Siku kuu ya Padre Pio.