Tafuta

PORTUGAL-VATICAN-POPE-RELIGION-WYD

Afrika:Kiswahili kwa asili yake ni lugha ya amani na biashara,Balozi Togolani Mavura

"Lugha ya Kiswahili ina maneno machache ya kugombana lakini ina maneno mengi ya maridhiano na imetusaidia Afrika Mashariki.Ni lugha ya biashara kwa asili yake.” Alisema hayo Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Togolani Mavura,katifa fursa ya Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili,Julai 7.Na Dk.Asiimwe,Katibu Mtendaji(EAKC)na mjumbe wa UNESCO:"Nguvu kubwa ipo katika uwezo wake wa kuwaunganisha watu huku ikihifadhi utofauti."

Habari za Umoja wa Mataifa(UN).

Kiswahili, ambacho kilitambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO)mwaka 2021 kama lugha ya kwanza ya Afrika kuwa na Siku ya Kimataifa iliyoteuliwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa, leo hii kinaunganisha zaidi ya wasemaji milioni 200 barani Afrika na kwingineko, kikihudumu kama daraja kati ya jamii, tamaduni na vizazi. Kwa mwaka 2026 siku hiyo iliongozwa na Kaulimbiu: "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Dunia."  Ni katika muktadha huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Togolani Mavura alifafanua zaidi kuhusu ni kwa namna gani lugha ya Kiswahili inaweza kuyafanikisha hayo. Balozi Mavura alisema, “Kiswahili kwa asili yake ni lugha ya amani. Ni vigumu kugombana na lugha ya Kiswahili.”


Kiswahili ni lugha ya biashara

Bwana Togolani alifafanua kuwa lugha ya Kiswahili ina maneno machache ya kugombana lakini ina maneno mengi ya maridhiano na aliongeza, “kwa ajili hiyo ni lugha ambayo imetusaidia sana katika eneo letu la Afrika Mashariki kwa sababu pia ni lugha ya biashara kwa asili yake. Ni lugha ya watu waliokutana kutoka katika maeneo mbalimbali. Ilikuwa lugha ya kuwaunganisha watu. Kwa hiyo Kiswahili ni lugha daraja na si lugha ya kutenganisha watu.” Bwana Togolani alisema katika jumuiya za kiuchumi ambazo zimefanikiwa sana barani Afrika ni Jumuiya ya Afrika Mashariki, “na moja ya siri yake ni kwa sababu inatumia lugha ya Kiswahili.”

Wazungumzao hawagombani

Balozi Togolani Mavura anaamini katika msemo wa Waswahili usemao: ‘Wazungumzao hawagombani’ na kwa hivyo alisema, “kwa hiyo tunaamini kwamba kadiri Kiswahili kitakavyopanuka kwenda kwenye maeneo mengine ndivyo amani itapanuka kwenda kwenye maeneo mengi na ndio maana lugha ya Kiswahili inatumika katika majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani.”

Kiswahili ni daraja la utofauti wa kitamaduni,mazungumzo na ubunifu wa kidijitali

Kwa upande wa Dk. Caroline Asiimwe, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC) na mjumbe wa timu ya wataalamu ya UNESCO ya Kamusi ya Akili Unde  ya Kiingereza–Kiswahili, nguvu kubwa ya Kiswahili ipo katika uwezo wake wa kuwaunganisha watu huku kikihifadhi utofauti. “Kiswahili kimejengwa kwa namna ya kipekee kama alama ya umoja, amani na uelewano wa pamoja,” alisema. “Kwa sababu hakimilikiwi na kabila moja, kinaunda nafasi isiyo na upendeleo wa lugha ambapo tamaduni tofauti zinaweza kukutana bila ubabe wa lugha.” Kiswahili kilichotokana na karne nyingi za mwingiliano katika pwani ya Afrika Mashariki, kimekuzwa kupitia biashara, mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano.

Katika historia yake yote, kimekopa msamiati kutoka jamii mbalimbali huku kikihifadhi utambulisho wake wa Kiafrika, na hivyo kuwa mfano hai wa mazungumzo ya kitamaduni. Leo, lugha hii ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiimarisha ushirikiano wa kikanda huku ikiunga mkono matumizi ya lugha nyingi. Tangu Novemba 2025, pia imekuwa lugha rasmi ya saba ya Mkutano Mkuu wa UNESCO, ikiungana na Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania. Badala ya kuchukua nafasi ya lugha za asili, Dk. Asiimwe anaamini Kiswahili kinazisaidia kwa kuwezesha watu kutumia lugha zao za mama ndani ya jamii zao, Kiswahili kwa mawasiliano ya kikanda, na lugha za kimataifa kwa mawasiliano ya kimataifa.


Kuimarisha lugha nyingi kupitia ubunifu wa kidijitali

Wakati akili Unde (AI) ikibadilisha jamii, UNESCO inafanya kazi kuhakikisha lugha za Afrika zinakuwa sehemu ya mustakabali wa kidijitali. Mwaka 2025, UNESCO ilizindua Kamusi ya Akili unde ya Kiingereza–Kiswahili, iliyotengenezwa kupitia mchakato wa ushirikiano uliowahusisha wanaisimu, wataalamu wa AI na wataalamu wa lugha. Rasilimali hii ya mtandaoni inayobadilika inaeleza na kutafsiri istilahi muhimu za akili unde hadi sasa ikiwa na istilahi 109 za msingi za AI kwa Kiingereza na Kiswahili, ikiwasaidia wanafunzi, walimu, watafiti, watunga sera na wavumbuzi kuelewa dhana za AI zinazobadilika kwa kasi kwa njia rahisi na inayofikika.

Akiwa mjumbe wa timu ya wataalamu ya UNESCO iliyochangia kamusi hiyo, Dk. Asiimwe anasema mpango huo ni zaidi ya kamusi ya kawaida. “Kamusi za jadi zinanasa lugha iliyosimama, kamusi hii ya AI ni nyenzo hai inayobadilika,” anaeleza. Inavuka tafsiri ya moja kwa moja kwa kunasa muktadha, nahau na muktadha wa kitamaduni, ikisaidia kuhakikisha maana ya dhana haipotei.” Kamusi hiyo pia inachangia juhudi pana za UNESCO za kupunguza vizuizi vya lugha katika ulimwengu wa kidijitali na kufanya teknolojia zinazoibuka ziwe rahisi kufikiwa na wazungumzaji wa lugha zisizo na rasilimali kubwa za kidijitali.

Kwa kutoa istilahi sanifu za AI kwa Kiswahili, inaunga mkono elimu, utafiti, ubunifu na maendeleo ya AI yenye maadili katika eneo hili. Dk Asiimwe anasisitiza kuwa akili unde inaweza kuwa nyenzo yenye nguvu ya kuhifadhi na kukuza Kiswahili, iwapo itajengwa kwa kutumia data ya lugha ya ubora wa juu na inayohusiana na mazingira ya ndani. “Mifumo ya AI lazima ioneshe utajiri na mabadiliko ya Kiswahili,” anasema. “Hii inamaanisha kuendelea kujumuisha fasihi ya kisasa, vyombo vya habari, maoni ya jamii na misemo ya kikanda ili teknolojia iheshimu mazingira ya Kiafrika badala ya kutafsiri maneno tu.”

Lugha inayokua kimataifa

Utambuzi wa kimataifa wa Kiswahili unaakisi kuongezeka kwa ushawishi wake zaidi ya Afrika. Lugha hii inazidi kufundishwa katika vyuo vikuu duniani, na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaaluma, mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano wa kiuchumi. Kwa wazungumzaji wengi, kuongezeka kwa umaarufu huu pia kunawakilisha kutambuliwa kwa thamani ya kiakili na kitamaduni ya lugha za Afrika. Uteuzi wa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili umehamasisha mashirika ya kimataifa, taasisi za elimu, wachapishaji na wavumbuzi wa kidijitali kuwekeza katika lugha hiyo. Kulingana na Dk. Asiimwe, UNESCO imekuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko haya kwa kukuza Kiswahili kama lugha ya ujumuishi na mazungumzo. “Kimekipandisha Kiswahili kutoka kuwa lugha ya kikanda ya mawasiliano hadi kuwa chombo muhimu cha amani, maendeleo endelevu na urithi wa pamoja wa kiutamaduni,” anasema.

Wakati UNESCO ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili, Shirika hilo linathibitisha tena kujitolea kwake kwa lugha nyingi na utofauti wa lugha kama msingi muhimu wa jamii jumuishi za maarifa. Katika zama za kidijitali, mipango kama Kamusi ya Akili unde ya Kiingereza–Kiswahili inaonesha jinsi teknolojia inavyoweza kulinda lugha huku ikipanua upatikanaji wa elimu, ubunifu na mazungumzo ya kitamaduni. Kwa Dk. Asiimwe, dira iko wazi: “Kiswahili kinapaswa kuwa mstari wa mbele katika mabadiliko ya kidijitali ya kimataifa. Kinapopanuka katika majukwaa ya kimataifa, kinaweza kukuza uelewano wa kina kati ya tamaduni, kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuhakikisha sauti za Afrika zinakuwa washirika sawa katika kuunda mustakabali wetu wa kidijitali wa pamoja.”  

Imesasishwa tarehe 8 Julai 2026 na Angella Rwezaula.

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

08 Julai 2026, 11:24